Majiha awatoa kwenye reli Kiduku, Mwakinyo
Dar es Salaam. Ni Fadhil Majiha! Huyu ndiye 'mwamba' wa masumbwi kwa sasa nchini akiwatoa kwenye reli nyota wote, akiwamo Twaha 'Kiduku' Kassim na Hassan Mwakinyo.
Majiha, ambaye ndiye namba moja kwenye kila uzani 'pound for pound' ya Tanzania akiwa bondia pekee aliyesalia na nyota tatu kwenye ubora wa kimataifa.
Kwa mujibu wa viwango vya mtandao wa ngumi za kulipwa wa Dunia (Boxrec), Majiha, bondia aliyewahi kuzichapa ulingo mmoja na Manny Pacquiao nchini China, akimsafishia ulingo kwenye pambano la utangulizi, ndiye 'mkali wao' akiwa na rekodi ya kuwa namba moja kwenye uzani wake wa super fly na kwenye 'pound for pound' ya Tanzania.
Rekodi hiyo imechangizwa na mapambano yake sita ya mwisho, hajawahi kupigwa tangu Oktoba 2019, hadi Juni mwaka huu, akiwa wa 19 duniani kati ya mabondia 744 kwenye uzani wake wake.
Mwenyewe ameweka mikakati ya kutotoka kileleni, akisisitiza kutaka kucheza na mabondia wakali, wenye viwango vya juu ili kuzidi kujiimarisha kileleni zaidi.
"Kama kuna promota anaweza kuniletea mabondia wakali, afanye hivyo, niko tayari hata kufia ulingoni, lakini sitaki kucheza na wabovu (wenye viwango vya chini)," alisema Majiha, ambaye anajiandaa kupandisha uzani kutoka bantam hadi super bantam ili kupanta nafasi ya kupigana na mabondia wakali wa ndani na nje ya nchi.
Kiduku, Mwakinyo walivyoporomoka
Mtandao huo umeanisha mabondia bora nchini, Mwakinyo akiporomoka kwa mara nyingine tena kutoka nafasi ya tatu hadi ya sita, ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Kiduku, ambaye naye ameporomoka hadi nafasi ya 14 kwenye pound for pound.
Licha ya kushinda kwa pointi, Aprili 23, dhidi ya Kuvesa Katembo, matokeo hayo hayajasaidia kumpandisha Mwakinyo kwenye renki, akiwa na kumbukumbu ya kupigwa na Liam Smith kwa TKO, Septemba mwaka jana.
Hadi jana mchana, Mwakinyo alikuwa ni wa 108 duniani kwenye uzani wake, akiwa na panda shuka tangu Septemba 2018, alipopanda hadi nafasi ya 14 kwa kumchapa Sam Eggington kwa TKO.
Kiduku ni wa 92 duniani, akiporomoka kwenye uzani wake nchini hadi nafasi ya pili, kwenye pound for pound na kidunia, huku kipigo cha pointi cha Julai 29, dhidi ya Asemahle Wellem kikimporomosha zaidi.
Kwa nyakati tofauti, Kiduku na Mwakinyo wamewahi kuwa namba moja kwenye pound for pound ya Tanzania, japo Mwakinyo ameendelea kusalia namba moja kwenye uzani wake wa super welter, Kiduku akiporomoka kwenye uzani wa super middle hadi nafasi ya pili akitolewa kileleni na Suleiman Kidunda.
Mabondia wengine walioingia kwenye tatu bora ya pound for pound ya Tanzania ni, Tony Rashid (super bantam) na Ibrahim Class Mgender (super feather), ambao wote wana nyota mbili na nusu, wakitofautiana pointi, sawa na ilivyo kwa Albert Kimario (super bantam), ambaye anashika nafasi ya nne.
Kwenye mabondia wa hadhi ya nyota mbili, kuna Juma Choki (feather) wa nafasi ya tano, Mwakinyo anayepigana uzani wa super welter ni wa sita akifuatiwa na Nasibu Ramadhani (feather), Abeid Zugo (light), Ismail Galiatano (light) na Pius Mpenda (middle) wanahitimisha 10 bora.
Kiduku ni wa 14, akiwa pia na nyota mbili, akiporomoka kwa nafasi tisa, wengine waliompiku ni Loren Japhet, George Bonabucha na Kidunda, ambaye sasa ndiye kinara wa uzani wa super middle.
Nyota mwengine wa ndondi aliyeporomoka kwenye pound for pound ya Tanzania ni Abdallah Paziwapazi (akishuka kwa nafasi 20) na sasa ni wa 38 akiwa na nyota moja.
Mfaume Mfaume amepanda kwa nafasi tatu kutoka ya 35 hadi 32, wakati bondia namba moja kwa heavyweight nchini, Awadh Tamim anayeishi Stockholm, Sweden akichanja mbuga hadi nafasi ya 36.
Chanzo chaanikwa
Licha ya ndondi nchini kuwa na amshaamsha, baadhi ya wadau wametaja mambo matano yanayochangia mabondia hao kuporomoka kimataifa.
"Tutakwenda huko mbeleni, mabondia wetu watakosa soko la nje, watabaki kucheza humu humu nchini," anasema promota maarufu wa ndondi, Jay Msangi.
Msangi hajatofautiana sana na bondia bingwa wa zamani wa dunia, Francis Cheka, ambaye anasema kinachowaangusha wengi ni kupigana na mabondia waliowazidi renki na kushindwa kuwapiga ipasavyo.
Bondia mkongwe, Rashid Matumla aliwahi kusema kunahitajika roho ya 'paka' kucheza ngumi akisisitiza kwamba bondia hatakiwi kuwa muoga na kumhofia mpinzani, zaidi ni kufanya mazoezi tu na ndicho kilimbeba yeye hadi kutwaa mara kadhaa ubingwa wa Dunia wa WBU enzi zake.