Majeruhi Arsenal ni pasua kichwa
Muktasari:
- Pigo la hivi karibuni la timu hiyo ni majeraha ya beki wa kati, William Saliba. Mfaransa huyo alitolewa katika dakika za mwanzo tu kwenye mechi ya kipigo kutoka kwa Liverpool, Jumapili iliyopita.
LONDON, ENGLAND: MSIMU wa Ligi Kuu England umeanza vibaya kwa chama la Emirates, Arsenal. Si tu kwamba itakuwa na ratiba yenye mechi nyingi ngumu, bali pia kuongezeka kwa idadi kubwa ya wachezaji wao muhimu kuwa majeruhi.
Pigo la hivi karibuni la timu hiyo ni majeraha ya beki wa kati, William Saliba. Mfaransa huyo alitolewa katika dakika za mwanzo tu kwenye mechi ya kipigo kutoka kwa Liverpool, Jumapili iliyopita.
Na kutokana na hilo, Saliba ameondoshwa pia kwenye kikosi cha Ufaransa kitakachokuwa na majukumu ya mechi za kimataifa. Kinachomsumbua ni maumivu ya enka ya mguu wa kushoto.
Winga matata, Bukayo Saka ni mchezaji mwingine muhimu kwenye kikosi cha Arsenal, ambaye ni majeruhi. Staa huyo alipatwa na maumivu ya misuli ya paja kwenye mechi dhidi ya Leeds United na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja hadi Oktoba.
Wakati huo huo, fowadi Mjerumani, Kai Havertz naye yupo kwenye orodha hiyo ya wachezaji majeruhi kwenye kikosi cha Arsenal. Staa huyo, ambaye alitokea kufanyiwa upasuaji ambao uliomfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu kwa msimu uliopita, ameumia tena kwenye mechi za mwanzo wa msimu huu.
Lakini, kocha Mikel Arteta anaamini Havertz hana muda mrefu atarejea uwanjani, aliposema: "Nadhani zitakuwa wiki tu, sijui kama itafika miezi. Ni bahati mbaya kwake, alikuwa akipona kwenye majeraha yaliyopita, amepata mengine. Ndivyo ilivyo kwenye hii kazi yetu.
"Tunaishi kwa kuzoea hilo. Ni kawaida kupoteza mchezaji mwingine mkubwa kwa muda mrefu.”
Habari njema kwenye kikosi cha Arsenal ni kuhusu mastaa Martin Odegaard, Christian Norgaard na Ben White. Nahodha, Odegaard alianzia benchini kwenye mechi dhidi ya Liverpool na kuingia katika dakika za mwisho kutokana na kuwa majeruhi, wakati Norgaard na White wanatarajia kurudi uwanjani baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Lakini, mchezaji ambaye hatazamiwi kurejea uwanjani kwa siku za hivi karibuni, Gabriel Jesus, ambaye amekuwa nje ya uwanja tangu Januari baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, jambo hilo limesababisha hadi jina lake kuondolewa kwenye kikosi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya.