Mayele amtisha beki Monastir

US MONASTIR ya Tunisia leo itamalizana na Yanga katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini beki mmoja wa timu hiyo ametamka wana presha kubwa na straika wa Yanga, Fiston Mayele akisema jamaa ni tishio.

Yanga itavaana na Monastir katika mechi itakayopigwa leo Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kusaka tiketi ya robo fainali na beki huyo, Ousmane Ouattara ameliambia Mwanaspoti kwa simu saa chache jana kabla ya kuanza safari ya kuja nchini kuwa Mayele ndiye mtu ambaye anawasumbua vichwani.

Ouattara aliyewahi kucheza na mastaa wengi wa Yanga enzi akiwa AS Vita alisema anamjua Mayele tangu wakiwa DR Congo lakini huyu Mayele wa Yanga yuko moto sana.

Alisema kasi yake ya kufunga na anavyoshirikiana na wenzake sio kitu rahisi kwao kusimamisha kasi yake, lakini watapambana naye dakika 90 zingine.

“Tunaijua Yanga ni timu nzuri. Wako nyuma yetu kwenye msimamo hata kama tuliwafunga huku haina maana kwamba itakuwa rahisi tena kuwafunga wakiwa kwao,” alisema Ouattara.

“Mtu ambaye tunatakiwa kuwa naye makini ni Fiston (Mayele). Sote tutakubaliana kwamba kwa sasa amekuwa katika kiwango bora sana tofauti na alivyokuwa Vita. Haikuwa rahisi kabisa kumzuia mchezo wa kwanza ambao hakufunga.

“Hatutacheza kwa kumuangalia mchezaji mmoja kwa kuwa Yanga ina wachezaji wengi bora ambao baadhi yao nawajua, lakini Fiston ni mtu ambaye anatakiwa kuwekewa umakini kutokana na ubora wake wa sasa.”

Ouattara aliongeza kuwa katika mchezo huo hawana watakachopoteza, lakini wanakuja na akili ya kulinda heshima na kutengeneza rekodi kuelekea hatua ya robo fainali.

“Kitu kibaya ni kwamba nakuja tena Tanzania uwanja ambao sijawahi kushinda tangu tunakuja kucheza na Simba nikiwa AS Vita, lakini tunakuja kulinda heshima yetu. Tunataka kuongoza kundi tukibaki kuwa vinara na kuweka rekodi yetu.”

Monastir ndiyo vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi 10, huku Yanga ikifuata na alama saba na TP Mazembe itakayomalizana na Real Bamako mjini Bamako inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu ilhali wenyeji wao wanaburuza mkia na pointi mbili, huku kila timu imecheza mechi nne.