Man City yaanza kulia na waamuzi England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola akizungumza na baadhi ya Waamuzi wa mchezo baada ya mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham kumalizika kwa sare ya 2-2. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Guardiola pia aliwakosoa waamuzi kufuatia matukio tata katika mechi dhidi ya Manchester United na Wolves.
Manchester, England. Kiungo wa Manchester City, Rodri, ametoa madai akisema waamuzi wa Ligi Kuu England hawachezeshi kwa haki mechi zinazohusisha klabu yake, akidai mafanikio makubwa ya City yameanza kuathiri maamuzi ya waamuzi.
Rodri, mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or, ameonesha hasira kubwa baada ya bao la kwanza la Dominic Solanke kuruhusiwa katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Tottenham Hotspur, akisisitiza kuwa kulikuwa na faulo ya wazi kabla ya bao hilo kufungwa.
Solanke alimgonga beki Marc Guehi wakati akifunga, lakini baada ya ukaguzi wa VAR bao hilo lilikubaliwa.
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, amedai kuwa endapo tukio hilo lingetokea mchezaji wa ulinzi akimkabili mshambuliaji, basi faulo ingepigwa bila kusita. Rodri naye hakuficha hisia zake akisema;
Kiungo wa Manchester City, Rodri. Picha na Mtandao
“Amempiga mguu, ni wazi kabisa. Alimuwahi Marc na ni faulo ya wazi. Lakini sio leo tu, ni mechi mbili au tatu mfululizo, na kwa kweli sijui kwa nini.
“Najua tumeshinda sana na watu hawataki tuendelee kushinda, lakini mwamuzi hatakiwi kuwa wa upande wowote. Kwa mtazamo wangu, hii si haki. Si haki kabisa,” amesema Rodri.
Kauli za Rodri zinafanana na malalamiko ya kocha wake Guardiola, ambaye amekuwa akilalamikia kile anachokiita kutokuwepo kwa uthabiti wa maamuzi ya waamuzi, akiamini hali hiyo imeigharimu City mara kadhaa msimu huu.
Matokeo hayo ya sare jijini London yameifanya Manchester City kushinda mchezo mmoja tu kati ya mechi sita zilizopita, huku wakibaki pointi sita nyuma ya vinara wa Ligi Kuu Arsenal, zikibaki mechi 14 za kucheza.
Guardiola amekuwa wazi katika kuwakosoa waamuzi kufuatia matukio tata katika mechi dhidi ya Manchester United na Wolves.
Mshambuliaji wa Spurs, Dominic Solanke (Kushoto), wakati akifunga bao la kusawazisha ambalo limekuwa na mjadara kuwa, kulikuwa na faulo ya wazi dhidi ya beki wa Man City, Marc Guehi (Ambaye yupo mbele kulia). Picha na Mtandao
“Hili limetokea tena. Nifanyeje? Marc ana mpira, anapigwa teke kutoka nyuma na inakuwa bao. Nisemaje zaidi? Hakuna. Tena na tena.
“Kama angefanyiwa mshambuliaji, ingekuwa penalti. Mimi si mwamuzi. Ni mambo ya kushangaza kwenye Ligi Kuu,” amesema Guardiola.
Akizungumzia kuporomoka kwa kiwango cha timu yake baada ya bao la kwanza, ambalo lilifuatiwa na bao la kusawazisha la Solanke kwa shuti la kisigino, Guardiola amesema kulikuwa na athari ya kisaikolojia.
“Kulikuwa na athari ya kihisia baada ya bao la kwanza kuruhusiwa, na baada ya hapo ni vigumu kudhibiti kasi ya mchezo. Haya ni mambo yanayotokea hapa England,” ameongeza.
Guardiola ameonyeshwa kadi ya njano kwa kupinga uamuzi huo. Hivi karibuni alitumikia adhabu ya kusimamishwa kuiongoza City kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Exeter City baada ya kufikisha kadi tatu za njano msimu huu.
Baadhi ya wachezaji wa Tottenham, wakishangilia moja ya bao katika mechi ya Ligi Kuu England 'EPL' dhidi ya Man City iliyomalizika kwa sare ya 2-2. Picha na Mtandao
Kwa upande wake, kocha wa Tottenham, Thomas Frank, amekiri kuwa uamuzi huo ulikuwa wa utata na ungeweza kwenda upande wowote.
Frank pia amempongeza Solanke, ambaye amerudi hivi karibuni baada ya majeraha ya muda mrefu, akisisitiza kuwa bado hajafikia ubora wake kamili.
“Dom alihangaika kukimbia mwishoni. Tulijua kucheza dakika 90 kungekuwa changamoto, bado hajafikia kiwango kamili cha mazoezi.
“Tumelazimika kumtumia. Lakini ana mabao manne katika mechi nne akiwa na asilimia 80 ya utimamu.
“Fikiria City kucheza bila Erling Haaland kwa miezi sita. Sisi tumepata pigo kubwa la majeraha. Dom alikuwa bora sana,” amesema Frank.
Frank pia amethibitisha kuwa nahodha Cristian Romero alitolewa kipindi cha mapumziko kutokana na kuugua, hali iliyomsumbua pia kwenye ushindi wao wa katikati ya wiki dhidi ya Frankfurt.
Kwa upande mwingine, Guardiola amebainisha kuwa jeraha la nyama ya paja lililomlazimu nahodha wake, Bernardo Silva kutoka halikuwa kubwa. Manchester City sasa wanajiandaa kuivaa Newcastle United kwenye mchezo wa Kombe la Carabao utakaopigwa Jumatano.