Mwakinyo sasa ni ubingwa wa dunia

Monday November 16 2020
mwakinyo pic

Mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini Ijumaa Novemba 13,2020 walishuhudia mapinduzi makubwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa kwa kufanyika pambano la kwanza la limataifa kwenye ukumbi wa kisasa wa Next Door Arena, Oysterbay.

Katika pambano hilo lililoandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports , bondia Hassan Mwakinyo alitetea vyema ubingwa wake mabara wa uzito wa Super Welter wa WBF baada ya kumchapa kwa TKO mpinzani wake Jose Carlos Paz wa Argentina katika raundi ya nne.

Ni mapinduzi kutokana na ukweli kuwa mapambano ya ngumi za kulipwa nchini kwa miaka mingi huwa yanafanyikia kwenye kumbi za ‘kawaida sana’ tofauti na wenye hadhi ya kimataifa kama wa Next Door Arena.

Ni mapinduzi vile vile kutokana na waandaaji kufanikiwa kuongeza wigo wa wadau wa mchezo wa ngumi za kulipwa nchini tokea kwenye asili yake kama vile Keko, Manzese (Friends Corner), Mabibo, Kinondoni Mkwajuni, Mwananyamala na eneo la Kwa Msisiri.

Miaka ya nyuma, mapambano makubwa ya ngumi za kulipwa yalikuwa yanafanyikia kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee , lakini kwa siku za hivi karibuni, uwanja wa Uhuru, PTA na mara moja tu kwenye Mlimani City.

Kumbi za zamani kama Kolini (Tandale), Friends Corner Hotel, Vijana Social, DDC Mlimani, King Palace (Keko), Texas (Manzese), Relwe Gerezani na nyinginezo zilikuwa maarufu sana kwa mapambano ya ngumi za kulipwa.

Advertisement

Pambano hilo lililojulikana kwa jina la “Jackson Group Fight Night” pia limeweka historia kwa upande wa kiingilio na kuzidi hata kile cha mpira wa miguu kwa mbali sana.

Katika pambano hilo, kiingilio cha kawaida kilikuwa Sh150,000 na watu 10 wa kukaa eneo maalum (VIP) walilipa jumlaya Sh milioni 3 na kupata huduma mbali mbali za eneo la VIP. Viingilio viliwalenda watu wenye vipato vya juu tofauti na hali ya zamani.

Watu waliokaa VIP ( kwa sh milioni 3 kwa meza ya watu 10), walipata huduma mbalimbali kuanzia vinywaji, chakula na choo.

Mashabiki walikaa kwenye sofa za kisasa na huduma ya choo. Pia kulikuwa na ulinzi mkali eneo hilo huku wakiwa na wahudumu maalum na kubadili taswira ya mchezo huo kuwa mashabiki wake ni wa maeneo yaliyozoeleka.

Tofauti na matarajio ya wengi, pamoja na kuwa na kiingilio kikubwa, ukumbi ulijaa mashabiki na kudhihirisha kuwa mchezo wa ngumi za kulipwa unapendwa sana hapa nchini.

Advertisement