Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtagwa: Bado Mungu ananipigania

Mtagwa: Bado Mungu ananipigania

Muktasari:

  • Hana tena ile kasi ya miguu, hawezi kupiga japo hatua moja bila msaada wa kushikiliwa, hayo ndiyo maisha ya nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Jellah Mtagwa.

Hana tena ile kasi ya miguu, hawezi kupiga japo hatua moja bila msaada wa kushikiliwa, hayo ndiyo maisha ya nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Jellah Mtagwa.

Mkewe, Mboni Ramadhan anasema Jellah sasa amekuwa kama mtoto mdogo, hawezi kufanya chochote bila msaada, anahitaji matibabu, lishe na huduma nyingine ili apate faraja.

Miaka 17 iliyopita, nahodha huyo wa kwanza kuiongoza Stars kwenye fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) alipata maradhi ya presha, wakati akipambana na ugonjwa huo, akapata sukari na kisha kiharusi.

“Sijui hata chanzo cha maradhi haya! lakini Mwenyezi Mungu ameendelea kunilinda tangu 2004 nilipoanza kuugua hadi sasa, japo kuna wakati nakosa hata dawa, napitiliza mpaka wiki tatu au zaidi bila matibabu, lakini nipo naishi na maumivu yangu na Mwenyezi Mungu ananilinda,” anasema.

Nyumbani kwake Manzese, Dar es Salaam, familia imekuwa ikilazimisha furaha, wanaumizwa na maumivu ambayo baba yao anapitia, wanasema hawakuwahi kuishi muda mrefu na baba yao wakati akiwa na nguvu.

“Maisha yake yalikuwa Yanga, Pan na kwenye timu ya taifa, muda mwingi aliutumia huko alipokuwa na nguvu, nilimuelewa mume wangu kwa kuwa nilifahamu analitumikia taifa.

“Hata yeye aliona fahari katika hilo, hivi sasa hana nguvu tena, ni mgonjwa na hakuna anayeukumbuka mchango wake,” anasema Mboni ambaye ndiye anajukumu kubwa la kumhudumia nguli huyo wa zamani wa soka hivi sasa.


Changamoto tatu za Mtagwa

Ukiachana na maradhi yanayomsibu, Jellah anasema changamoto nyingine kwake ni kupata matibabu, usafiri na makazi.

“Mvua ikinyesha hapa kwetu ni tabu, maji yanaingia ndani, nilitamani kujenga kwenye kiwanja changu cha Mkuranga, japo chumba na sebule, lakini maradhi yamenirudisha nyuma.

“Huku hata Televisheni, unapomaliza kutizama sebuleni lazima uifiche uvunguni, vinginevyo wajanja watakusaidia kutunza,” anasema.

Nyumbani kwa Mtagwa, Manzese ni eneo ambako gari haifiki, ili uweze kufika barabarani, lazima kutembea si chini ya dakika 10 au kutumia usafiri wa pikipiki.

“Napata wakati mgumu hasa ninapotakiwa kwenda hospitali, siwezi kutembea, natamani kuwa na usafiri utakaonirahisishia, lakini sina uwezo huo.

“Siwezi kufanya chochote, nimekuwa mtu wa kusaidiwa kila kitu, binti yangu alinikatia bima ya afya ambayo ni mwaka sasa imekwisha, nakosa japo pesa ya kununua vidonge ili nipunguze maumivu, lakini nashukuru Mungu, bado anapenda niishi bado,” anasema.

Jellah ambaye licha ya kuugua kwa muda mrefu yuko vizuri katika kutunza kumbukumbu anasema nusu ya dozi ya dawa anazotumia zinauzwa Sh 69,000.

“Nina wiki ya tatu sasa (tangu wiki iliyopita) nimekosa pesa ya kununua dawa, naishi kwa nguvu za Mungu tu, hata lishe yangu ni duni pia,” anasema kwa uchungu.

Huku akilia, mkewe anasema familia inaumizwa na mapito anayopitia Jellah.

“Tumekuwa tukipambana kumsaidia, tunachoweza tunafanya kama familia na tunaposhindwa basi tunamwachia Mungu,” anasema.


Atamani kuonana na rais Samia

Jellah anasema ana jambo lake na siku atakayobahatika kuonana na rais Samia Suluhu Hassan atamueleza.

“Nilitamani sasa kuonana na Magufuli (John Pombe aliyekuwa rais wa Tanzania ambaye sasa ni marehemu), lakini sikupata nafasi hiyo siku alipoialika Stars Ikulu, sikuitwa.

“Japo nilitarajia kama nahodha wa kwanza kuiongoza Stars kwenye AFCON ningepata nafasi hiyo, lakini haikuwa hivyo.

Anasema anaamini kwa rais Samia, ipo siku atapata nafasi ya kuonana naye na atamueleza dukuduku lake.


Hajutii ustaa wake wa soka ila...

Katika mambo ambayo Jellah anasema uwa yanampa faraja ni yeye kuwa mwanasoka maarufu nchini, japo mpira haukumnufaisha.

Maisha yake ya sasa hayaendani na umaarufu aliokuwa nao kwenye soka, Jellah baba wa watoto wanne anasema anafarijika kuwa mwanasoka.

“Soka ndiyo nimenifanya niendelee kutambulika kwa jamii, nilistaafu kucheza soka la ushindani mwaka 1984, lakini hadi sasa bado mchango wangu unatambulika,”.

Asikitishwa na Yanga

Jellah ambaye aliitumikia Yanga kwa mafanikio anasema licha ya timu hiyo kuwahi kuweka kambi mara kwa mara kwenye hoteli ya Nefaland, Manzese iliyo jirani kabisa na anakoishi, lakini haijawahi kukosea njia na kwenda kumjulia hali.

“Watu walikuwa wananiambia ‘wenzako’ Yanga wako hapo (Nefaland), nenda kawatembelee, ila ndiyo hivyo, naanzaje kwenda wakati wao hawanikumbuki?,”.


Alitamani kumkabidhi kijiti Samatta

Jellah anakumbuka namna chama cha wachezaji wa zamani walivyomfuata kwenda kuishuhudia mechi ya Taifa Stars na Uganda ya kufuzu kucheza Afcon msimu uliokwisha.

“Waliniletea gari nikamwambia kijana wangu anisaidie kunikokota hadi barabarani nikaenda uwanjani, tuliambiwa tutaonana na Waziri Mkuu baada ya mechi lakini tulishindwa.

“Niliishuhudia Stars ikifuzu, nilitamani kuongea na Mbwana Samatta kama nahodha ambaye alichukua kijiti changu kuiongoza Stars kwenye Afcon.

“Mimi niliiongoza 1980, yeye ameiongoza 2020, hakuna nahodha mwingine aliyeweka rekodi hiyo, lakini sikupata nafasi hiyo,”anasema.

Goti ndilo lilimuondoa kwenye soka

Jellah aliyewahi kuwa nahodha wa Stars kwa miaka 10 mfululizo anasema kama si maumivu ya goti kumuondoa kwenye soka la ushindani, angecheza muda mrefu zaidi.

“Nilistaafu mwaka 1984, lakini nilikuwa bado na kiwango kizuri tu, sema maumivu ya goti ndiyo chanzo cha mimi kujiweka kando na soka,” anasema beki huyo na nahodha wa Stars tangu 1974.