Prime
Mikataba mastaa Simba hasara tupu
Muktasari:
- Dalili hizi zinaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa Simba ikatumia kitita kikubwa zaidi cha fedha sokoni kuliko kile ambacho ilitumia mwanzoni mwa msimu uliopita.
Klabu ya Simba ipo kwenye mtego mbaya kuhusu mikataba ambayo ilitoa kwa wachezaji wake na kuna hatari ikatumia kitita kikubwa cha fedha kwenye dirisha hili la usajili au ukawapoteza mastaa wake wengi.
Hiki ni kipindi cha dirisha kubwa la usajili Ligi Kuu Bara, Championship, Ligi ya Wanawake, First League pamoja na timu za vijana ambapo usajili huo ulifunguliwa Julai Mosi na utafungwa Septemba 7, 2025.
Katika dirisha lililopita la usajili, Simba iliachana na kundi kubwa la wachezaji na kusajili wachezaji 17 wapya ikiwa inaelezwa kuwa wanakwenda kujenga timu mpya na kwa mujibu wa klabu hiyo kila mchezaji alisaini kuanzia miaka miwili na kuendelea ambapo wageni wengi walipewa miaka mitatu wakiwa na wastani wa miaka 24.
Hadi sasa, Simba ndiyo timu kwenye Ligi Kuu Bara ambayo wachezaji wake wengi wameondoka, ikiwa imeshaachana na Aishi Manula aliyejiunga na Azam, Kelvin Kijili aliyerudi kwenye timu yake ya zamani Singida Black Stars.
Wengine ni Hussein Kazi inayedaiwa kuwa ametua Namungo, Fabrice Ngoma ameshaaga na anaweza kujiunga na timu nyingine muda wowote kuanzia sasa, pamoja na Valentin Nouma ambaye juzi aliwaaga mashabiki wa timu hiyo.
Mbali na wachezaji hao kuondoka, lakini klabu hiyo imepata hasara kubwa kwa kuwa mastaa hao wote wameondoka bure na fedha za usajili wataweka mfukoni mwao, kutokana na aina ya mikataba ambayo walikuwa wamesaini na timu hiyo.
Mikataba ikoje
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kinasema kuwa aina ya mikataba ya klabu hiyo ilibadishwa kuanzia dirisha la usajili lilopita ambapo klabu ilikuwa ikitangaza kuwa wachezaji wamesaini mikataba ya miaka mitatu, lakini kiuhalisia ulikuwa mwaka mmoja.
"Mfumo wa mikataba ya Simba ilibadilishwa kwenye kipindi cha usajili kilichopita, wachezaji walikuwa wanasaini mkataba wa mwaka mmoja lakini una kipengele cha kuongeza miaka miwili, sasa athari yake ni kwamba mchezaji akimaliza mwaka mmoja kama hajaridhika na klabu anaweza kuondoka bure na kama klabu haijaridhishwa naye inaweza kumuacha akatimka bure ndicho kinachotokea sasa.
"Ukitazama kundi la wachezaji wanaoondoka, ukiacha Aishi Manula ambaye walimuacha hadi mkataba wake umalizike aondoka bure hawa wengine wote wametumia kigezo hicho, hivyo klabu imepata hasara kwa kuwa kama wangeuzwa timu ingeingiza fedha nyingi sana za kutumia kwenye usajili huu," kilisema chanzo kutoka Simba.
Kwa upande wa Kijili amesema yeye amejiunga na Singida Black Star kwa kuwa alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Simba.
"Mkataba niliopewa ulikuwa wa mwaka mmoja, lakini una kipengele cha kuongeza mwaka mwingine hivyo kwa kuwa nilikuwa sijazungumza na mabosi kuhusu kuongeza, nimeondoka kwa kuwa mwaka umeisha.
"Nimefurahia kujiunga na Singida Black Stars. Hii ni nafasi nyingine ya kuonyesha uwezo wangu na kusaidia timu kufikia malengo yake msimu ujao. Najua changamoto ni nyingi, lakini nipo tayari kupambana.”
Hata hivyo, beki huyo alisema fedha ya usajili ambayo alipewa wakati anasaini mkataba ilikuwa ya mwaka mmoja tu na siyo vinginevyo.
Mbali na wachezaji, pia klabu hiyo ina kipengele hicho hata kwa kocha mkuu wa timu hiyo Fadlu Davids, pamoja na wasaidizi wake, isipokuwa Selemani Matola ambaye alisaini kabla mfumo huu mpya haujaanza.
"Kwa Fadlu labda kama walimalizana mwishoni wakati anaondoka kwenda mapumzikoni, lakini naye mkataba wake ulikuwa wa miaka mitatu lakini 'option' ni hizohizo kama wachezaji, alitakiwa kumaliza mwaka mmoja halafu aongeze mmoja, sasa hofu hapa ni kama atapata dili sasa hivi na kuondoka, hakuna mwenye uwezo wa kumzuia na hatalipa fedha yoyote kwa uongozi.
"Kwa Matola yeye alisaini kabla ya mfumo huu, sina uhakika sana lakini alisaini miaka miwili ya moja kwa moja na mkataba wake ulimalizika mwishoni mwa msimu, kama wamemalizana naye sijui, lakini atakuwa ni kocha huru kwa sasa kama hajasaini tena."
Kama mfumo huu ndiyo ulitumika kwa wachezaji wote ina maana kuwa bado mashabiki wanatakiwa kuendelea kusubiri kuona kile ambacho kinaweza kutokea kwa mastaa wengine ambao walionyesha kiwango bora kwenye timu hiyo msimu uliopita, akiwemo Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua, Moussa Camara, Abdulrazack Hamza, Shomari Kapombe na wengine ambao walitarajiwa kuwika na timu hiyo msimu ujao.
Simba inapata hasara hapa
Pamoja na mambo mengi, ili klabu yoyote iweze kufanikiwa duniani suala la kuuza wachezaji ni moja ya njia yake kubwa ya mapato na mfumo huo umekuwa ukitumika kote duniani.
Hata hivyo, hali hiyo imekuwa tofauti ya kwa Simba msimu huu ambapo wachezaji wengi wameonekana kuondoka bure na kuipa hasara kubwa klabu hiyo.
Kitendo cha kudaiwa kuzigomea klabu kadhaa kwa msimu uliopita ambazo zilikuwa zikimtaka Manula ni kuonyesha kuwa timu hiyo ilikuwa tayari kupata hasara, kwa kuwa baada ya msimu kumalizika ameondoka bure ikiwa msimu mzima uliopita alilipwa, mishahara, alipewa posho za mechi kama wachezaji wengine, alilipiwa nyumba na vitu vingine ambavyo alitakiwa kupewa kwa mujibu wa mkataba wake, lakini hakufanikiwa kucheza mchezo hata mmoja wa mashindano akiwa alipata dakika 45 tu kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Ayoub Lakred ambaye amecheza kwa msimu mmoja ndani ya Simba huku mmoja akitumika kuuguza majeraha yake akiondolewa kabisa nje ya mfumo Simba pia walipata msala kwani walishindwa kuvunja mkataba wa kipa huyo na kuamua kuingia tena sokoni kutafuta mbadala wake.
Lakred alijiunga na Simba Agosti 11, 2023 aliitumikia timu hiyo kwa msimu mzima na baadaye uongozi ulishawishika kumuongeza mkataba mwingine ambao aliusaini Julai 8, 2024 ambao hajautumikia hata kidogo kutokana na kupata majeraha ya misuli ya paja akiwa kambini Misri, jeraha ambalo liliwafanya viongozi wa timu hiyo kurudi sokoni.
Kipa huyo amedumu Simba msimu mzima bila kucheza mechi yoyote akiondolewa kwenye mfumo na nafasi yake kuchukuliwa na Mbrazil Jefferson Luiz ambaye aliishia kambini nchini Morocco na ndipo Simba walipomsajili Moussa Camara ambaye naye ana mkataba kama mastaa wenzake wa timu hiyo.
Hii ina maana kwamba hata kama Simba ingemuuza Manula kwa shilingi 50 milioni, ingekuwa imeokoa mishahara yake ya zaidi ya miezi 12, pamoja na marupurupu yake jambo ambalo lingekuwa faida kwa klabu hiyo na fedha hizo ingeweza kuzitumia kwenye usajili wa mastaa wengine kwenye dirisha hili.
Lakini pia kitendo cha kuwaacha nyota wake akiwemo Mohammed Hussein 'Tshabalala' hadi sasa akiwa mchezaji huru ni hatari na kuna uwezekano mkubwa akapata timu muda wowote na kuondoka bure kama alivyofanya Manula.
"Tshabalala ni mchezaji huru kwa sasa, hana mkataba na Simba na kwa sasa tuna ofa kadhaa kutoka nje ya nchi, ukweli ndani tunayo ya Simba tu," alisema meneja wa mchezaji huyo Carlos Sylvester 'Mastermind.
Hili ni jambo la hatari kwa timu hiyo kwa kuwa kama Simba hawajamalizana na mchezaji huyo na wanamtaka kwenye klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao basi hata kiwango cha fedha lazima kitakuwa juu zaidi ya kila ambacho wangelipa endapo angekuwa na mkataba na klabu hiyo.
Dalili hizi zinaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa Simba ikatumia kitita kikubwa zaidi cha fedha sokoni kuliko kile ambacho ilitumia mwanzoni mwa msimu uliopita, lakini pia inaweza kuwapoteza wachezaji wengi zaidi ambao ilitaka kubaki nao.