Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa Tabora Utd watia mgomo, kuivaa Azam

Muktasari:

  • Tabora iliyopanda daraja msimu uliopita ikifahamika kama Kitayosce kabla ya kubadilisha jina, kwa sasa ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ikimiliki pointi 37 zilizotokana na mechi 28, ikishinda 10 kutoka sare saba na kupoteza 11, ikifunga mabao 27 na kufungwa 39.

Dar es Salaam. Wakati kikosi cha Tabora United kikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC itakayochezwa Jumatano wiki hii, inadaiwa wachezaji baadhi wa wa timu hiyo wameweka mgomo baridi wa kutocheza hadi pale ambapo viongozi watakapowalipa mishahara yao ya miezi miwili.

Timu hiyo imebakisha mechi mbili za kuhitimisha msimu huu ikianza ugenini dhidi ya Azam, huku kikosi hicho cha Nyuki wa Tabora, kikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mabao 2-1 katika mechi ya duru la kwanza iliyopigwa Desemba 13, 2024.

Baada ya hapo, Tabora itaufunga msimu kwa kucheza na Coastal Union pia ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga Juni 22, huku timu hizo zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 zilipokutana mechi ya mkondo wa kwanza mjini Tabra Desemba 17, 2024.

Licha ya kikosi hicho kurejea mazoezini kujiandaa na michezo hiyo miwili, lakini mgomo huo umekuja siku chache kabla ya kuanza safari kutoka Tabora kuifuata Azam jijini Dar es Salaam ambapo hadi leo mchana hawakuwa wametoka mkoani humo.

Baadhi ya wachezaji kutoka ndani ya timu hiyo ambao wameomba kuhifadhiwa majina yao, wameliambia Mwananchi kuwa wameamua kuchukua uamuzi wa kugoma kutokana na madai ya mishahara yao ambayo hawajalipwa kuanzia mwezi wa tano na huu wa sita.

"Tumekuwa tukipiga kelele sana juu ya hili lakini viongozi hawaonyeshi ushirikiano wowote jambo ambalo limetufanya kwa umoja wetu kugomea hadi watakapolipa au kusikiliza mahitaji yetu muhimu tunayoyahitaji," amesema mmoja wa wachezaji hao.

Mchezaji huyo alisema suala la kucheza kwao halina shida kwa sababu ndio kazi yao, japo wanachohitaji ni kuona viongozi wanachukulia kwa uzito mahitaji yao, kwani wana familia na watu mbalimbali wanaowategemea katika kuendesha maisha yao.

"Suala hili limeanza kwa baadhi ya benchi la ufundi tangu mwanzoni ambao pia wamekuwa wakiondoka kwa sababu za aina hii na uongozi hauchukulii kwa usiriasi mkubwa, sasa tumeona na sisi wachezaji tufanye uamuzi huu," amesema mchezaji huyo.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny amesema hawezi kuzungumza mambo ya mtandaoni kwa sababu kwa sasa malengo yao ni kuhakikisha wanamaliza mechi mbili vizuri zilizobakia.

"Kama kuna suala la kutolipwa ambalo linaelezwa hilo halijafika bado mezani kwangu na likiwepo sisi kama uongozi tutatoa taarifa, pia inapotokea mtu anadai hawezi kutumia kigezo cha kugoma bali anapaswa kufuata utaratibu," amesema Charles.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tabora United, Richard Abwao ambaye pia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, amesema wamelazimika kukaa kikao na wachezaji kuweka mambo sawa kabla ya kuanza safari ya kuifuata Azam.

"Kwa sasa tupo katika kikao na wachezaji kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya ndani ya timu kabla ya kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kucheza na Azam," amesema kiongozi huyo.

Tabora iliyopanda daraja msimu uliopita ikifahamika kama Kitayosce kabla ya kubadilisha jina, kwa sasa ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ikimiliki pointi 37 zilizotokana na mechi 28, ikishinda 10 kutoka sare saba na kupoteza 11, ikifunga mabao 27 na kufungwa 39.