Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashabiki Japan wanavyojitofautisha kwa usafi Kombe la Dunia


Muktasari:

  • Wajapani wana msemo maarufu unaosema "Tatsu tori ato wo nigosazu", unaomaanisha kuwa mtu anapaswa kuondoka mahali bila kuacha uchafu au usumbufu wowote nyuma yake.

Arlington, Texas. Dakika chache baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa kwenye Uwanja wa AT&T mjini Arlington, wengi walidhani simulizi kubwa ya usiku ingekuwa sare ya mabao 2-2 kati ya Japan na Uholanzi.

Lakini, kama ilivyokuwa mara nyingi katika michuano mikubwa ya soka duniani, mashabiki wa Japan walihakikisha kuwa gumzo halikuishia ndani ya uwanja pekee.

Wakati maelfu ya mashabiki wakielekea kwenye njia za kutokea, kundi kubwa la mashabiki wa timu ya taifa ya Japan, maarufu kama Samurai Blue, lilibaki kwenye viti vyao na kuanza kazi waliyoizoea vyema ya kuokota taka zilizokuwa zimeachwa viwanjani.

Wakiwa na mifuko maalumu ya kuhifadhia taka, mashabiki hao walikusanya chupa za maji, vikombe vya vinywaji, vifungashio vya chakula na mabaki mengine yaliyosalia kwenye majukwaa ya uwanja huo mkubwa wa Texas.

Kitendo hicho kimeendelea kuifanya Japan kuwa mfano wa kuigwa duniani, huku utamaduni wao wa kuacha sehemu ikiwa safi kuliko walivyoikuta ukizidi kuvutia macho ya mashabiki na waandaaji wa mashindano makubwa ya kimataifa.

Baadhi ya mashabiki wa Japani wakiwa wanafanya usafi uwanjani baada ya mechi ya Kombe la Dunia kumalizika


Utamaduni uliojengeka toka utotoni

Kwa mujibu wa wataalamu wa utamaduni wa Japan, tabia hiyo si jambo la kushangaza kwa wananchi wa nchi hiyo.

Tangu wakiwa shule za msingi, watoto hufundishwa umuhimu wa kusafisha madarasa, viwanja na maeneo ya pamoja kama sehemu ya kuwajengea nidhamu, uwajibikaji na kuheshimu mali ya umma.

Wajapani wana msemo maarufu unaosema "Tatsu tori ato wo nigosazu", unaomaanisha kuwa mtu anapaswa kuondoka mahali bila kuacha uchafu au usumbufu wowote nyuma yake.

Kauli hiyo imekuwa falsafa inayotafsiriwa kwa vitendo katika matukio ya michezo, tamasha na mikusanyiko mikubwa duniani.

Si mara ya kwanza kwa mashabiki hao kuvutia hisia za dunia.

Walifanya hivyo katika Kombe la Dunia la mwaka 2018 nchini Russia na wakaendeleza utamaduni huo nchini Qatar mwaka 2022, jambo lililowafanya kupongezwa na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali.

Baadhi ya mashabiki wa Japani wakiwa wanafanya usafi uwanjani baada ya mechi ya Kombe la Dunia kumalizika


Mchezo uliojaa msisimko

Ndani ya dakika 90, Japan ilionyesha moyo mkubwa wa kupambana baada ya kutoka nyuma mara mbili na kuibana Uholanzi kwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa Kundi F.

Uholanzi ilitangulia kupitia mabao ya Virgil van Dijk na Crysencio Summerville, lakini Japan ilijibu kupitia Keito Nakamura kabla ya Daichi Kamada kuisawazishia dakika za mwisho na kuipa pointi muhimu katika mbio za kufuzu hatua ya 16 bora.

Mchezo huo ulioshuhudiwa na zaidi ya mashabiki 69,000 ndani ya AT&T Stadium ulitawaliwa na shamrashamra kubwa kutoka kwa pande zote mbili, huku mashabiki wa Uholanzi wakionyesha utamaduni wao wa shangwe na rangi ya machungwa, na wale wa Japan wakitoa somo la ustaarabu baada ya mchezo kumalizika.

Baadhi ya mashabiki wa Japani wakiwa wanafanya usafi uwanjani baada ya mechi ya Kombe la Dunia kumalizika


Jameis Winston ajiunga nao

Katika tukio lililogusa wengi zaidi, nyota wa zamani wa NFL na mchambuzi wa FOX Sports, Jameis Winston, alionekana akishiriki kuokota taka pamoja na mashabiki wa Japan.

Akiwa amevaa jezi ya timu hiyo, Winston alionekana akisaidia kukusanya uchafu huku akipongeza utamaduni huo wa kipekee.

Katika enzi ambayo matukio ya vurugu na utovu wa nidhamu viwanjani yamekuwa yakiongezeka sehemu mbalimbali duniani, mashabiki wa Japan wameendelea kuthibitisha kuwa ushabiki wa kweli haupimwi kwa sauti ya nyimbo wala ukubwa wa shangwe pekee, bali pia kwa heshima kwa wengine na mazingira yanayowazunguka.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.