Marekani yaibwaga Mexico na kuandika historia CONCACAF

Monday June 07 2021
marekani pc

Denver, Marekani. Marekani jana Jumapili iliibwaga Mexico kwa mabao 3-2 na kutwaa ubingwa wa michuano ya kwanza ya soka ya Ligi ya Mataifa ya Amerika Kaskazini na Kati (CONCACAF) katika mechi ambayo ilikuwa na penati iliyopigwa katika muda wa nyiongeza na Christian Pulisic na pia kipa Ethan Horvath, aliyetokea benchi, kuokoa penati nyingine.

Marekani ilizinduka mara mbili baada ya kutangulia kufungwa-- kwanza ikiwa nyuma kwa bao 1-0 na baadaye kwa mabao 2-1 -- na kulazimisha mchezo huo uliofanyika uwanja wa Epower Field, uongezewa muda.

Mwishoni mwa muda wa kawaida, matokeo yalikuwa mabao 2-2 na katika dakika ya 114, Pulisic, anayeichezea Chelsea, aliifungia Marekani bao la kuongoza alipopiga penati iliyotolewa baada ya kuangalia marudio ya VAR.

Dakika sita baadaye, penati ya Andres Guardado -- iliyotolewa baada pia ya VAR kuthibitisha kuwa Mark McKenzie aliunawa mpira ndani ya eneo la hatari -- ilipanguliwa na Horvath.

Hadi wakati huo, kocha wa Mexico, Gerardo "Tata" Martino ambaye ni raia wa Argentina, alikuwa ameshatolewa nje kwa kumshika refa John Pitti wakati akiangalia marudio ya video kuthibitisha tukio la Carlos Salcedo kumuangusha Pulisic akiwa ndani ya eneo la penati.

Uamuzi ulikuwa ni kutoa penati, kitu kilichosababisha mashabiki wa Mexico kurusha vitu uwanjani.
Mexico ilianza mchezo huo kwa kwa kasi, ikifunga bao la kuongoza mapema katika dakika ya pili kwa bao la Jesus Corona.

Advertisement

Gio Reyna alijibu mapigo kwa kuifungia Marekani bao la kusawazisha katika dakika ya 27 -- dakika moja baada ya Mexico kudhani kuwa imeshafunga bao la pili baada ya Hector Moreno kuunganisha mpira wavuni kwa kichwa, lakini marudio ya VAR yalionyesha alikuwa ameshaotea.

Uamuzi huo ulitengeneza mazingira mazuri kwa Reyna, kiungo mwenye miaka 18 wa Borussia Dortmund, ambaye aliuwahi mpira uliogonga mwamba baada ya Weston McKennie kuunganisha kona ya Pulisic.

Baadaye mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Diego Lainez aliirudisha Mexico katika uongozi alipofunga bao dakika ya 79, akipiga kiki iliyompita Horvath ambaye aliingia uwanjani dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Steffen aliyeumia mguu.

Kwa mara nyingine, Marekani ilisawazisha, safari hii mpira wa kichwa wa McKennie ulimtoka kipa wa Mexico, Guillermo Ochoa na kujaa wavuni.

Timu hizo mbili hazikuweza kufungana katika dakika zilizosalia na kipindi cha kwanza cha muda wa nyongeza, Marekani ilimaliza ubishi.
Pulisic, akiwa ndio kwanza ametoka kuipa Chelsea kombe la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, aliingia ndani ya eneo la penati akipambana na mabeki wawili wa Mexico.

Awali Pitti hakutoa penati, lakini alibadili uamuzi baada ya muda mrefu wa kusubiri ambao ulisababisha hasira zitamalaki jukwaani.
Pulisic alirudi nyuma hatua mbili na kupiga mpira kuingia kona ya juu ya goli kuipa Marekani bao la ushindi.

Wakati marudio ya VAR yalipothibitisha kuwa McKenzie aliunawa mpira, Guardado aliyekuwa akicheza mechi ya 116 ya kimataifa, alipiga penati kwa kujiamini lakini Horvath akachupia upande wa kulia na kuokoa mpira.

"Kusema kweli sina la kusema," Horvath aliiambia televisheni.
"Kama ukiwa benchi, kama kipa hutegemei kuingia uwanjani," aliongeza. "Ni lundo la hisia. Ni kipindi cha aina yake kwangu katika mji wangu wa Denver."

Hii ni mara ya pili kwa Marekani kupata ushindi dhidi ya Mexico katika mechi saba za CONCACAF, mara ya kwanza ikiwa mwaka 2007 katika Gold Cup.


Advertisement