Msala mpya sakata la Kakolanya  

Muktasari:

  • Ipo hivi; Wakati Singida Fountain Gate wakidai kuwa mchezaji huyo katoroka kambini kutokana na kujichukulia uamuzi wa kuondoka bila ruhusa maalum, pia wameweka wazi kuwa wanafanya uchunguzi kwenye suala la upangaji wa matokeo.

Uongozi wa Singida Fountaine Gate, umeendelea kusisitiza kuwa nahodha wao Beno Kakolanya ni mtoro kambini, huku wakimuangushia jumba bovu jingine.

Ipo hivi; Wakati Singida Fountain Gate wakidai kuwa mchezaji huyo katoroka kambini kutokana na kujichukulia uamuzi wa kuondoka bila ruhusa maalum, pia wameweka wazi kuwa wanafanya uchunguzi kwenye suala la upangaji wa matokeo.

"Ni kweli tumetoa taarifa kwamba Beno Kakolanya katoroka kambini muda mchache kabla ya mechi, tafsiri ya mtu kutoroka katika eneo lake la kazi kwa mujibu wa taratibu kama unaondoka kazini kwako bila ruhusa huo ni utoro," amesema Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Masanza.

"Kakolanya tunafahamu aliomba ruhusa na aliyemuomba ruhusa ni meneja ambaye hana uwezo wa kumruhusu mchezaji. Jukumu lake ni kuwasiliana na viongozi wa juu ili waweze kutoa ruhusa,  lakini yeye akachukua uamuzi wa kuondoka."

Masanza amesema baada ya meneja kufikisha taarifa kwa uongozi wa juu ulikataa kutoa ruhusa hiyo kutokana na kuonekana kutokuwa ni taarifa yenye uzito kwani kulikuwa na mchezo uliokuwa mbele yao wakimtaka asubiri mechi iishe.

"Alichofanya ni utovu wa nidhamu, hivyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake, lakini pia kuna tuhuma zinafanyiwa kazi na kamati yetu ya nidhamu inafanyia kazi madai ya uhujumu katika mechi yetu dhidi ya Yanga, kamati ikikamilisha ripoti yake tutawafahamisha," amesema.

Mwanaspoti lilipomuuliza utaratibu wa mchezaji kuomba ruhusa kwa mastaa wao wawapo kambini, Masanza amesema unaanza kwa meneja wa timu ambaye ni lazima aushirikishe uongozi wa juu ili upitishe ruhusa.

"Mtendaji mkuu ndio mtu wa mwisho kupitisha ruhusa za wachezaji au mwajiriwa yeyote wa Singida Fountain Gate ilishawahi kutokea mchezaji akaomba ruhusa na ikapitishwa na meneja, baadaye ikaleta shida, hivyo hatutaki hilo lijirudie tena," amesema Masanza.

Sakata la mchezaji huyo limeghubikwa na taarifa tofauti ikiwamo ishu za kifamilia, ambapo inadaiwa aliomba ruhusa ili kwenda kutatua changamoto za kifamilia.

Vilevile kuna madai kwamba nyota huyo wa zamani wa Simba amekuwa akihusishwa na timu nyingine kwa ajili ya msimu ujao, suala ambalo halijathibitishwa na upande wowote kati ya pande hizo.

Wakati Singida Fountain Gate ikianzisha uchunguzi juu ya upangaji matokeo, lakini chanzo kimoja kimeiambia Mwanaspoti kuwa mchezaji huyo anashauriana na mwanasheria wake ili kuchukua hatua za kisheria akidai kuchafuliwa.

Hata hivyo, si Kakolanya wala uongozi wa klabu hiyo waliothibitisha ama kupokea malalamiko kutoka kwa mchezaji huyo au nyota huyo kuwasilisha madai hayo.
Mwanaspoti ilipomtafuta mchezaji huyo kuzungumzia sakata hilo alikataa kuongea chochote.

"Nitakucheki baadaye siwezi kuongea kitu kwa sasa," alijibu Kakolanya na kukata simu.

Kakolanya alitoroka kambini muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya wageni, Yanga na wenyeji wa mchezo huo, Singida Fountain Gate.

Katika mchezo huo wa ligi Singida Fountain Gate walikubali kichapo cha mabao 3-0 yakifungwa na Joseph Guede aliyeingia kambani mara mbili na moja likifungwa na Stephane Aziz Ki.