Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MPAPASO WA MASAU BWIRE: Histori mpya kuandikwa kimataifa

Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele akijaribu kumtoka beki wa Al Hilal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa. Picha| Lovenes Bernard.

LEO, Jumapili tunatarajia historia nyingine kubwa kuandikwa na klabu za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya CAF, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Historia tunayoitarajia Watanzania, ni klabu zetu zote zinazoshiriki mashindano ya CAF kufuzu, kucheza hatua nyingine ya mashindano hayo.

Klabu nne, tatu kutoka Bara, ambazo ni Simba SC, Yanga SC na Azam FC na moja kutoka Zanzibar, Kipanga FC, zitakuwa katika viwanja tofauti kucheza mechi za mkondo wa pili zitakazoziwezesha kusonga mbele, hatua nyingine ya mashindano hayo, au kuondolewa mashindanoni.

Klabu za Simba SC na Yanga SC, zenyewe zinashiriki Ligi ya Mabingwa, wakati Azam FC na Kipanga FC zinashiriki Kombe la Shirikisho.

Klabu ya Simba SC itakuwa nyumbani, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 10.00 jioni ikiialika klabu ya Primeiro de Agosto kutoka nchini Angola.

Katika mchezo wa awali uliochezwa huko nchini Angola, klabu ya Simba SC ikiwa ugenini iliweza kuibuka na ushindi mnono wa magoli 1-3 dhidi ya mwenyeji Agosto.

Matumaini ni makubwa mno kwa klabu hiyo ya Msimbazi kuweza kupenya hatua hiyo ya mzunguko wa kwanza na kuingia hatua inayofuata ya makundi ya mashindano hayo.

Ili mgeni, klabu ya Agosto iweze kuiondosha Simba SC katika hatua hiyo na kufanikiwa kufuzu kucheza hatua ya makundi, italazimika kupata ushindi wa magoli 0-3, matokeo ambayo siyo rahisi kabisa kupatikana kwa Mkapa.

Simba SC ikiwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, historia yake ni kufanya vizuri, hasa katika mashindano ya kimataifa, kaulimbiu yake ya ‘kwa Mkapa hatoki mtu’ wamekuwa wakiitendea haki, hivyo Agosto katika mchezo huo, kupata ushindi wa magoli matatu itakuwa ni muujiza tu wa mwenyezi Mungu, mlima ni mrefu mno.

Mzee wa Mpapaso naamini, miujiza ipo, na lolote la kuumiza, lisilotarajiwa na wengi, linaweza kujitokeza, likashangaza na kuwaacha midomo wazi ambao hawakufikiria wala kutarajia muujiza kutendeka.

Kwa dharau, na Simba SC kudhani kwamba, watashinda tu, wameshinda ugenini ushindi wa kishindo, hivyo nyumbani ni kumsukuma tu mlevi, haihitajiki nguvu kubwa, ushindi upo tu, ni kujaribu kuruhusu muujiza kutendeka.

Kama Simba SC ilivyopata ushindi ugenini, ndivyo hivyo Agosto wataweza pia kupata ushindi wa kutosha kwa Mkapa endapo itatokea dharau yoyote kuelekea mchezo huo.

Ili kuonesha na kuithibitishia Afrika kwamba, Simba SC ni klabu kubwa, yenye mafanikio makubwa katika mashindano ya CAF, kama uwezo upo, basi, ikung’uteni vya kutosha, hata magoli saba au zaidi klabu hiyo Agosto iwe simulizi katika Ligi hiyo ya Mabingwa msimu huu.

Mashabiki wa klabu ya Simba SC, Watanzania wote Wazalendo, kesho tufurike katika uwanja wa Benjamin Mkapa, tukawashangilie Watanzania wenzetu, tuhakikishe kwa nguvu na umoja wetu, ushindi wa kutisha unapatikana.

Wana Jangwani, Wananchi, Yanga SC, wao wako ugenini, nchini Sudan, kukwaana na mwenyeji, Klabu ya Al Hilal.

Katika mchezo wa awali uliochezwa nchini, uwanja wa Benjamin Mkapa, klabu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya magoli 1-1.

Ili mwananchi, Yanga SC aweze kuingia hatua ya makundi, ushindi wowote unahitajika au sare ya kuanzia magoli 2.

Mzee wa Mpapaso hana shaka na uwezo wa Mwananchi, kikosi kizuri, bora na imara, benchi la ufundi lenye weledi, akili na maarifa mengi, naamini tutawapapasa, wananchi tutatoboa, tutacheza makundi.

Najua ni ugenini, kuna changamoto na ugumu wake, lakini kwa kujipana na kujiandaa kiuwezo, kitawezekana kisichowezekana.

Tusiende Sudan kinyonge, twende kibabe na kwa kujiamini, wachezaji wakajitume, tukawatungue nyumbani kwao, inawezekana.

Yanga SC ni moja ya klabu kongwe, zenye uzoefu wa mashindano ya CAF, uzoefu na mbinu nyingine halali katika mpira wa miguu, hasa katika mchezo wa kesho zinahitajika ili ushindi upatikane.

Furaha na raha yetu Wananchi na Watanzania wote wazalendo ni kushuhudia ushindi klabu yetu hiyo ya Jangwani, inawezekana, ni wachezaji tu kucheza kwa weledi, umakini na kujituma zaidi.

Azam FC, pamoja na ugumu uliopo kutokana na kichapo cha ugenini cha magoli 3-0, bado naamini wanawamudu klabu ya Al Akhdar kutoka Libya.

Katika uwanja wa Chamazi Complex, kesho kuanzia saa 1.00 jioni, tujitokeze twende uwanjani, tukawashangilie na kuwapa nguvu Azam FC waweze kupata ushindi utakaowezesha wasonge mbele, kwa neema ya Mungu inawezekana.

Kipanga FC wao pia wako ugenini, Tunisia kucheza na Club Africain, inahitaji ushindi wowote au sare yoyote ya magoli kwani katika mchezo wa awali uliochezwa uwanja wa Amaan, Zanzibar, klabu hizo zilisuluhu 0-0.

Kila la heri klabu za Simba SC, Yanga SC, Azam FC na Kipanga FC katika mchezo wenu huo, Mzee wa Mpapaso nawatakia ushindi wa kuwavusha kuwapeleka hatua inayofuata.