Marefa wa Dabi ya Kariakoo wapewa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia 2026 baina ya wenyeji Mexico na Afrika Kusini itachezeshwa na refa Wilton Sampaio wa Brazil.
Marefa wawili waliochezesha mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara 2024/2025 baina ya Watani wa Jadi, Yanga na Simba, Juni 25, 2025 wameteuliwa kuchezesha mechi ya pili ya Kombe la Dunia mwaka huu baina ya Korea Kusini na Jamhuri ya Czech.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa Juni 12, 2026 saa 11:00 alfajiri kwa muda wa Afrika Mashariki.
Marefa hao ni Amin Mohamed ambaye amepangwa kuwa mwamuzi wa kati na Mahmoud Abouregal aliyepangwa kuwa msaidizi namba moja.
Amin na Abouregal ndio walichezesha mechibya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu 2024/2025 ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika uteuzi uliofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Mmisri mwingine, Ahmed Taha amepangwa kuwa refa msaidizi namba mbili na Juan Calderon kutoka Costa Rica atakuwa refa wa akiba.
Mbrazil apewa ufunguzi
Mechi ya ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 baina ya Mexico na Afrika Kusini, Juni 11, 2026 itachezeshwa na refa Wilton Sampaio wa Brazil.
Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki, katika Uwanja wa Azteca, Mexico.
Refa msaidizi namba moja ni Bruno Pires na msaidizi namba mbili ni Bruno Boschilia wote kutoka Brazil na refa wa akibani Juan Benitez kutoka Paraguay.