Mwandishi wa habari za michezo auawa kwa kuchomwa moto
Mwandishi maarufu wa habari za soka Italia, Luigi “Luca” Esposito.
Muktasari:
- Alikuwa mwandishi wa safu za maoni katika gazeti la La Città di Salerno na mchambuzi wa mara kwa mara katika kituo cha televisheni cha OttoChannel TV, akiripoti habari za klabu za Serie B, zikiwemo Avellino na Juve Stabia.
Mwandishi maarufu wa habari za soka Italia, Luigi “Luca” Esposito, ameuawa kikatili kwa kupigwa risasi kisha mwili wake kuchomwa moto katika mauaji yanayoonekana kutekelezwa kwa umakini mkubwa.
Watu wake wa karibu walianza kuwa na wasiwasi baada ya kushindwa kuwasiliana na Esposito mwenye umri wa miaka 53, Jumamosi jioni.
Moto ulizuka katika eneo la shamba lililojitenga mjini Salerno, Italia, ambapo vikosi vya zimamoto vilifika haraka na baadaye kugundua mabaki ya mwili wa Esposito alfajiri ya Jumapili.
Kifo chake kinachunguzwa kama ni mauaji, huku uchunguzi ukisimamiwa na mwendesha mashtaka mkuu wa kupambana na makundi ya kimafia wa Salerno, Rafaele Cantone.
Wapelelezi walipata maganda ya risasi karibu na mwili wa Esposito katika eneo la Bivio Cioffi, Salerno, na waliweza kuthibitisha utambulisho wake baada ya gari lake kupatikana karibu na eneo hilo.
Uchunguzi wa maiti umepangwa kufanyika ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake.
Wapelelezi pia wanachunguza maisha binafsi ya Esposito ili kubaini sababu zinazoweza kuwa nyuma ya mauaji hayo, zikiwemo migogoro ya kifedha au ya kimapenzi.
Hadi sasa, mamlaka hazijaondoa uwezekano wa mwelekeo wowote wa uchunguzi.
Marehemu, ambaye alikuwa anatokea Nocera Inferiore huku akiwa shabiki mkubwa wa klabu ya Salernitana 1919, alikuwa akiendesha tovuti ya TuttoSalernitana.com.
Mbali na hilo, alikuwa mwandishi wa safu za maoni katika gazeti la La Città di Salerno na mchambuzi wa mara kwa mara katika kituo cha televisheni cha OttoChannel TV, akiripoti habari za klabu za Serie B, zikiwemo Avellino na Juve Stabia.