Maoni yatawala gharama Uwanja wa Samia

Muktasari:

  • Kiwango hicho cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya uwanja huo  ambao unatarajiwa kuingiza takribani mashabiki 30,000 ni zaidi ya mara mbili ya kile kilichotumika kujengea Uwanja wa Benjamin Mkapa uliojengwa kwa takriban Sh134 bilioni

Wakati mkataba wa Sh286 bilioni ukisainiwa juzi baina ya Serikali na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa soka wa Samia Suluhu jijini Arusha ambao utatumika kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, kumekuwa na maoni tofauti juu ya gharama za ujenzi huo.

Kiwango hicho cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya uwanja huo  ambao unatarajiwa kuingiza takribani mashabiki 30,000 ni zaidi ya mara mbili ya kile kilichotumika kujengea Uwanja wa Benjamin Mkapa uliojengwa kwa takriban Sh134 bilioni.

Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), mwanaharakati Chris Cyrilo alihoji kwa nini gharama za ujenzi wa uwanja huo zimekuwa kubwa huku ukiingiza mashabiki wachache.

"Uwanja wa Mkapa wa kubeba watu 60,000 ulijengwa kwa USD 56 milioni sawa na TZS 64 bilioni wakati huo. Uwanja wa Samia Arusha wa kubeba watu 30,000 unajengwa kwa USD 112 milioni sawa na TZS 286 bilioni. Ni kushuka thamani kwa sarafu zote USD na TZS au kuna mengine tusiojua?" alihoji Cyrilo.

Joseph Sinde naye alihoji nini kimesababisha uwepo wa gharama kubwa za ujenzi wa uwanja huo kulinganisha na Benjamin Mkapa.

"Tuambiwe tofauti ya kimahesabu kwa gharama za Uwanja wa Benjamin Mkapa ni mkubwa na huo wa Samia Suluhu Hassan ni mdogo. Tueleweshwe kwa mfano nondo ilikuwa Tsh... sasa ni Tsh.. sementi ilikuwa ni Tsh.... sasa ni Tsh... Dola ilikuwa Tsh... sasa ni Tsh....," aliandika Sinde.

Hata hivyo, katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Angetile Osiah alisema kuwa sio jambo la kushangaza kwa Uwanja wa Samia kujengwa kwa gharama kubwa kuliko ule wa Benjamin Mkapa.

"Kuna mambo ambayo yanafanya gharama ziongezeke na sio uwezo wa kuchukua idadi fulani ya watazamaji pekee. Kuna suala la kupanda kwa gharama ya ujenzi, lakini pia teknolojia ambayo itawekwa kwenye uwanja husika.

Mfano Uwanja wa Tottenham Hotspur una teknloojia ya hali ya juu kulinganisha na Emirates wa Arsenal ambao unaingiza idadi kubwa ya mashabiki," alisema Osiah.

Mkurugenzi wa zamani wa wanachama wa Simba, Hashim Mbaga alisema kuwa sio jambo la kushangaza kwa gharama za ujenzi kwa viwanja hivyo kutofautiana.

"Uwanja wa Mkapa ulijengwa na kukamilika 2007 wakati huo sokoni Dola ikiwa ni Sh1,150 wakati uwanja huu mpya unajengwa 2024, soko la Dola ni Sh2,550. Mahitaji ya wakati ule na wakati huu katika ujenzi ni tofauti kulingana na aina za mikataba, vifaa vinavyotumika na eneo la ujenzi," alisema.

Mkandarasi Victor Ndozero alisema tathmini halisi ya usahihi wa bajeti itategemea taarifa za nini kitakachokuwa ndani ya uwanja huo na sio kuangalia namba ya mashabiki pekee.

"Kwa sasa ni mapema kusema kama bajeti hiyo inastahili au haistahili hadi pale tutapofahamu ni vitu gani hasa vitakuwemo ndani (drawing 3D) ambayo inaonyesha mwonekano wa ndani na vipi vitakuwepo, " alisema Ndozero."Hata hivyo gharama ya ujenzi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati ule haiwezi kuwa sawa na sasa."

Uwanja wa Samia Suluhu Hassan unatajwa kuwa utakuwa na maboksi ya kutazama mechi kwa watu maalumu, hautatuamisha maji, kumbi za kimataifa za mikutano, hoteli na vinginevyo.