Mikasa 9 ya kibabe ya Hans Poppe Simba

NI msiba wa wanamichezo kutokana na kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Zacharia Hans Poppe ambaye roho yake iliacha mwili usiku Septemba 10, 2021.

Umauti wa Hans Poppe umemkuta akiwa Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam akiwa anapigania afya yake baada ya kupumzishwa hapo kwa takribani wiki mbili.

Ndani ya Simba Hans Poppe alikuwa na nguvu kubwa, kwa sasa unaweza kusema ukimwondoa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mohammed Dewji ‘MO’ na makamu wake Salim Abdallah ‘Try again’ basi anayefuata alikuwa Hans Poppe.

Hapo nyuma kabla ya ujio wa MO Hans Poppe ndio alikuwa alfa na omega, ndani ya Simba alikuwa hachoki kutumia fedha zake kuhakikisha Simba inakaa sawa sawa, lakini baadaye baada ya kuja kwa mabadiliko ya kiuongozi baada ya mchakato wa uwekezaji, hapo ndipo kijiti alipokipokea MO na Try again na yeye akibaki kuwa mjumbe ingawa bado alikuwa na nguvu yake.

Hebu tuangalie matukio ya kibabe ambayo Hans Poppe alikuwa akiyafanya enzi za uhai wake ndani ya klabu ya Simba aliyoipigania mchana na usiku kuhakikisha inakaa sawa.


AMLIPUA RAGE KWENYE NDEGE

 Wakati wa utawala wa mwenyekiti Ismail Rage wakati fulani mambo yalikuwa hayaendi na Hans Poppe ndio alikuwa akitoa fedha nyingi kuihangaikia Simba. Akaanzisha mpango wa kumwondoa Rage madarakani.

Wakati kikao hicho kinafanyika Rage hakuwepo nchini nyuma yake yakafanyika mapinduzi kwa kikao cha kamati ya utendaji kuitishwa na wakapiga kura ya kukosa imani na Rage kisha mambo yakawekwa hadharani.

Baadaye Hans Poppe alisafiri na kurudi ndani ya siku chache, akakutana na Rage ndani ya ndege na akaulizwa juu ya mapinduzi hayo, Hans Poppe hakumung’unya maneno, aliweka wazi ni kweli mapinduzi yamefanyika na zaidi yeye alikuwemo na ameshiriki kupiga kura, kauli hiyo ilimwacha Rage mdomo wazi akishangaa ujasiri huo. Hata hivyo, Rage alifanikiwa kurudisha nafasi yake baada ya kutua nchini.


 AWALIPUA WACHEZAJI KINESI

Katika utawala huo huo wa Rage, Simba ilishuka ubora ndani na nje ya uwanja. Wakati huo, kikosi kilikuwa kikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, pale Ubungo.

Baada ya hali ngumu ya kifedha wachezaji walikosa michahara na hivyo waligoma wakitaka kujua kulikoni.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi waliogopa kwenda kutuliza hali, lakini Hans Poppe aliibuka mazoezini akakuta wachezaji wanamalizia mazoezi, huku mashabiki wachache wakiwa jukwaani.

Alipouliza kipi wanataka kisha kuelezwa kuwa ishu ni mishahara jamaa akaibuka na kusema: ”Nyinyi hamshindi uwanjani mnatarajia Simba itapata wapi fedha? Mashabiki hawaji viwanjani kwa sasabu hamjitumi sasa hapa fedha hakuna msidanganyane mkishinda mashabiki watakuja na tutawalipa kwa hiyo kazi kwenu labda nitawaachia nauli kidogo tu’” alisema Hans Poppe kisha akaingia mfukoni akatoa kibunda na kuwapa wagawane. Mashabiki walimshangilia huku wachezaji wakitoka vichwa chini na kazi iliendelea.


 AMPIGIA MANJI, AMCHIMBA MKWARA

Wakati Hans Poppe anaibeba Simba kule Yanga mambo yalikuwa safi hakuna walichokosa wakiwa chini ya Bilionea Yusuf Manji.

Manji aliisumbua Simba anavyotaka kila aliposikia wekundu hao wanamtaka mchezaji flani alikuwa anavamia na kumzoa anavyotaka, hali ile ilikuwa inampandisha mlima Hans Poppe akilazimika kutunisha msuli kupata mchezaji wanayemtaka Simba.

Hali ilipozidi kuwa mbaya hakuficha alimpigia simu Manji na kumwambia aachane na hiyo tabia sio kila mchezaji anayetakiwa na Simba yeye amvamie akimtaka kutumia fedha zaske kwa ustaarabu na sio kuwanyanyasa wengine, kauli ile ilimfanya Manji acheke huku Poppe akikata simu kwa hasira.


AUTAKA UENYEKITI, SIMBA WAMZUNGUKA

Wakati Rage anaondoka madarakani Hans Poppe alitaka kuwa mwenyekiti wa Simba lakini kulikuwa na kizuizi kimoja cha kuhusu kuwahi kushtakiwa kwa kesi ya uhaini na alianza kupambana kuondoa kizuizi hicho baada ya kuona watu wanaoiongoza wanashindwa kuiinua Simba.

Kumbuka Hans Poppe alikuwa mjumbe katika kundi lenye nguvu la Friends of Simba (FOS) na inasemekana wenzake wakashtuka kwa ubabe wake akifanikiwa na kuingia ndani nani anaweza kumzuia na maamuzi yake?

Wakamfanyia mpango akwame ili asipate na mchezo huo ukafanikiwa lakini wakamtoa kafara mmmoja wa waajiriwa wa Simba (yupo sasa ndani ya sekretarieti ya Simba) aonekane alifanya makosa na alimwondoa kazini kwa makosa hayo ila lengo la wenzake lilifanikiwa na Evance Aveva akaingia madarakani.


 AJICHOTEA MGAO WA MAUZO YA OKWI

Fedha za Hans Poppe ndio zilitumika kumsajili Emmanuel Okwi baada ya Simba kunusa mkataba wake uko mwishoni na kuna ofa ya Etoile du Sahel inakuja baada ya mashindano ya Chalenji kule Kenya.

Hans Poppe alisafiri na Rage mpaka Kenya kwenda kumalizana na Okwi akitumia fedha zake kwa makubaliano kama mshambuliaji huyo atauzwa Simba itamrudishia fedha zake na wakafanikiwa baada ya miezi michache Okwi aliuzwa rasmi Etoile lakini zile fedha zilichelewa sana kuja Simba na kuzusha taharuki kubwa.

Fedha zile zilifika wakati Rage akiwa ameondoka madarakani na utawala wa Evance Aveva ukiwa madarakani, Hans Poppe akakumbuka ahadi ni deni, akataka chake kwanza kirudishwe tena bila riba na bahati mbaya wakati huo uongozi wa Aveva ulikuwa na malengo makubwa na fedha zile wakitaka kujenga uwanja kule Bunju.

Hans Poppe hakuwaelewa na sakata lile lilifika kwa kiongozi mmoja wa juu wa serikalini, kina Aveva wakitaka msaada wa kumtaka Poppe asifanye anachotaka kwani kitafifisha malengo ya uongozi. Hata hivyo, Poppe alipoitwa, akasisitiza fedha zake anazitaka na alishinda na kupewa fedha hizo.


 AMLIPUA KAPOMBE KISA MAJERAHA

Simba ilimsajili beki Shomari Kapombe na baada ya usajili alikuwa akiuguza majeraha mara kwa mara. Hata hivyo, klabu ilimvumilia.

Baadaye Hans Poppe akihojiwa na chombo kimoja cha habari, alionekana kuchoka kumsubiri Kapombe apone na kumtaka hadharani atoke na aseme lini atakuwa amepona akisema Simba itachoka kumsubiri.

Kauli ile ilimkera sana Kapombe. Hata hivyo, ilionekana ni kama ilisaidia na kumrudisha kwa nguvu kwani alikuwa katika nyakati za mwisho kupona na aliporejea aliupiga mwingi na mpaka sasa hajakaa tena nje kwa muda mrefu.


AMLIPUA MANARA

Kuna tukio moja lilitokea nchini DR Congo na aliyekuwa msemaji wa Simba Haji Manara alianzisha vurugu kubwa katika hoteli iliyofikia Simba.

Ni baada ya Simba kulala kwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita. Manara alichukizwa na tukio la mwandishi wa Clouds FM, Shafih Dauda kuweka kibonzo kimoja ya jitu kubwa likipigana na ‘kamtu’ kadogo na Manara kutafsiri Dauda anaidhihaki Simba.

Wakati wa vurugu hizo Manara akikaribia kuzipiga na Dauda, huku baadhi ya viongozi wakiwa upande.

Hans Poppe akauliza nini shida na Manara akamsimulia, bahati mbaya Hans Poppe hakumung’unya maneno na kujibu, “Hivi wewe Haji una akili timamu? Hapa kilichokufanya wewe ukasirike ni kipi? Mbona hiki ni kitu kidogo sana? Kuna mtu anakera kama wewe kwa maneno machafu na mbona hakuna anayekupiga? Hebu acha kelele,” Manara haraka akanyamaza na maisha yakatulia.


AWALIPUA MIQUISSONE NA CHAMA

Msimu mmoja uliopita Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga, wekundu wakitangulia kupata mabao 2 kisha yakarudishwa.

Hans Poppe alikerwa na matokeo yale akatoka hadharani na kudai wachezaji Luis Miquissone na Clatous Chama walicheza chini ya kiwango na wanatakiwa kuwekwa kitimoto, hakujali ukubwa wa majina yao nyakati hizo.

Baada ya kusema hivyo, Hans Poppe baadaye alitangaza vita akasema atakuwa akitembea na rungu ili akimnasa mtu au mchezaji anayetaka kuihujumu Simba rungu hilo litamhusu kauli ambayo ilizua gumzo na baada ya mechi hiyo mchezo uliofuata baina ya tim hizo Simba ilishinda kibabe kwa mabao 4-1 na wachezaji hao aliowatuhumu walicheza vizuri na wakafunga mabao.


ACHAFUA HALI YA HEWA KESI YA MORRISON

Hakuna kesi ya Simba inapomgombea mchezaji na Hans Poppe awe ndani ya kamati, kisha ikampoteza mchezaji.

Kesi ya kwanza ilikuwa ni kwa Okwi wakati anataka kuondoka Yanga na Poppe alikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya sheria na hadhi za wachezaji na Yanga walilalamika Okwi akirudishwa Simba.

Kikao hicho kilichofanyika katika hoteli ya Colloseum pale Masaki.

Kesi ya pili ni hivi karibuni alipokuwa kwenye kamati ya TFF ikimhusu mshambuliaji Bernard Morrison.

Akiwa humo, Hans Poppe alicheza karata ndani ya kikao na alipokuwa anatoka nje akawa anatoa taarifa za kikao hicho kwa Simba.

Kamati ilipojua hilo ilimchukulia hatua na alipelekwa kamati ya nidhamu. Hata hivyo, Simba tayari ilikuwa ishamchukua Morrison.


ALICHANGIA UKUAJI WA FILAMU

Wakati wa uhai wake Hans Poppe hakuwa tu kwenye soka. Alipenda pia kushikiri kwenye tasnia nyingine kama burudani na aliwahi kushiriki kuunda umoja wa PAPAZI kwa ajili ya kukuza sanaa wa nyota wa filamu Tanzania na miongoni mwao alikuwepo Jackline Wolper.


KWENYE NGUMI PIA ALIHUSIKA

Pia alisaidia pakubwa kwenye mchezo wa ngumi na aliwasaidia mabondia mbalimbali waliofika kwake kueleza shida zao.


AJENGA UWANJA

Hans Poppe alikuwa anaishi Ununio Mbezi na kwa kushirikiana na majirani zake, walijenga uwanja wa Boko Veteran.

Uwanja huo ulitumika kwa mazoezi ya Simba na Yanga waliokuwa wakiukodi, huku Simba ikipata punguzo kutokana na Hans Poppe kuwa ndani ya uongozi wa wanaomiliki uwanja huo.


AMPA TSHABALALA GARI

Hans Poppe alifanya mengi ndani ya Simba lakini tukio la kipekee ni pale alipokoshw ana kiwango cha beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na kuamua kumzawadia gari ya kisasa aina ya Toyota Raum.

Pumzika kwa Amani Zacharia Hans Poppe wanamichezo watakukumbuka kwa moyo wako na uliyoyafanya yatabaki kuwa elimu kwetu.