Magera Cup kuliamsha Rock City, timu nane kukinukisha

Muktasari:

Katika uzinduzi huo, timu shiriki zimegawiwa vifaa vya michezo huku zikipigwa pia mechi mbili kuashiria kuanza kwa michuano hiyo ambayo itakuwa inafanyika kwenye uwanja wa Babptist Kona ya Bwiru jijini humo.

Baada ya kimya cha muda mrefu kwa wakazi wa Jiji la Mwanza kukosa burudani ya soka la mchangani ‘ndondo’ mdau wa soka, Hussein Magera ameamua kuwasogezea uhondo huo kwa kuanzisha ligi ya Magera Cup ambapo bingwa ataondoka na Sh 300,000.

Jumla ya timu nane zinatarajia kushiriki michuano hiyo ambayo itaanza rasmi Jumatano kwa kushuhudia First Born FC na Ibungiro Stars zikikata utepe kuanza kusaka ubingwa wa ligi hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, muandaaji wa ligi hiyo, Magera ambaye ni Diwani wa kata ya Ibungiro amesema ikiwa ni mara ya kwanza kuanzisha michuano hiyo anahitaji kuona mabadiliko kwenye soka jijini Mwanza.

Amesema katika kuhakikisha anafikia malengo hayo, ameamua kuweka zawadi nono ambapo bingwa atapata Sh 300,000, wa pili Sh 250,000 na wa tatu akitanua na Sh 150,000, huku mfungaji na mchezaji bora wakiamsha na Sh 50,000 kila mmoja sawa na timu ya nidhamu.

‘‘Jiji haliwezi kulala hivi hivi, sisi kama wadau na wachezaji wa zamani wa soka lazima tuje na vitu vya kulichangamsha jiji, lakini kuona vijana wakipata fursa kupitia michezo, sasa kazi inaendelea’’ amesema Magera.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Ilemela (IDFA), Ephraim Majinge amesema kuwapo kwa ligi hiyo ni katika kufikia mikakati yao kwa Wilaya hiyo kuwa na michezo mingi ya kuibua vipaji.

‘‘Wakati tunaingia madarakani hivi karibuni, tuliahidi mpira kuchezwa ili kuibua vipaji lakini kutoa fursa kwa vijana wetu hapa Ilemela, hii ligi ina baraka zote hivyo timu shiriki zijiandae kiushindani’’ amesema Majinge.