Mvua yazitibulia Yanga, JKT mechi yaahirishwa

Muktasari:

  • Ipo hivi; Leo ilipangwa JKT Tanzania icheze dhidi ya Yanga katika muendelezo wa Ligi Kuu Bara, lakini mchezo huo umeahirishwa kutokana na uwanja kujaa maji, hivyo utapangiwa siku nyingine.

YANGA SC ilikuwa na hesabu zake leo iende Jenerali Isamuhyo kucheza na wenyeji wao JKT Tanzania ili kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya kutetea ubingwa wao, lakini mvua kubwa iliyonyesha Dar es Salaam, imewatibulia.

Ipo hivi; Leo ilipangwa JKT Tanzania icheze dhidi ya Yanga katika muendelezo wa Ligi Kuu Bara, lakini mchezo huo umeahirishwa kutokana na uwanja kujaa maji, hivyo utapangiwa siku nyingine.

Kamishna wa mchezo huo, Kamwanga Tambwe, amesema: "Maamuzi ambayo yamefikiwa baada ya kujiridhisha kabisa kwa mimi kamisaa na waamuzi ambao tulikagua kiwanja chetu kwa ajili ya mchezo wetu wa leo jioni mchezo namba 135 ambao ulikuwa uwakutanishe JKT Tanzania ambao walikuwa wenyeji na Young Africans waliokuwa wageni, tumejiridhisha na uwanja bado umejaa maji na mchezo hauwezi kuchezwa kwa mujibu wa sheria za soka na kanuni zetu za ligi.

"Hivyo maamuzi ambayo yamefikiwa mchezo huu umeahirishwa na taarifa rasmi itatoka baadaye ni lini mchezo huu utachezwa aidha ni hapahapa au utahamishwa kwenye uwanja mwingine.

"Kwa hiyo bado tunakwenda kufanya mawasiliano na viongozi wetu wa juu ili kufikia maamuzi sahihi ya mwisho ambayo ndiyo yatakuwa maelekezo ya kurudiwa mchezo huu baada ya kuahirishwa kwa siku ya leo kutokana na uwanja kujaa maji.

"Kikanuni mchezo huu kama ambavyo umeahirishwa utatambulika na umeahirishwa kabla haujachezwa hata sekunde moja. Kutokana na hilo, aidha unaweza kuchezwa kesho au kupangiwa siku nyingine. Lakini kikanuni kama ungekuwa umechezwa hata kwa dakika moja au sekunde 30, maana yake mchezo huu ulipaswa urudiwe siku ya kesho saa 4 asubuhi.

"Ndiyo maana nimesema kutokana na hali hiyo, basi sisi tunaendelea kupeleka taarifa zetu kwenye vyombo husika na watatoa maamuzi ya huu mchezo ni kwa namna gani utatakiwa kurudiwa kuchezwa baada ya kuahirishwa."

Kabla ya kuahirishwa kwa mchezo huo, timu zote mbili zilifika uwanjani na wachezaji kuanza kufanya mazoezi mepesi kujiweka tayari kwa mapambano.

Kabla ya mchezo wa leo, hesabu za Yanga ambayo imebakiwa na michezo nane kukamilisha msimu huu, inatakiwa kushinda sita ili kufikisha pointi 76 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, hivyo itatangaza ubingwa.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikikusanya pointi 58 baada ya kucheza mechi 22, wakati JKT Tanzania ikiwa nafasi ya 15 katika hatari ya kushuka daraja baada ya kucheza mechi 22 na kuambulia pointi 22.