Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maswali mabilioni ya Mo Simba

Muktasari:

  • Katika mchanganuo wa fedha hizo, Mo alisema ametumia Sh45 bilioni kulipa mishahara, kufanikisha usajili, maandalizi ya timu na uendeshaji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji 'MO' usiku wa Julai 14, 2025, alitumia muda huo kuzungumza na Wanasimba na wapenda soka kwa ujumla huku akitaja mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya klabu hiyo ikiwemo suala la uwekezaji wake.

Mo ambaye hii ni mara ya pili anafanya hivyo kupitia akaunti yake ya Instagram baada ya awali Juni 11, 2024 kuzungumza, amesema klabu hiyo itarudi kwa nguvu msimu ujao, huku akitangaza maboresho ya kikosi.

Akizungumzia mchango wake ndani ya Simba, bilionea huyo amesema kuanzia mwaka 2018 hadi sasa ametumia kiasi cha Sh87 bilioni kwa matumizi mbalimbali ndani ya klabu hiyo.

Katika mchanganuo wa fedha hizo, Mo alisema ametumia Sh45 bilioni kulipa mishahara, kufanikisha usajili, maandalizi ya timu na uendeshaji.

Tajiri huyo alisema pia ameweka Sh20 bilioni kama sehemu ya ununuzi wa hisa asilimia 49 za mwekezaji ndani ya klabu ya Simba. Pia ametumia Sh22 bilioni kuanzia 2017 hadi 2024 kwenye misaada mbalimbali pale ambapo imekuwa ikihitajika Simba.

"Kusema kwamba Mo hatoi fedha hiyo ni kauli ya kupotosha yenye mwelekeo wa chuki. Tuachane na fitina Wanasimba wenzangu, tuzibe panapovuja, tuzibe ufa," alisema Mo.


USAJILI

“Msimu ujao tunarejea kwa nguvu mpya, kipaumbele chetu kikubwa kitakuwa kwenye usajili makini na wa kimkakati tukilenga kuleta Wachezaji bora watakaoongeza ushindani bora na kina ndani ya kikosi, sambamba na hilo tutaongeza nguvu kwenye benchi la ufundi ili kuhakikisha timu yetu inapata mwongozo sahihi wa kufikia mafanikio, nimetenga fedha za kutosha kuhakikisha timu yetu inakuwa bora zaidi," alisema Mo ambaye pia ni rais wa heshima wa Simba.


MALENGO

Simba iliyomaliza nafasi ya pili kwenye ligi na Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia kupoteza fainali mbele ya RS Berkane, malengo ya Mo ni kuona siku moja timu hiyo inakuwa bingwa wa Afrika.

“Msimu huu haukuwa rahisi, tumepitia changamoto nyingi lakini tumeonesha uimara mkubwa, leo hii Simba inashikilia nafasi ya tano kwenye viwango vya CAF huku bado tukiwa katika mchakato wa kujenga upya kikosi chetu, ni mafanikio ya kujivunia kwa klabu iliyokuwa nafasi ya 85 mwaka 2017/18 wakati uwekezaji ulianza, Simba imeendelea kuandika historia.

"Ni klabu pekee kutoka Tanzania kufika fainali ya CAF mara mbili ingawa hatukutimiza kila lengo tumeonesha dhamira tukipambana kwa heshima na moyo wa Simba, bado ndoto yangu ni ileile kuipa Simba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Wakati Mo akibainisha kutumia kiasi cha Sh87 bilioni ndani ya Simba kipindi hicho, kuna maswali kibao yamebaki vichwani mwa wadau wengi wa soka wakihoji bajeti, mikataba ya udhamini na fedha za mafanikio inazopata timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali zinafanya kazi ipi.

Mbali na hilo, pia fedha za viingilio vya mlangoni ambavyo Simba imekuwa na rekodi nzuri ya kujaza viwanja ikiwemo Benjamin Mkapa, mapato yanakwenda wapi.

Swali lingine ambalo wengi wanajiuliza, kama Mo anatoa fedha za usajili kisha haoni mabadiliko huku akiahidi kuendelea kutoa, viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia usajili wanawajibikaje, kwa nini asiwawajibishe kwa kushindwa kufikisha malengo yake na klabu kwa ujumla.

Ukiangalia msimu uliomalizika, Simba ilisajili wachezaji 14 wapya, ambapo hadi sasa kati ya hao wapya, imeachana nao watatu ambao ni Valentine Nouma, Augustine Okejepha na Kelvin Kijili, huku mmoja ikimtoa kwa mkopo Omary Omary. Hata hivyo, inaelezwa haijaishia hapo, kuna wengine watakatwa kabla ya usajili kufungwa Septemba 7 mwaka huu.


FEDHA ZA CAF

Simba kuanzia 2018-2019, imefanikiwa kucheza angalau robo fainali ya michuano ya CAF, huku msimu uliopita ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika kipindi chote hicho cha kufanya vizuri kwa Simba, timu hiyo imeingiza fedha kutoka CAF ikiwa ni kwa kiwango cha tofauti.

Mchanganuo wa fedha hizo upo hivi; msimu wa 2024/25 ambao imecheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikimaliza nafasi ya pili, imepata Dola milioni 1 ambazo ni takribani Sh2.6 bilioni za Kitanzania.

Katika michuano hiyo pia msimu wa 2021/22, Simba iliishia robo fainali na kupata dola 350,000 ambazo ni takribani Sh909 milioni.

Upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imecheza robo fainali nne ambazo ni msimu wa 2018/19, 2020/21 na 2022/23 na 2023/24. Katika misimu hiyo, zile tatu za kwanza iliambulia dola 650,000, takribani Sh1.7 bilioni kila msimu na 2023/24 ikachukua dola 900,000 ambazo ni takribani Sh2.3 bilioni.

Kwa ujumla, kupitia mafanikio ya michuano ya CAF, Simba imeingiza takribani Sh10.9 bilioni ndani ya kipindi cha kuanzia 2018 hadi 2025.


BAJETI YA KLABU

Kwa misimu miwili ya karibuni, Simba bajeti yake ya mwaka ni jumla ya Sh53.8 bilioni ambapo msimu wa 2023/2024 ilikuwa

Sh25 bilioni na 2024-25 ni Sh28.4 bilioni.

Kwa mujibu wa Simba, bajeti ya msimu hutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo udhamini kutoka makampuni mbalimbali.

Katika bajeti ya msimu uliopita ambayo ilipitishwa na wanachama ilionyesha kuwa Simba ilitrarajiwa kupata shilingi 2.9 bilioni kutoka kwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo, M-Bet, 1.5 bilioni kutoka kwa mdhamini wa jezi, milioni 155 mdhamini wa Ligi Kuu Benki ya NBC, milioni 500 Kampuni ya Serengeti, milioni 250 kutoka Kampuni ya A1 na shilingi milioni 250 kutoka vyanzo vingine

Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa klabu hiyo, Suleiman Kaumbu mbele ya wanachama 700 waliohudhuria mkutano huo alisema kuwa Mo ametoa sh 7 bilioni ambazo zilianza kutumika kusajili mastaa wapya klabuni hapo.


WADAU WANASEMAJE?

Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alisema kauli alizozitoa Mohamed 'MO' Dewji, zinategemea na ushirikishwaji nje na hapo atakuwa hajawatendea haki wengine.

"Kama hizo pesa alizokuwa anazitoa alikuwa anawashirikisha viongozi wengine wa Simba basi ana haki ya kutoka hadharani na kuyasema hayo, kama alikuwa anafanya kwa utashi wake kutoa pesa bila wengine kujua hilo halijakaa sawa," alisema Mogella na kuongeza.

"Kitu pekee ninachoweza kushauri wanahitaji utulivu na vitu vifanyike kwa uwazi zaidi, nasisitiza kama pesa alizotoa Mo Dewji walishirikishwa basi ana haki kabisa kutoka hadharani."

Katibu wa kundi la ushangiliaji la Simba la Ubungo Terminal, Joel Mwakitalima alisema: "Kama kweli Mo Dewji anatoa pesa ndefu hivyo, basi amewafumbua macho watu, hadi anatoka hadharani kuzungumza huenda anaona zinatumika sivyo ndivyo.

"Kitu ninachoweza kuwashauri viongozi wa Simba wachangamke kama ilivyo kwa wenzao Yanga, wamepoa sana wakati hiyo ni klabu kubwa Afrika, jambo la msingi ambalo tajiri kalizungumza ni mshikamano wa kuhakikisha tunavuka tulipo."

Mtaalamu wa uchumi wa magazeti ya Mwananchi, Ephrahim Bahemu amesema kwa ukubwa wa klabu kama Simba si ajabu kuwa imewezeshwa kiasi hicho cha pesa kilichotajwa kwa muda husika ikizingatiwa kuwa klabu zetu kubwa kwa sasa zinatumia kwenye usajili, mishahara ya wachezaji na utunzaji wa timu.

“Swali muhimu sasa pengine ni viongozi kuwaeleza wanachama juu ya vyanzo vingine vya mapato vinatumikaje maana kiasi kinachotajwa ni karibu thamani ya bajeti ya klabu hivyo pengine mapato mengine kama viingilio na malipo ya wadhamini mbalimbali yamehifadhiwa sehemu,”

Aliongeza kuwa kwa uwekezaji huo wa Mo bila shaka thamani ya klabu imongezeka muhimu ni kuwa na uwazi wa matumizi ya pesa hizo ili kuondoa utata kwa kuwa kiwango hicho kinanoneka kikubwa kuliko inavyoweza kufikirika.