Mastaa hawa kunogesha nusu fainali AFCON
Muktasari:
- Nigeria itakabiliana na wenyeji Morocco ambao watakuwa na faida ya sapoti ya mashabiki wao wa nyumbani.
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zinaelekea ukingoni zikiwa zimebakisha timu nne pekee, zilizotinga nusu fainali ambazo ni Nigeria, Senegal, Misri na wenyeji Morocco zitakazokuwa uwanjani leo katika muendelezo wa kuwania taji hilo la Afrika.
Kwa upande wa Nigeria ‘Super Eagles’ takwimu zinaeleza kila kitu. Katika mechi tano ilizocheza hadi sasa timu hiyo imeshinda zote, ikifunga mabao 14 huku ikiruhusu magoli mawili pekee.
Nigeria imekuwa imara tangu mwanzo hadi sasa, ikionyesha uimara na ukomavu mkubwa wa kikosi chake.
Kwa upande wa wenyeji Morocco chini ya kocha Walid Regragui, wameshinda mechi nne kati ya tano, wakitoa sare moja dhidi ya Mali ambayo ni kwenye hatua ya makundi.
Morocco hadi sasa imeonyesha uimara wa safu yao ya ulinzi ambayo imeruhusu bao moja tu mashindanoni, ambalo lilifungwa kwa mkwaju wa penalti kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Mali.
Kadri Morocco inavyojiandaa kwa nusu fainali ya kihistoria itakayochezwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Mwananchi inawaangazia wachezaji watano wenye uwezo wa kuamua hatima ya pambano hilo kali.
Achraf Hakimi (Morocco)
Ni vigumu kuzungumzia Morocco bila kumtaja Achraf Hakimi. Beki huyu wa PSG amekuwa na msimu mzuri katika ngazi ya klabu, akitwaa mataji ya Ligue 1, Coupe de la Ligue, UEFA Super Cup na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hakimi ambaye ni mchezaji Bora wa Afrika kwa sasa, alirejea uwanjani katika mchezo wa tatu wa makundi baada ya kuanza michuano akiwa majeruhi, na mara moja akaonyesha thamani yake kwa kutoa pasi ya bao dhidi ya Tanzania katika hatua ya 16 bora.
Victor Osimhen (Nigeria)
Mshambuliaji wa Galatasaray anaendelea kuwa tishio kubwa kwa safu yoyote ya ulinzi. Osimhen tayari ana mabao manne na pasi mbili za mwisho kwenye michuano hii, akiwatesa mabeki kwa kasi, nguvu na ustadi wake wa kufunga mabao.
Kwa upande wa Morocco, mabeki kama Nayef Aguerd na Adam Masina watakutana na mtihani mgumu zaidi pindi watakapojaribu kumdhibiti kwa dakika 90.
Brahim Diaz (Morocco)
Brahim Diaz amekuwa nyota wa mashindano kwa upande wa Morocco, akifunga katika mechi tano mfululizo rekodi ambayo ni adimu katika mashindano ya AFCON.
Mabeki wa Nigeria wana kazi ya kuhakikisha nyota huyo wa Real Madrid ya Hispania apati nafasi ya kukaa mguuni na mpira kwa muda mrefu kwani inaweza kuwa hatari kwenye lango lao kutoka na uwezo alionao mchezaji huyo wa kutumia nafasi ndogo kupachika mpira wavuni.
Diaz anakumbukwa katika mchezo wa 16 bora dhidi ya Tanzania ambapo aliibeba Morocco baada ya kutumia nafasi ndogo iliyokuwa imeachwa na golikipa, Hussain Masalanga pembeni ya lango.
Sofyan Amrabat (Morocco)
Amrabat ni injini ya Morocco. Udhibiti wake wa mpira, uwezo wa kupiga pasi sahihi humfanya kuwa hatari kila anapokuwa na mpira. Beki wa kushoto wa Nigeria, Bruno Onyemaechi, atalazimika kuwa makini kuepuka kubaki mmoja mmoja dhidi ya kiungo huyu wa Fenerbahce.
Alex Iwobi (Nigeria)
Akiichezea Fulham, Iwobi amekuwa mhimili wa mafanikio ya Nigeria katika hatua za mtoano. Kutoka upande wa kulia wa kiungo cha kati cha Nigeria, amehusika karibu katika kila jambo zuri walilofanya Super Eagles.
Amekuwa mchezaji muhimu katika kupika mabao akifanya hivyo mara tatu dhidi ya Msumbiji, mara mbili dhidi ya Algeria, Iwobi amehusika katika jumla ya pasi tano muhimu zilizozaa mabao.
Ikiwa Morocco wanataka kuizuia Nigeria isifikie eneo la hatari, Iwobi lazima azuiwe kwanza.
Yassine Bounou (Morocco)
Lango la Morocco limekuwa chini ya ulinzi madhubuti wa Yassine Bounou. Hadi sasa golikipa huyo hajaruhusu bao (clean sheet) katika mechi nne kati ya tano ambazo Morocco imecheza hadi sasa.
Uwezo wake wa kuokoa mipira, kupanga ulinzi na utulivu wake katika nyakati za presha unamfanya kuwa ngome imara.
Kwa kiwango bora cha Nigeria ilichokionesha hadi sasa leo itakuwa na wakati mgumu wa kuwazuia wenyeji Morocco ambao watakuwa na faida ya sapoti kutoka kwa mashabiki wao wa nyumbani lakini mchezo hautakuwa rahisi kutokana na ushindani wa pande zote mbili.