Mastaa waliombeba Gomes siku 100 Simba

Sunday May 02 2021
LUIS CHAMA
By Thobias Sebastian

ITAKAPOFIKA Mei 4, mwaka huu kocha wa Simba, Mfaransa Didier Gomes atakuwa amefikisha siku 100, tangu alipoanza kibarua cha kukinoa kikosi hicho.

Gomes aliyekuja nchini 24, Januari na kuanza kazi siku hiyo hiyo alichukua mikoba hiyo kutoka kwa Sven Vandenbroeck aliyeondoka pasipo kutegemewa na wengi.

Katika muda huo ambao Gomes amekuwa na kikosi cha Simba kuna mafanikio mbalimbali ameyapata katika mashindano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwenye mafanikio hayo wachezaji wote wa Simba waliopata nafasi ya kucheza kila mmoja alitoa mchango wake kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia malengo.

Gomes akiwa ndani ya Simba kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa watamu kutokana na rekodi zao mbalimbali ambazo wanazo mpaka wakati huu.


Advertisement

Meddie Kagere

Wakati wa Sven Kagere hakuwa anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara na kuna baadhi ya mechi alikuwa akiingia zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya mchezo kumalizika.

Gomes mara baada ya kufika Simba mambo yalibadilika kwa Kagere na straika huyo wa Rwanda akaanza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na ilivyokuwa awali.

Kagere ameonekana kumbeba Gomes kwani mpaka wakati huu ndio kinara wa mabao katika kikosi cha Simba akifunga 11, bao moja nyuma ya kinara, Prince Dube wa Azam mwenye 12.


John Bocco

Amekuwa akipata majeraha ya mara kwa mara ambayo kuna nyakati yanamuweka nje na kukosa mechi nyingi katika mashindano mbalimbali.

Bocco licha ya kupitia changamoto hiyo ameonekana kumbeba Gomes kwani anashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi katika kikosi cha Simba.

Bocco amefunga mabao kumi katika Ligi Kuu na kuchangia kuipa timu yake pointi tatu muhimu kama alivyofunga katika mchezo dhidi ya Mwadui bao lake la pekee lililoipa ushindi timu yake.


Chriss Mugalu

Wakati wa Sven, Mugalu alikuwa akipewa nafasi ila mara nyingi alitokea benchi la wachezaji wa akiba lakini wakati huu mambo ni tofauti kwake.

Mugalu mpaka sasa ameingia katika orodha ya nyota waliombeba Gomes kwani amefunga mabao nane na anakuwa mchezaji wa tatu mwenye mabao mengi kwenye kikosi hicho.

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo amembeba Gomes si katika mashindano tu, bali hata kwenye Ligi ya Mabingwa alifunga mabao mawili kwenye hatua ya makundi.


Clatous Chama

Kiungo fundi roho ya kikosi cha Simba katika kupika mashambulizi, ndiye kitovu cha takribani kila hatari inayojengwa na Simba

Chama katika kikosi cha Simba mpaka sasa amevunja rekodi yake ya mabao aliyofunga msimu uliopita pamoja na pasi za mwisho.

Msimu uliopita Chama alitoa asisti kumi na kufunga mabao mawili, lakini msimu huu kufikia sasa baada ya mechi 25 ametoa asisti 13 na kufunga mabao saba.

Kiungo huyo raia wa Zambia amechangia mabao 20, kwenye kikosi cha Simba amekuwa akionyesha makali yake mpaka katika Ligi ya Mabingwa Afrika.


Luis Miquissone

Miongoni mwa nyota ambao chini ya Gomes wamefaya vizuri ni Miquissone ambaye katika Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya makundi ndio mchezaji aliyefunga mabao mengi.

Katika makundi amefunga mabao matatu, wakati katika ligi ameifungia timu yake mabao saba na kuwa katika orodha ya wachezaji wenye mabao mengi ndani ya timu hiyo

Miquissone amekuwa mchezaji hatari katika kikosi cha Simba na kwenye mashindano yote amefanya vizuri.


Aishi Manula

Kipa chaguo la kwanza katika kikosi cha Simba, ameonyesha kiwango bora kiasi kwamba katika kila mechi timu hiyo imekuwa kwenye mikono salama.

Usalama huo wa Simba ni kutokana na kiwango cha Manula kuimarika zaidi chini ya Gomes na kupunguza makosa yake kama kufungwa mabao ya mbali, mabao ya frii-kiki na mipira ya kona au krosi.


Joash Onyango

Katika kikosi cha Simba, Gomes amekuwa akifanya mabadiliko ya mara kwa mara, lakini si kwa beki wa kati, Onyango ambaye ametumika katika mechi nyingi.

Beki huyu raia wa Kenya, ameonyesha kiwango bora msimu huu pengine tofauti na ambavyo ilitarajiwa wakati anasajiliwa kutoka Gor Mahia ya Kenya. Wengi walimfanyia dhihaka wakitania kuwa ni mzee.

Kebehi hizi zilizidi baada ya kuachwa kwa kasi ya umeme na winga wa Yanga, Tuisila Kisinda, lakini tangu hapo amethibitisha kuwa yeye ni ‘nusu mtu nusu chuma’.

Mbali ya kujenga ukuta wa chuma, Onyango ameifungia Simba bao moja na asisti moja.

Advertisement