Maeneo haya kuamua mechi ya dabi

Dar es Salaam. Keshokutwa Jumamosi kutakuwa na mchezo wa dabi ya Kariakoo wa 112, huku kila timu ikihitaji pointi muhimu kwenye mchezo huo.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 55 huku Simba ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46, lakini ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja.

Mchezo huu umeonekana kuwa na maana tofauti kwa kila timu, endapo Simba ikishinda itakuwa imerejea kwenye mbio za ubingwa, lakini kama Yanga ikiibuka na ushindi itakuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Hata hivyo, mwenendo wa timu hizo msimu huu umeonekana kuwa tofauti ambapo Yanga imeonekana kushikilia kwenye idara nyingi muhimu, ufungaji na ulinzi lakini bado jambo lolote linaweza kutokea.

Kutokana na mwenendo wa timu hizo kwenye mashindano makubwa ambayo zimeshiriki msimu huu, inaonekana kuwa kila timu inatakiwa kufanya kazi kubwa.

Yanga inaonekana kuwa na kasi nzuri kwenye eneo la ushambuliaji msimu huu ikiwa ndiyo timu inayoongoza kwa kufunga mabao kati ya timu zote 16, ikiwa imeshafunga mara 52 yakiwa ni 12 zaidi ya Simba ambayo imefunga mabao 40, ikishika nafasi ya tatu kwa ufungaji baada ya Azam yenye 49.

Kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu zote zilishiriki eneo hili lilionyesha uwiano sawa baada ya zote kumaliza kwenye hatua ya makundi zikiwa zimefunga mabao tisa kila moja.

Timu hizo ndiyo zilishikilia rekodi ya kufunga idadi kubwa kwenye hatua hiyo msimu huu, lakini kwa kufuata uhalisia wa ligi Simba inatakiwa kuhakikisha inajidhatiti zaidi kwenye eneo hili kwa kuwa Yanga imeonekana kugawa mabao yake kwa wachezaji wengi.

Kwenye chati ya ufungaji wa ligi msimu huu Yanga ina wachezaji watatu kwenye kumi bora, Stephen Aziz Ki anaongoza  akiwa na mabao 14, na pia katika chati hiyo yupo Maxi Nzengeli ambaye anashika nafasi ya nne,  nafasi ya saba yupo Mudathir Yahya mwenye mabao manane.

Lakini hadi nafasi ya kumi hakuna mchezaji yoyote wa Simba zaidi ya Jean Baleke ambaye ameshondoka kwenye timu hiyo, huku Clatous Chama akiwa chini na mabao saba.

Hii inaonyesha kuwa kasi ya Simba kufunga mabao ina tofauti kubwa na ile ya Yanga ambayo ipo kwenye mwendo mzuri, hivyo ni lazima Simba ijidhatiti kwenye eneo la ushambuliaji kwenye mchezo huu.

Eneo la ulinzi nalo litashikilia mchezo huu utakaochezwa Jumamosi kuanzia saa 11:00 jioni, kwa kuwa kama ilivyo kwenye ushambuliaji ndiyo hali ilivyo huku.

Yanga pia imeonekana kuwa kwenye kasi nzuri katika michezo ya Ligi Kuu Bara kwenye eneo la ulinzi ikiwa inashika nafasi ya kwanza kwa timu iliyoruhusu mabao machache baada ya nyavu zake kutikiswa mara 11 tu, Simba ikiwa imefungwa mabao 19 katika nafasi ya tatu pia nyuma ya Azam iliyofungwa mabao 16.
 

Hili ni eneo ambalo pia Simba itatakiwa kuhakikisha haifanyi makosa mengi kwa kuwa michezo minne iliyopita inaonyesha hali siyo nzuri baada ya kuruhusu mabao matano.

Huku upande wa Yanga ikicheza michezo minne mfululizo ya mwisho bila kuruhusu bao kuonyesha kuwa eneo hilo timu hii limekaa vizuri na hivyo ni sehemu nyingine ambayo inashikilia mchezo huu.


Wachezaji wa zamani

Meddie Kagere anasema Dabi haina mazoea na jambo lolote linaweza kutokea uwanjani bila kujali timu gani ilikuwa na matokeo mazuri huko nyuma.

Kiraka wa zamani wa Simba, Erasto Nyoni, alisema dabi anayoikumbuka ni ya msimu wake wa mwisho Msimbazi, Aprili 16, 2023, waliyoshinda mabao 2-0. “Ilikuwa mechi ya ushindani uwanjani, kabla ya mechi yenyewe  wachezaji tulihamasishana, lakini kuhusu mechi ya Aprili 20, haina mwenyewe.”

Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya  FC Lubumbashi Sport ya DR Congo anasema: “Dabi haina nani yupo vizuri nani yupo vibaya, msimu wa 2018/19 Simba ilikuwa na kikosi cha moto, lakini tulipambana tukatoka suluhu.”