Mangungu, Hersi 'wasifunge' milango kwa wengine TFF

Muktasari:
- Hofu ya kisichojulikana inaanza kuzidi. Siyo tu Tanzania, bali Afrika nzima. Watu wana hofu dhidi ya kitu wasichojua kwa kuwa hawajui kinachokuja.
Kumeibuka utamaduni unaolenga kudumisha hali iliyopo pengine ni kwa kutojua kinachoweza kutokea mbele kama ni kizuri kwa maendeleo au kibaya kwa maendeleo.
Hofu ya kisichojulikana inaanza kuzidi. Siyo tu Tanzania, bali Afrika nzima. Watu wana hofu dhidi ya kitu wasichojua kwa kuwa hawajui kinachokuja.
Na pengine hofu hiyo siyo ya kweli, bali ni ya kupikwa na baadhi ya watu ili hali isibadilike na mambo yaendelee kwenda hivyo hivyo kwa sababu wananufaika na hali iliyopo sasa wakidai ni nzuri. Hii inaua ushindani.
Katikati ya mwaka huu zaidi ya marais 40 wa vyama vya soka vya nchi za Afrika wameeleza msimamo wao kuwa vinamuunga mkono rais wa sasa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe ili aendelee kukiongoza chombo hicho baada ya kuona makubwa katika kipindi chake cha kwanza.

Nina uhakika sehemu kubwa ya viongozi hao zaidi ya 40 wa nchi waliotoa msimamo huo ni wale walioandika barua kwa rais wa zamani wa CAF, Ahmad Ahmad kuwa wanamuunga mkono aendelee kuliongoza shirikisho hilo baada ya kuona mazuri katika kipindi chake cha kwanza.
Kumbe Ahmad alikuwa na madudu mengi ambayo yalimfanya asiwe na sifa za kushika wadhifa huo ikiwa ni pamoja na tuhuma za rushwa, unyanyasaji wa wafanyakazi wa makao makuu, kuingia mikataba ya hovyo na mambo mengine.
Wakati huo alitoa ruzuku ya Dola 100,000 kwa kila shirikisho la nchi akielekeza kuwa Dola 20,000 kati ya hizo zielekezwe kwa marais wa vyama vya nchi akidai kuwa wanatumia muda wao mwingi katika mpira na kupoteza mali zao.

Mtindo huo ndio umerudiwa na Motsepe ambaye ameahidi kutoa Dola 50,000 kwa kila mwenyekiti wa nchi mwanachama kwa ajili ya kuendesha mambo yake. Kwa hiyo ukisikia kuna viongozi zaidi ya 40 wamemuunga mkono ujue wapo waliovutiwa na ruzuku hiyo binafsi na si uendeshaji bora wa mpira wa miguu.
Sitaki kusema kuwa Motsepe amehonga, lakini kutoa ahadi kama hiyo mwishoni mwa kipindi chako cha uongozi na ukiwa unataka kutetea nafasi yako kuna maswali mengi na pengine kunaweza kuwa na ruzuku binafsi zaidi ya hizo.
Lakini tatizo kubwa zaidi liko kwa wale wanaohangaika hadi kulazimika kutoa kauli rasmi kwamba watamuunga mkono rais aliyepo sasa wakihofu kuwa pengine anayekuja anaweza kuondoa hata mambo ya ruzuku.

Utamaduni kama huo wa kuanza kampeni kabla ya muda umejitokeza katika mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu kusema mkutanoni kuwa atakayetaka kugombea urais wa shirikisho hilo watamhoji anataka kuongeza nini kwa sababu rais wa sasa, Wallace Karia ameshafanya mengi.
Kauli ya Mangungu pia imeungwa mkono na rais wa Yanga, Hersi Said kwamba wataenda na Karia.
Si vibaya wawili hao kuwa na mtu wanayekusudia kumpa kura wakati wa uchaguzi, lakini ni kitu gani kimesukuma kutoa matamko kama hayo wakati huu?
Nani amewaambia kuwa Watanzania wenye uwezo wa kuongoza shirikisho hilo wameisha na hivyo hawataki mtu mwingine yeyote zaidi ya wanayemjua kwa sasa.

Siasa za ushindani ni muhimu kwa maendeleo ya jamii yoyote au taasisi kama TFF. Pale kunapokuwepo na ushindani ndipo wanaopewa dhamana ya kuongoza chombo huwa makini kufanya maendeleo ili muda unapofika kazi zao ziweze kushawishi watu kuwa anafaa kuendelea.
Lakini watu 'wanapofunga' milango kuzuia watu wasiowajua kuja kujaribu kuomba kura, basi yule aliyepo madarakani hubweteka na kufanya mambo bora liende kwa kuwa tayari ameshawateka wapigakura.
Hakuna sababu ya kuwa na hofu ya kutokea mtu ambaye hatakuwa na uwezo. Pengine anaweza kutokea kiongozi mzuri zaidi akaharakisha maendeleo kuliko haya tunayoyaona leo.
Kama Mshindo Msolla angefunga milango kwa wana Yanga kuingia kugombea urais tungewezaje kujua kuwa Hersi ana uwezo huo mkubwa ulioifikisha klabu hiyo hapo ilipo?
Kama wana Yanga wangejitokeza kama Mangungu kusema mtu atakayekuja kutaka urais tutamuhoji ataongeza nini zaidi ya kilichofanywa na Msolla, Yanga ingefikia hapa ilipo? Pamoja na ukweli kwamba wapo wanachama wengine pengine wenye uwezo mkubwa zaidi, bado kitendo cha wanachama kutofungiwa milango wengine kilitoa mwanya kwa Hersi kuingia na kufanya hayo aliyofanya.

Tunahitaji ushindani wa kweli katika uongozi wa mpira wa miguu. Tunajua mabadiliko ya katiba ya mwaka 2020 yalifunga milango mingi kwa wanafamilia ya mpira wa miguu kuingia kushika nafasi ya uongozi hadi kwa ridhaa ya walio mamlakani. Lakini si vizuri kufunga kabisa hata upenyo mdogo uliobaki wa watu wengine pengine wenye uwezo mzuri zaidi kugombea uongozi.
Mangungu kama mmoja wa wanasiasa wakongwe anajua athari za kutoa matamko kama hayo. Na hata kwenye klabu yake ya Simba wakitokea wanachama na kumfanyia kampeni mtu mwingine wanayemtaka hata kabla ya muda, atalalamika tu, tena sana.
Yule kipofu aliyefunguka macho siku moja na kuona tembo alidhani kitu chochote kizuri, kikubwa, chembamba, kipana au kirefu kinafanana na tembo ndio maana kila alipohadithiwa kuwa kuna mtu kaona sungura mzuri aliuliza “kama tembo?” kwa kuwa ndiyo kitu pekee alichokiona.
Tuache tabia za kipofu huyo. Tunahitaji watu wengi zaidi kugombea ili kuwe na wigo mpana wa kuchagua.