Manula hatihati kuikosa Derby

What you need to know:

  • Manula na Inonga wote walikosa mechi iliyopita ya Ligi Kuu dhidi ya Ihefu baada ya kutolewa uwanjani kwenye pambano la robo fainali ya Kombe la ASFC pale Simba ilipovaana na Ihefu haohao na kushinda mabao 5-0.

Dar es Salaam. Habari ya kushtua ni kwamba kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula anaweza asisimane langoni kesho saa 11:00 jioni dhidi ya Yanga katika pambano la Kariakoo Derby la 110 la Ligi ya Bara lakini beki wa kati wa timu hiyo Henock Inonga ameibuka na mzuka. Inonga alikuwa majeruhi anasema kwa sasa yupo fiti na analitaka pambano hilo amalize mambo Kwa Mkapa.

Manula na Inonga wote walikosa mechi iliyopita ya Ligi Kuu dhidi ya Ihefu baada ya kutolewa uwanjani kwenye pambano la robo fainali ya Kombe la ASFC pale Simba ilipovaana na Ihefu haohao na kushinda mabao 5-0.

Hata hivyo beki huyo wa kazi ameanza kupiga tizi tofauti na kipa huyo namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars ambaye hajaanza mazoezini hadi jana asubuhi.

Kuumia kwa mastaa hao wawili awali kulileta hofu na sintofahamu ndani ya kikosi, kwani kurejea kwa Inonga, huku kukiwa na makipa wenye viwango vikubwa Beno Kakolanya na Ally Salim kumeleta ahueni. Kakolanya hakutumika kwenye mechi iliyopita ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu na langoni alikaa Salim wakati Simba ikishinda 2-0 kwenye Uwanja wa Highland Estate ambao Yanga na Azam zilipasuka mbele ya Ihefu.
Staa wa zamani wa Mecco na Coastal Union, Charles Makwaza amewataka Simba kumuamini Salim kwani mechi ya Ihefu alionyesha utayari.

Habari kutoka ndani ya kambi ya Simba zinasema kuwa, Inonga kwa sasa ameanza mazoezi na wenzake, lakini jukumu la kutumika linabaki kwa Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na wasaidizi wake, ila kwa Manula bado mambo ni magumu na sio ajabu Simba ikamtumia Salim kwenye pambano hilo, ingawa Kakolanya yupo kikosini sambamba na kipa chipukizi Ahmad Feruzi Teru.

"Inonga juzi (Alhamisi) alifanya mazoezi, lakini alishindwa kumaliza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu ambayo aliyapata kwenye mchezo dhidi ya Ihefu FC wa kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Lakini kwa upande wa Manula hajapata nafasi ya kufanya mazoezi kabisa na hali yake sio nzuri kutokana na kukiri bado anajisikia vibaya hivyo suala la kucheza au kutocheza mimi siwezi kulizungumzia labda kocha," kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwe gazetini.

Alipotafutwa na Mwanaspoti, Inonga alithibitisha kuwa kwa sasa yupo fiti na anaendelea vizuri na mazoezi yupo tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumapili ambao ameutaja kuwa ni muhimu kwao.

"Naendelea vizuri na nimeshaanza mazoezi kuhusu kucheza au kutokucheza ni jukumu la kocha, lakini natamani kuwa miongoni mwa wachezaji watakaopambana dakika 90 bora zitakazoamua matokeo kwa pande zote mbili.

"Tunatarajia mchezo bora na wa ushindani tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu huku tukiwa tumejiandaa vyema kuhakikisha hatupotezi pointi hata moja zaidi ya kupata zote tatu ambazo ni muhimu kwetu," alisema Inonga - beki aliyetengeneza ukuta imara Msimbazi tangu msimu uliopita akishirikiana na Mkenya Joash Onyango sambamba na mzawa Kennedy Juma, japo Mohamed Ouattara naye yumo kikosini.