Mayele, Bangala wamvuta nahodha TP Mazembe Jangwani

Saturday November 27 2021
mayelepic
By Ramadhan Elias
By Leonard Musikula

KIWANGO wanachokionesha mastaa wapya wa Yanga kutoka DR Congo, Fiston Mayele, Yannick Bangala, Jesus Moloko, na Djuma Shaban kimemuibua nahodha wa zamani wa TP Mazembe, Yannick Tusilu na kuwapigia saluti.

Tusilu ambaye kwasasa anakipiga nchini, katika klabu ya DTB inayoshiriki Championship ni miongoni mwa mastaa waliowahi kukiwasha pale Mazembe na kupewa unahodha huku akiwa na rekodi kibao akicheza na Mbwana Samata,

Tressor Mputu na Rainford Kalaba kwenye kile kikosi kilichotwaa ubingwa wa Afrika 2015, pia aliwahi pia kucheza michuano mikubwa ya klabu Bingwa Dunia akiwa na Mazembe.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na kiungo huyu maarufu kama ‘Kaka’ ambapo amewazungumzia kina Mayele na kusema Yanga imepata bahati kuwa na wachezaji kama wale;

“Naweza kusema Yanga imepata wachezaji wa daraja la juu, wameanza msimu vizuri na kutokana na viwango wanavyovionyesha uwanjani kila timu inatamani kuwa na wachezaji kama wale kwani tangu wapo DRC wamekuwa na kiwango bora kinachomvutia kila mtu,” alisema Tusilu na kuongeza;

“Wote wale ni wachezaji wakubwa tena wenye uzoefu na wametoka timu kubwa hivyo Yanga inabahati kubwa kwani wanajua nini wanafanya na wataisaidia sana kufikia malengo yake,” alisema Tusilu.

Advertisement

Aidha pia Tusilu alifunguka namna wachezaji kutoka DRC wanavyopenda na kujivunia kuja kucheza soka Tanzania kutokana na namna mazingira yalivyo.

“Ingawa ni mara yangu ya kwanza kucheza hapa nchini lakini uwepo wa wachezaji wengi wanaotokea DRC kunaonyesha kua soka la Tanzania ni kubwa tena lenye ushindani mkubwa na sababu hii imewavutia wachezaji wengi waje kwani kuns mazingira rafiki kwa mchezaji,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mwinyi Zahera ambeye piac ni Mkongomani alifunguka kuwa kina Mayele, Djuma, Moloko, Bangala, Mukoko Tonombe na Heritier Makambo wanajitambua ndio maana wanafanya vizuri pale Yanga.

“Ubora wao kila mmoja ameuona, na namna kila mmoja anavyocheza unaona kabisa anakiu ya kufanya vizuri zaidi nadhani hio ndio sababu kuu inanyowafanya wanang’ara kwenye ligi hii na kadri siku zinavyosonga wanazidi kuimarika zaidi,” alisema Zahera.

Wakongomani hao, Djuma, Mayele, Moloko na Bangala wamejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha Yanga huku Mukoko na Makambo nao wakiwa na nafasi kubwa ya kuingia kutokea benchi.


Advertisement