Liverpool yachezea kichapo tena kipa akiongeza presha
Muktasari:
- Liverpool inaongoza msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa na pointi 15 ilizokusanya katika michezo sita.
Liverpool imepokea kichapo cha bao 1-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ugenini dhidi ya Galatasaray ya Uturuki jana Jumanne Septemba 30, 2025 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Rams Park, Istanbul.
Kipigo hicho ni cha pili mfululizo msimu huu baada ya Jumamosi iliyopita kutandikwa mabao 2-1 na Crystal Palace katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL).
Bao pekee la Victor Osimhen ambalo lilitokana na mkwaju wa penalti, lilitosha kuipa ushindi Galatasaray ambayo iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Eintracht Frankfurt kwa mabao 5-1.
Ni mchezo ambao haukumalizika vizuri kwa Liverpool kwani kipa wake tegemeo Allison alipata majeraha ambayo yalilazimisha atolewe katika dakika ya 56 kumpisha Giorgi Mamardashvili.
Chelsea ilitumia vyema Uwanja wake wa nyumbani wa Stamford Bridge kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Benfica ambalo lilitokana na Richard Rios wa timu pinzani kujifunga katika dakika ya 18 ya mchezo.
Eintracht Frankfurt ambayo iliifunga Galatasaray mabao 5-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, imejikuta nayo ikipokea kichapo kama hicho kutoka kwa Atletico Madrid katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitan.
Wafungaji wa Atletico Madrid walikuwa ni Julian Alvarez, Giuliano Simeone, Antoine Griezmann, Robin Le Normand na Giacomo Raspadori
Ikiwa ugenini dhidi ya Kairat Almaty, Real Madrid ilitoa kichapo kizito cha mabao 5-0 ambapo Kylian Mbappe alipachika mabao matatu huku mengine yakifungwa na Brahimi Diaz na Eduardo Camavinga.
Nchini Cyprus, Harry Kane aliiongoza Bayern Munich kuiangamiza Pafos kwa mabao 5-1 ambapo yeye alipachika mabao mawili huku mengine yakifungwa na Michael Olise, Nicolas Jackson na Raphael Guerreiro.
Kwingineko, Bodo/Glimt ilitoka sare ya mabao 2-2, Inter Milan ikashinda mabao 3-0 dhidi ya Slavia Prague, Marseille ikaichapa Ajax mabao 4-0 na Atalanta ikashinda mabao 2-1 dhidi ya Club Brugge.