Liverpool yamalizana na Hugo Ekitike
Muktasari:
- Ekitike, alifunga mabao 22 katika mechi 48 msimu uliopita akiwa Frankfurt.
Liverpool, England. Liverpool imekamilisha makubaliano ya kumsajili mshambuliaji chipukizi anayeng’ara barani Ulaya, Hugo Ekitike, kwa mkataba unaoweza kufikia hadi pauni milioni 79 (Sh276 bilioni) ikiwa ni sehemu ya matumizi yao makubwa ya usajili msimu huu wa kiangazi.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka England, Liverpool imekubali kutoa pauni milioni 69 kama ada ya awali, pamoja na milioni 10 nyingine kama nyongeza kulingana na mafanikio ya mchezaji na timu. Ekitike, ambaye msimu uliopita aling'ara akiwa Eintracht Frankfurt, anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya ndani ya siku chache zijazo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Ekitike alikataa kujiunga na Newcastle, licha ya klabu hiyo kutoa ofa ya pauni milioni 70 ambayo ilikataliwa kwa kuwa ilikuwa chini ya kipengele cha kuachia mkataba wake.
Liverpool sasa imefikisha matumizi ya jumla ya pauni milioni 289 katika dirisha hili la usajili, baada ya pia kuwasajili Florian Wirtz, Jeremie Frimpong, Milos Kerkez, na Giorgi Mamardashvili. Ekitike anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa rasmi msimu huu.
Wirtz, aliyesajiliwa kwa ada ya rekodi ya klabu ya pauni milioni 116 kutoka Bayer Leverkusen, alipata dakika zake za kwanza katika mechi ya kirafiki dhidi ya Stoke City iliyomalizika kwa ushindi wa 5-0. Kikosi cha Arne Slot kiliondoka kuelekea kwenye ziara ya maandalizi barani Asia (Hong Kong na Japan) usiku wa Jumapili, na Ekitike anatarajiwa kujiunga nao pindi tu taratibu za usajili zitakapokamilika.
Ekitike, ambaye alifunga mabao 22 katika mechi 48 msimu uliopita akiwa Frankfurt, alitangazwa kwenye kikosi bora cha Bundesliga.
Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya vijana ya Ufaransa chini ya miaka 21 aliwahi pia kusajiliwa na Paris Saint-Germain kutoka Reims, lakini hakupata nafasi ya kung’ara kwa kiasi kikubwa, akicheza mechi 33 tu na kufunga mabao manne.
Katika dirisha hili la usajili, Liverpool pia imewaaga nyota kadhaa akiwemo Trent Alexander-Arnold aliyekwenda Real Madrid, Jarell Quansah aliyejiunga na Bayer Leverkusen, na Caoimhin Kelleher aliyehamia Brentford.
Klabu hiyo ya Anfield bado haijamaliza shughuli zake za usajili, huku tetesi zikieleza kuwa wachezaji kama Darwin Núñez, Luis Díaz, na Harvey Elliott wanaweza pia kuuzwa kabla ya dirisha kufungwa.