Prime
Makocha Afrika wachangangamkia kibarua Simba
Dar es Salaam. Wakati Simba ikiwa katika hatua za mwisho kumpata Kocha Mkuu Mpya, nafasi hiyo imeonekana kuvutia kundi kubwa la makocha wenye wasifu mzuri na baadhi waliopata mafanikio makubwa ndani ya bara la Afrika.
Inaripoti kwamba katika mchakato wa kusaka kocha mkuu mpya, Simba imezingatia zaidi vigezo vitatu.
Kigezo cha kwanza ni leseni ya juu ya ukocha ambayo ni ama ya Daraja A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika au ile ya juu ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA Pro).
"Safari hii hatuko tayari kurudia kosa lililofanyika wakati tunamchukua Pantev. Maombi yamekuwa mengi lakini kama kocha hana leseni inayoruhusiwa kikanuni kuwa Kocha Mkuu kwenye Ligi Kuu au mashindano ya CAF, anapoteza sifa moja kwa moja hata awe amefanya vizuri kiasi gani huko aliko au hata kama ana historia nzuri," kimefichua chanzo ndani ya Simba.
Kigezo cha pili ni uzoefu wa mazingira ya soka la Afrika na kingine ambacho sio muhimu sana ni uzoefu na mafanikio yake ya nyuma.
Baada ya vikao kadhaa vya kupitia wasifu wa makocha mbalimbali ambao wameomba kazin ndani ya Simba, Bodi ya klabu hiyo kwa sasa imebaki na majina takribani 10 ambayo ndio yatatoa Kocha wa kubeba mikoba ya Pantev
Mwananchi Digita imenasa baadhi ya majina ya makocha ambao wameonyesha shauku ya kuinoa timu hiyo ambayo imetoka kuachana na Dimitar Pantev kutokana na mwenendo ambao usioridhisha kwenye mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kuna jina la kocha wa Stellenbosch, Steve Barker lakini pia yupo Mkurugenzi wa Ufundi wa TS Galaxy ya Afrika Kusini, Nermin Bašić.
Maombi ya kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda ambaye kwa sasa anainoa Gambia, Johnathan McKinstry pia yapo mezani kwa mabosi wa timu hiyo huku pia likiwepo jina la kocha wa zamani wa Burkina Faso, Hubert Velud.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa mchakato wa kumsaka kocha mpya unakaribia kukamilika.
"Makocha waliotuma maombi ni wengi na kazi ya kuwapunguza imeshafanyika na kilichopo sasa wale wachache waliobakia ni kupitia wasifu wao na kuwachuja ili wabakie watano ambao watafanyiwa usaili na kocha mpya atapatikana hapo," amesema Ahmed Ally.
Ally amesema kuwa suala la kocha wanataka walimalize mapema ili waanze mchakato wa usajili wa dirisha dogo kwa vile utategemea mapendekezo na maoni yake.