Mastaa sita waliokosa Kombe la Dunia dakika za jioni
Muktasari:
- Kwa wachezaji, kushiriki mashindano hayo ni kumbukumbu nzuri inayobaki kwa muda mrefu katika maisha yao.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 linalofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico hapana shaka litakuwa tukio la kukumbukwa sana.
Ni tukio linalowakutanisha nyota wengi wa soka duniani ambao wanazitafutia timu zao za taifa heshima huku wakijaribu kuwapa burudani na msisimko mashabiki wao.
Kwa wachezaji, kushiriki mashindano hayo ni kumbukumbu nzuri inayobaki kwa muda mrefu katika maisha yao.
Hivyo inapotokea mchezaji anapata majeraha muda mfupi kabla ya fainali hizo yanayosababisha aondolewe kikosini, huwa anabaki na historia inayoumiza ambayo inaweza kumuathiri hata kisaikolojia kwa muda mrefu.
Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, wapo wachezaji kadhaa ambao walishafanikiwa kuingia katika vikosi vya mwisho vya timu zao za taifa kwa ajili ya mashindano hayo lakini muda mfupi kabla ya mechi zao za kwanza, wakapata majeraha yaliyolazimishwa waondolewe vikosini na nafasi zao kuzibwa na wengine.
Spoti Mikiki inakuletea orodha fupi ya nyota ambao katika dakika za mwisho, wamekosa fursa ya kucheza Kombe la Dunia kutokana na majeraha.
Kiungo wa Ujerumani, Lennart Karl. Picha na Mtandao
Lennart Karl (Ujerumani)
Kiungo huyu anayetajwa kuwa na kipaji kikubwa akiwa na umri wa miaka 18, alipata jeraha la kuchanika kwa misuli ya paja la kushoto akiwa tayari kambini na timu ya taifa ya Ujerumani, wakijiandaa kwa Kombe la Dunia.
Nafasi ya Karl imezibwa na nyota wa RB Leipzig, Assan Ouedraogo.
Kocha wa Ujerumani, Julian Nagelsmann, alielezea kumkosa Lennart kama pigo kubwa kwa kikosi chake.
"Nampa pole Lenny (Karl). Kwa wepesi, ubunifu, kasi na haiba yake, anafiti katika timu vizuri kabisa. Ni mshtuko mkubwa kwake na kwetu sote kuona akikosa Kombe la Dunia," alisema Nagelsmann.
Kiungo wa RB Leipzig na nyota wa Austria, Christoph Baumgartner. Picha na Mtandao
Christoph Baumgartner (Austria)
Kiungo wa RB Leipzig na nyota wa Austria alipata jeraha wakati wa maandalizi ya mashindano na hatashiriki Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Austria haitamwita mchezaji mwingine kuziba nafasi yake na itaingia kwenye mashindano ikiwa na wachezaji 25 pekee.
Beki wa Arsenal na timu ya taifa ya Uhoranzi, Jurrien Timber. Picha na Mtandao
Jurrien Timber (Uholanzi)
Beki huyu mwenye umri wa miaka 24 hajapona vya kutosha jeraha la nyonga ili kushiriki Kombe la Dunia kwa usalama wa kiafya.
Baada ya mashauriano na timu ya madaktari, imeamuliwa kwamba Timber ataondoka katika kambi ya maandalizi ya timu ya taifa huko New York baada ya mchezo dhidi ya Uzbekistan.
Kocha Ronald Koeman amemuita Lutsharel Geertruida (Sunderland) kuchukua nafasi ya Timber. Hivyo, kikosi cha Uholanzi kilichoweka kambi yake huko Kansas kimerejea kuwa na wachezaji 26.
Ikumbukwe, Timber kabla ya Kombe la Dunia, alikaa nje kwa muda wa miezi miwili kutokana na majeraha hayo ya nyonga kuanzia Machi mwaka huu hadi Mei alipokuja kuibukia katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya timu yake Arsenal dhidi ya PSG, Mei 30.
Mshambuliaji wa Real Betis na timu ya taifa ya Morocco, Abde Ezzalzouli. Picha na Mtandao
Abde Ezzalzouli (Morocco)
Mshambuliaji wa Real Betis, Ezzalzouli, alipata jeraha la goti katika mechi ya kirafiki dhidi ya Norway mwishoni mwa wiki iliyopita.
Ameondolewa kwenye kikosi cha Morocco na nafasi yake kuchukuliwa na Amine Sbai wa Angers, kulingana na orodha ya kikosi iliyotolewa na FIFA.
Beki wa kati wa Marseille,na timu ya taifa ya Morocco, Nayef Aguerd. Picha na Mtandao
Nayef Aguerd (Morocco)
Beki wa kati wa Marseille, Aguerd, ambaye hajacheza tangu Machi baada ya kufanyiwa upasuaji wa tatizo la nyonga (groin), ameondolewa kwenye kikosi na nafasi yake kuchukuliwa na Marwane Saadane anayekipiga nchini Saudi Arabia.
Morocco iliamua kwenda na Aguerd katika Kombe la Dunia ikiamini angeweza kupona kwa wakati kabla ya mashindano hayo kuanza lakini mambo yakawa ndivyo sivyo hadi ikaamua kuengua jina lake kikosini.
Nahodha wa timu ya taifa ya Japan, Wataru Endo. Picha na Mtandao
Wataru Endo (Japan)
Maandalizi ya Japan kuelekea Kombe la Dunia la FIFA 2026 yamepata pigo kubwa baada ya nahodha wao, Wataru Endo, kujiondoa dakika za mwisho — siku tatu tu kabla ya kuanza kampeni yao ya Kundi F dhidi ya Uholanzi huko Arlington.
Zaidi ya hayo, kiungo huyo wa Liverpool mwenye umri wa miaka 33 ametangaza pia kustaafu mara moja soka la kimataifa.
Tangu mwishoni mwa Februari, Endo amekuwa akisumbuliwa na jeraha la mguu alilopata akiwa katika majukumu ya klabu yake ya Liverpool, ambalo lilihitaji upasuaji.
Hata hivyo, awali ilionekana kwamba alikuwa amepona vya kutosha baada ya kujumuishwa katika kikosi cha wachezaji 26 cha Samurai Blue.