Makocha Zanzibar waichangia Singida BS fainali Mapinduzi
LEO ni fainali ya Kombe la Mapinduzi baina ya Singida Big Stars na Mlandege ambayo huenda ikaambatana na Sapraizi kadhaa.
Kwanza, katika hali isiyo ya kawaida, Kocha maarufu wa Zanzibar anayeinoa KMKM,Hemed Morocco ameongeza nguvu kwenye benchi la Mlandege kuhakikisha Kombe halitoki Unguja leo usiku na amesisitiza kwamba amewapa uzoefu na mbinu zote anazozijua dhidi ya Singida. Morocco amesema si yeye tu makocha wengi wa Zanzibar wako nyuma ya Mlandege kwa heshima ya visiwa vyao.
Lakini Singida ambao wanacheza kwa mara ya kwanza fainali hizo, wamepiga mkwara kwamba leo itakuwa ni mechi yao ya kipekee na watacheza mpira mkubwa ambao haujazoweleka kuonekana kwao kwenye siku za karibuni.
Mechi hiyo itaanza saa 2:15 usiku, ambapo mastaa wa Mlandege wameahidiwa Pikipiki aina ya Honda kama wataibuka na ushindi kwenye mchezo huo ambao wamepania kuujaza uwanja wa Amaan kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Ni mechi ambayo Singida licha ya kuwategemea mastaa wao Wabrazili, itakuwa na Fancy Kazard mwenye moto mkali kwa sasa huku Mlandege ikiwa na wachezaji wengi machachari wenye uwezo mkubwa lakini hawavumi sana masikio mwa mashabiki.
Beki wa Mlandege Abdallah Said Ali, amewatahadharisha mastaa wenzie kuwa makini kwani hawapo tayari kupoteza na watawaduwaza leo.
“Nimewashuhudia kwenye mechi zao walizocheza hapa, ni timu bora na kubwa lakini linapokuja suala la kutafuta taji hatuwezi kuishi katika ubora wao wakati na sisi tupo kwenye nafasi nzuri ya kuonyesha ushindani,” alisema Ali na kuongeza;
“Naamini tutaingia katika mechi tukiwa imara zaidi na tutashinda,” alisema beki huyo ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wao dhidi ya Simba huku timu yake ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kiungo, Abdulsamad Kassim Ali alieleza kuwafahamu baadhi ya wachezaji wa Singida aliokutana nao kipindi anachezea Kagera Sugar, Ruvu Shooting na Simba ambayo hakupata nafasi ya kucheza.
“Itakuwa ni mechi yenye ushindani lakini naamini baada ya dakika 90 tutakuwa wenye furaha zaidi,”alisema. Kocha wa Mlandege, Abdallah Mohammed ‘Bares’ alisema; "Nimefurahishwa na morali ya wachezaji wangu wananipa moyo na imani kubwa kuelekea mchezo huo.”
Kocha wa KMKM, Hemed Moroco amesema ameishuhudia timu hiyo ikifanya mazoezi anaimani nayo kama makocha wa ligi na Zanzibar wapo nyuma kumpa sapoti ili taji hilo libaki nyumbani.
Morocco ameongea na kocha Bares wapi anatakiwa kuboresha na kuongeza nguvu ili timu yake ibebe taji na anaamini Wazanzibari watapata furaha leo.
“Tunatambua hautakuwa mchezo rahisi lakini maandalizi yaliyofanyika yanatija kwa timu na kwa wana Zanzibar kwa ujumla ambao wanaomba Dua kuhakikisha taji linabaki hapa,” alisema na kuongeza;
“Ubora waliouonyesha wachezaji kuanzia mwanzo wa mashindano hadi nafasi waliyofika tunatarajia kuuona mara mbili zaidi ili kuendeleza ushindani kwa timu za Bara na kuwapa furaha Wazanzibar waliyoikosa kwa muda mrefu,”alisema Morocco.
Kocha msaidizi wa Singida, Shadrack Nsajigwa alisema dakika 90 ndio zitaamua nani bora kati yao na Mlandege lakini wanatarajia ushindani mkubwa kwasababu ni fainali na kila timu inahitaji taji.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu tutaingia kwa kuwapa heshima ni wazuri ndio maana wamefika hatua hii ya fainali.”