Dabi za ndondi za kibabe Bongo

UHONDO wa vitasa, mawe, ndonga au vyovyote utakavyoziita unaaanzia nje ya ulingo na kumalizikia ulingoni.

Pamoja na mashabiki kutamani kuwashuhudia kwenye ulingo mkali wa ndondi, Hassan ‘Champez’ Mwakinyo na Twaha Kassim ‘Kiduku’, wakitarajia kuona moja ya mapambano makali zaidi, lakini yapo yanayotengeza dabi za kibabe za masumbwi nchini.

Wapo mabondia wakizichapa amshaamsha yake baadhi ya mitaa ni lazima ifungwe. Hivi sasa ulimwengu unatamani kushuhudia pambano la wababe wa uzani wa juu raia wa Uingereza, Tyson Fury na Anthony Joshua (AJ).

Lile pambano la Manny Pacquiao na Floyd Maywether lilitengeneza dabi iliyotikisa dunia miaka ya karibuni, ukiachana na zile za miaka ya nyuma ikiwamo ya Mike ‘Iron’ Tyson na Evander ‘The Real Deal’ Holyfield.

Kwa Bongo pia kuna dabi ambazo zikipigwa baadhi ya mitaa hufungwa. Hizi hapa dabi hizo za kibabe nchini.


Pengo vs Mfaume

Hii iliwahi kusababisha mashabiki kupigwa mabomu ya machozi saa chache kabla ya mabondia kupanda ulingoni Uwanja wa Kinesi, Dar.

Habibu Pengo na Mfaume Mfaume waliingia kwenye ‘uhasimu’ baada ya Mfaume kutangaza ufalme wa ndondi wa Mabibo na Manzese anakotokea Pengo, jambo ambalo bondia huyo na timu yake hawakukubaliana nalo hadi zilipochapwa.

Pambano liliwagawa mashabiki ambao wengi wao walifurika uwanjani. ‘Team’ Mabibo na ‘team’ Manzese walitambiana na tambo hizo kukolezwa na mabondia wao, na baada ya raundi 10, Mfaume alitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwa pointi.

Sasa Pengo amerejea Nakos, kambi ya ndondi ya Mabibo ambayo Mfaume ni nahodha wake.

“Bado tuna upinzani, lakini ni wa ulingoni tu,” anasema Mfaume akibainisha kwamba ‘uhasimu’ ulianza baada ya Pengo kuhama Nakos na kujiunga na kambi ya Manzese. Mfaume pia ni mpinzani wa Keis Ally ambaye pambano lao lilifunga baadhi ya mitaa, ingawa Mfaume alishinda kwa pointi.


Kiduku vs Mbabe

Majina yao halisi ni Twaha Kassim ‘Kiduku’ na Abdallah Pazi. Hawa ni mabondia wanaokamata namba moja na mbili kwenye uzani wa super middle.

Ni kama ilivyo kwa Fury na AJ kwenye uzani wa juu Uingereza. Tofauti ni kwamba Kiduku na Mbabe wamezichapa mara mbili na Fury na AJ hawajawahi kuzitwanga. Upinzani ulianza miaka kadhaa iliyopita mabondia hao walipozichapa kwenye Ukumbi wa Msasani Club, Dar es Salaam.

“Najua lile pambano nilishinda, lakini kwa kuwa Mbabe alikuwa nyumbani, majaji wakatoa sare,” anasema Kiduku.

Upinzani wao wa jadi ulianzia hapo, walipitisha miaka kadhaa kila mmoja akijinasibu kuwa bora, hadi walipoandaliwa pambano la marudiano Agosti 28, mwaka jana na Mbabe kuchapwa kwa pointi.

Pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, liliacha gumzo na baadhi ya mashabiki wa Mbabe waliangua kilio hadharani huku likinogesha upinzani baina ya mabondia hao na ‘team’ zao uliodumu mpaka sasa.


Miyeyusho vs Matumla

Japo Mbwana Matumla amestaafu, lakini dabi yake na Francis Miyeyusho haiwezi kusahaulika namna ilivyofunga baadhi ya mitaa ya Dar es Salaam.

Mabondia hao walitengeneza dabi ya Temeke na Kinondoni iliyokuwa ni vita ya piga nikupige wakikutana ulingoni.

“Nakumbuka pambano ambalo nilichukua ubingwa wa dunia Diamond Jubilee nilimchapa Miyeyusho punch ikampeleka chini, raundi hiyohiyo alijibu mashambulizi nikaenda chini, hakuna aliyetaka kuonekana mnyonge,” anasema Mbwana.

Miyeyusho anasema alipokuwa akijiandaa kuzichapa na bondia huyo, kambi yake ililindwa na mashabiki. “Ni dabi ambayo ilikuwa haisemeki, nakumbuka mtaani walikuwa wananipa ulinzi mazoezini sababu tu najiandaa kucheza na Mbwana,” anasema Miyeyusho au Chichi Mawe kama anavyojiita.


Mastiki The Don vs Baina Mazola

Uhasama wao ulitokana na makocha waliokuwa wakiwasimamia, Rama Jaha na Christopher Mzazi.Muksini Swalehe au Mastiki The Don kama anavyopenda kujiita baada ya kutua kwenye kambi ya Nakos chini ya kocha Rama Jaha aliandaliwa pambano na Baina ambaye alikuwa kwa kocha Mzazi.

Pambano hilo liliibua dabi ya Mabibo na Mburahati, japo Baina alichapwa kwa Knock Out pambano hilo lilianzisha dabi nyingine iliyofunga baadhi ya mitaa ya Mabibo kuanzia siku wanapima uzito.


Nasibu vs Majiha

Pambano lao la Juni 9, 2012 lilikuwa gumzo, lakini hadi leo hawajawahi kurudiana.

Fadhil Majiha alichapwa na Nasibu Ramadhan kwa pointi za majaji 2-1 kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese Dar es Salaam, pambano ambalo liliteka hisia za mashabiki, lakini hawakuwahi kurudiana.


Class vs Nasibu

Hii ni dabi ambayo kama itarudiwa itafunga mtaa, sio mashabiki wa Ibrahim Class wala wa Nasibu Ramadhan ambao watakubali kuwa wanyonge, achilia mbali mabondia wenyewe.

Mara ya kwanza walizichapa Agosti mwaka jana, na Class kushinda kwa majaji 2 huku jaji mmoja akitoa droo, japo baadae alidai hakutoa droo na matokeo yake yamechakachuliwa.


Mchumiatumbo vs Ashraf

Japo dabi ya Ashraf Suleiman na Awadh Tamim ilitikisa nchi miaka ya nyuma, Alphonce Mchumiatumbo alikuja kufanya mapinduzi baada ya Awadh kutimkia Sweden. Mabondia hao wa uzani wa juu waliendelea kutikisa na kuwagawa mashabiki hasa waliposaini kuzichapa pambano la raundi sita lililotikisa 2011. Pambano hilo liliisha kwa sare na hawakuwahi kurudiana huku Mchumiatumbo akidai wapinzani wamekuwa wakimkimbia.


Hizi pia zilitikisa

Ukiachana na mapambano ya sasa, baadhi ya dabi za miaka ya nyuma zilizotikisa ilikuwa ni ile ya Rashid Matumla na Joseph Marwa waliowahi kuitumikia klabu ya ndondi ya Simba na Yanga.

Dabi nyingine ni ya Matumla na Maneno Oswald, Stanley Mabesi na Charles Libondo, Karama Nyilawila na Francis Cheka, Japhet Kaseba na Mada Maugo.