Mukoko: Tunakamiwa sana

Sunday March 07 2021
mukoko pic
By Khatimu Naheka

YANGA imeangusha pointi tatu za kwanza nzima katika Ligi Kuu Bara wakikubali kipigo cha mabao 2-1, lakini kiungo wao, Mukoko Tonombe akawapa meseji nzito mabosi endapo wanautaka ubingwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mukoko kwanza akawageukia wachezaji wenzake akisema watu wa kwanza wanatakiwa kujilaumu ni wao kama wachezaji kwa kushindwa kucheza kwa umakini hasa katika mechi za hivi karibuni.

“Watu wa kwanza wa kulaumiwa ni sisi kama wachezaji, mechi hizi chache tumeshindwa kucheza vyema kama ilivyokuwa huko nyuma, tumekuwa na makosa mengi katika kulinda na hata kufunga,” alisema kiungo huyo ambaye ni raia wa DR Congo.

“Kama tunautaka ubingwa basi kazi ya kwanza ya kubadilika ni sisi kama wachezaji, tulikutana na kuzungumza lakini bado tumefanya yaleyale, hatukuwa katika ubora wetu katika dakika 90 zingine.”

Mukoko alienda mbali zaidi akisema ni wakati wa viongozi wao kutafuta kinachoiangusha zaidi timu yao kwa mechi zao kuwa ngumu.

Alisema amekuwa akiangalia mechi zingine za ligi na kugundua kwamba kila mchezo wao unakuwa ni kama fainali huku wapinzani wao wengine wakiwa na mechi rahisi. “Sijajua kipi kina shida hapa, mechi zetu zimekuwa ngumu sana huwa naangalia mechi zingine naona wanacheza na kushinda kirahisi sana, hili viongozi wetu wanaweza kulifanyia kazi na kuangalia kwanini sisi tunakamiwa sana.

Advertisement

“Hapa Yanga hata ukishinda mechi lazima umetumia nguvu nyingi ni kama kila mechi kwetu tunacheza fainali,” aliongeza


ILE PENATI

Mukoko alifichua kwamba wakati Mkongomani mwenzake Tuisila Kisinda akichukua mpira na kwenda kupiga penalti alijikuta anatetemeka kabla hata hajapiga mpira.

“Namwamini Kisinda katika penalti, lakini sijajua kwanini ila aliposhika mpira tu nikajikuta natetemeka kabla hata hajaipiga,” alisema mchezaji huyo.

“Haikuwa kawaida yangu lakini nafikiri hakutakiwa kupiga, sikushtuka alivyokosa niliumia tu moyoni.”

Advertisement