Mamelodi yacheza mechi tatu bila bao

Congo. Timu nne juzi zilivaana kwenye michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya nusu fainali, huku likifungwa bao moja tu kwenye michezo hiyo, lakini safu ya ushambuliaji ya Mamelodi ikiendelea kuwa butu.
Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo ilivaana na TP Mazembe nchini DR Congo na kulazimisha suluhu, jambo ambalo linawapa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa pili nchini Misri. Ahly ilifika hapa baada ya kuichapa Simba jumla ya mabao 3-0 kwenye michezo ya robo fainali.
Katika mchezo huo timu zote zilionyesha kiwango cha juu huku Mazembe ikionekana kutawala sehemu ya mchezo huo na mastaa wake Zemanga Soze na Glody Likonza wakipoteza nafasi kadhaa za wazi.
Al Ahly ambayo baada ya mchezo huo wachezaji wake walionekana wakifurahia, ilikuwa ikishambulia kwa kushtukiza huku ikiwa na nidhamu nzuri kwenye eneo la ulinzi.
Matokeo haya siyo mazuri kwa Mazembe ambayo inatafuta nafasi ya kwenda fainali kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka kumi kutokana na ubora ilionao Ahly kila inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Kwa upande wa Mamelodi Sundowns ambao waliitupa nje Yanga kwenye hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti, walikutana na kitu kizito baada ya kuchapwa bao 1-0 na ES Tunis nchini Tunisia, shukrani kwa bao safi lililowekwa kimiani na Mbrazil Yan Sasse.
Mamelodi iliyonyesha kiwango cha juu kwenye mchezo huo, lakini ikajikuta ikipoteza kutokana na makosa binafsi lakini jambo la kushtua kwao ni kitendo cha kucheza michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika bila kufunga bao lolote.
Mastaa hao wa Afrika Kusini walicheza na Yanga michezo miwili na yote walitoka suluhu.
Mastaa wa timu hiyo Peter Shalulile na Themba Zwane walikosa nafasi kadhaa za wazi la kufunga mabao huku kipa wa Tunis Amanallah Memmich akiibuka shujaa.
Sasa Mamelodi inatakiwa kutumia faida iliyonayo ya kumalizia hatua ya robo fainali nyumbani na nusu fainali kwenye mchezo wa wikiendi ijayo ili iweze kwenda fainali kutafuta ubingwa wa pili wa michuano hiyo mikubwa Afrika mbele ya Tunis ambao wanatafuta ubingwa wao wa tano.