MTU WA MPIRA: Kuna Pascal Wawa mmoja tu

Monday June 27 2022
wawapiic

Hakuna marefu yasiyo na ncha. Hakuna mafupi yasiyo na mvuto. Hivi ndivyo maisha ya beki raia wa Ivory Coast, Serge Pascal Wawa yamefikia tamati pale Simba.

Alhamisi usiku, Simba ilitumia mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kumuaga Wawa baada ya kuhudumu klabuni hapo kwa miaka minne.

Imekuwa ni miaka minne ya mafanikio makubwa kwa Wawa. Ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam na mengine kadhaa ikiwemo Ngao ya Hisani na Kombe la Mapinduzi.

Pia Wawa amekuwa sehemu ya kikosi cha Simba ambacho kilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili, pamoja na kombe la shirikisho mara moja.

Katika miaka hii minne, Wawa amekuwa chaguo la kwanza pale Simba, ukiachana na msimu huu ambao Henoc Inonga amechukua nafasi yake.

Wakati Simba inamrejesha Wawa nchini mwaka 2018, watu wengi walibeza wakidai kuwa ni mzee. Nini kimetokea? Wawa amekuwa katika kiwango bora kwa miaka minne. Kila kocha anayepewa kazi Simba amekuwa akichagua kufanya kazi na Wawa.

Advertisement

Unadhani ni bahati mbaya? Hapana. Kwanza, Wawa ni beki wa kisasa. Anaweza kusoma mikimbio ya washambuliaji. Ana hesabu sahihi za kukaba. Pia ni ngumu kumpiga chenga na kupita.

Halafu baada ya hapo akipokonya mpira ana utulivu katika kuanzisha mashambulizi. Pia ndiye funguo ya mashambulizi ya Simba kutokea chini. Ana jicho la mbali na pasi zilizonyooka. Huyo ndio Wawa.

Mbali na hayo ana nidhamu kubwa kazini. Anawahi mazoezini kila siku. Anaonyesha bidii katika mazoezi ya kila siku. Kwa kifupi, Wawa hajawahi kuwa mvivu wa mazoezi hata siku moja.

Wakati akiwa Azam FC, Wawa alionyesha utofauti mkubwa sana. Alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Azam FC kilichotwaa taji la Kagame mwaka 2015 bila kuruhusu goli hata moja.

Ni wakati huo Wawa alipendwa na mashabiki wote wa soka nchini. Alipendwa ma Simba na Yanga. Kila timu ilitamani kuwa na beki aina ya Wawa. Wakamuita Waziri wa Ulinzi.

Bahati mbaya Azam FC ikaleta makocha fulani wa mchongo kutoka pale Hispania, wakapendekeza kuachana na Wawa. Wakati huo alikuwa ametoka majeruhi, wakasema ameisha.

Uzuri ni soka halidanganyi. Timu yake ya zamani, El Merrikh ikarejea tena kumsajili. Bado waliona kitu ndani yake. Akarejea Sudan na kuwasha moto.

Miaka sita baada ya kuondoka Azam FC bado Wawa amekuwa wa moto. Pengine tutamwona katika kiwango bora pia kama ataendelea kucheza Ligi Kuu Bara.

Kuna mengi mabeki wetu wanapaswa kujifunza kwa Wawa. Kwanza ni nidhamu ya mchezo. Nidhamu ya mazoezi na binafsi pia.

Pia ni utulivu. Beki huhitaji kucheza kama unapigana vita pale Vietnam ama Iraq. Mpira wa kisasa unahitaji zaidi utulivu. Nadhani unamuona beki kama Dickson Job wa Yanga. Ni aina ya Wawa hivi. Anacheza soka la kisasa.

Mabeki aina ya Joash Onyango, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ watapata ugumu kwenye soka la kisasa. Beki wa kisasa anapaswa kuwa na mfanano wa Wawa. Anacheza soka la burudani. Hakupi upenyo wala nafasi lakini anafurahia zaidi kucheza soka.

Yote kwa yote tukiri kuwa Wawa ni miongoni mwa mabeki bora zaidi wa kati kuwahi kucheza nchini. Azam FC ilimuona, ikamtumia. Lakini Simba ikamrejesha nchini kuja kutuaga.

Baada ya miaka minne, hakuna mtu wa Simba anajuta kuwa na Wawa. Amethibitisha thamani yake. Anaondoka kwa heshima kubwa.

Tunavyojidanganya kuhusu Fei Toto wetu

Nimemsikia Msemaji wa Yanga, Haji Manara akizungumza kuhusu uwezekano wa kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuuzwa na klabu hiyo.

Manara anasema angalau klabu inayomtaka Feisal itoe kuanzia Dola 500,000 ndipo wataweza kuzungumza. Inachekesha sana.

Manara anadai kuwa Fei Toto siyo mchezaji wa kuuzwa kwa Dola 200,000. Inafikirisha kidogo.

Ni kweli, Fei Toto ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Ana utulivu mkubwa akiwa na mpira. Ana uwezo mkubwa pia wa kukaba.

Hata hivyo msimu huu pamoja na kucheza nyuma ya straika, bado namba zake haziridhishi. Ana mabao sita na asisti nne tu.

Hizi namba hazitoshi. Kuna wakati msimu huu Feisal alikaa miezi mitatu bila kufunga goli wala asisti. Huyu ndiye kiungo anayeuzwa Bilioni moja?

Huyo Clatous Chama hajawahi kuwa na namba duni kama hizi za Feisal. Chama kwa misimu miwili alitoa pasi za mabao 10 ama zaidi. Katika msimu wake wa mwisho kabla ya kuuzwa kwenda RS Berkane alitoa pasi 15 za mabao.

Hapo achilia mbali mashambulizi aliyoanzisha ambayo yalizaa mabao. Halafu naye akafunga mabao saba. Akawa amehusika kwenye mabao zaidi ya 22 kwa msimu mmoja.

Akafanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika. Kuna nyakati Chama aliibeba Simba mgongoni mwake. Lakini bei yake haikufika Dola 500,000. Vipi kuhusu Fei Toto?

Ni Luis Miquissone pekee ambaye ameuzwa zaidi ya fedha hizo kutokea Ligi ya Tanzania. Na kila mtu anakiri Miquissone ni mchezaji wa daraja la peke yake. Hafananishwi na mchezaji yeyote kutoka Ligi yetu.

Ila kwa Fei Toto bei tunayotaja ni uongo mtupu. Hana thamani hiyo.

Advertisement