Mbeya City yajipiga kifua ikipoteza kwa Azam FC
Muktasari:
- Mbeya City ni miongoni mwa timu mbili zilizopanda Ligi Kuu msimu huu, nyingine ikiwa ni Mtibwa Sugar.
Mbeya. Licha ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC, katika mechi ya kilele cha Tamasha la Mbeya City Day leo Jumamosi, Septemba 6, 2025, Mbeya City imetamba kufanya vyema katika Ligi Kuu msimu ujao.
Mbeya City ikiadhimisha siku yake kwa tamasha hilo, ilicheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Azam FC na kulala mabao 2-0 yakifungwa na Landry Zouzou dakika ya 18 na Ben Zetoun dakika ya 82.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Malale Hamsini amesema pamoja na matokeo hayo, lakini anawapongeza vijana wake kwa ubora walioonesha.
Amesema kilichowaangusha ni ukubwa wa jina la Azam na kukosa utimamu wa mchezo kama walivyo wapinzani ambao wamekuwa na michezo kadhaa ya kirafiki ndani na nje ya nchi.
"Ratiba yetu ni ngumu na tumeona mechi tunazoanza nazo, Ila niwahakikishie ligi inapoanza hadi mchezo dhidi ya Yanga hapa Sokoine mtaona maajabu yetu,”amesema Malale.
Ameongeza kuwa kwa muda uliobaki, timu itaendelea kujifua kwa ajili ya ligi akieleza kuwa michezo miwili wanayoanzia ugenini dhidi ya Fountain Gate na Azam FC watafanya kweli akiomba ushirikiano zaidi kwa mashabiki.
Naye Afisa Habari wa timu hiyo, Gwamaka Mwankota amesema kwa muitikio wa mashabiki katika tamasha hilo wanaenda kulipa fadhila kwa matokeo mazuri katika Ligi Kuu.
Amesema mbali na matokeo ya kupoteza leo, lakini City ni machinjio inayotembea na shughuli inaenda kuanzia Babati katika uwanja wa Kwaraa kuwatembezea kipigo Fountain Gate.
"Bado malengo yetu ni yaleyale, hii ni machinjio inayitembea, tutampiga yeyote tutakayekutana naye, niwapongeze na kuwashukuru mashabiki kwa namna walivyoitikia tukio hili," amesema Mwankota.