Nabi atua Sauzi na mkwara, mastaa waitaka fainali

WAKATI Yanga ikitua salama nchini Afrika Kusini tayari kwa maandalizi ya mchezo wa marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants, kocha Nasreddine Nabi amechimba mkwara akisema wenyeji hawataamini, huku akiwataka mastaa wake wakacheze kijeshi.

Yanga iliondoka usiku wa kuamkia jana mara baada ya pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji iliyowafunga mabao 4-2 na kutangaza ubingwa kabla msimu haujaisha na keshokutwa itashuka uwanjani nchini humo kuvaana na Marumo ikiwa na hazina ya mabao 2-0 ya mechi ya awali jijini Dar.

Kocha Nabi aliliambia Mwanaspoti saa chache kabla ya timu hiyo kupaa kuwa, bado hawajafuzu  fainali za CAF, licha ya ushindi wa nyumbani, hivyo dakika 90 za ugenini ndizo zitaamua hatma yao.

Nabi alisema anajua wenyeji watashuka uwanjani kivingine, lakini wenyeji hawataamini watakachokutana nacho kutokana na ukweli ameshazungumza na wachezaji na kuwataka kucheza kwa kujitolea muda wote kama ambavyo anavyocheza kwa jihadi beki wao wa kati Ibrahim Bacca.

"Tunakwenda kwenye mchezo utakaoamua hatma yetu kama tutamalizia mguu wa pili kwenda fainali au vinginevyo, mimi ukiniuliza nitarudia kukwambia hii ni mechi ngumu kwetu kuliko ile ya kwanza," alisema Nabi na kuongeza;

"Nitaendelea kuwakumbusha wachezaji wangu kwamba tunatakiwa kwenda kuipigania heshima ya klabu yetu kwa kucheza kama wanajeshi tunatakiwa kwenda kuipigania Yanga, tunatakiwa kwenda kuipigania Tanzania."

Nabi aliyeipa Yanga taji la pili mfululizo la Ligi Kuu, alisisitiza kwa kusema; "Natamani kuona kila mchezaji akicheza kwa jihadi na kujitolea nguvu zake zote kama anavyocheza beki wetu Bacca, napenda sana kumuona anavyojituma uwanjani, tunatakiwa kukaba kwa nguvu na kushambulia kwa nguvu lakini kikubwa tukipata nafasi tuzitumie.

"Wapinzani wetu watakuja na nguvu kubwa kutokana na matokeo ya mchezo uliopita nasi tunatakiwa kuwa na nguvu ya kutoruhusu watufunge kuwathibitishia kwamba hatukubahatisha.

Kocha huyo aliweka wazi hesabu zake ni kutokwenda kupaki basi na kwamba watahakikisha wanakwenda kutafuta pia bao au mabao zaidi ili kuwapandisha mlima mrefu zaidi Marumo.

"Mimi sio muumini wa soka la kupaki basi, lakini nahusudu timu yenye nidhamu ya kujua mbinu bora za kuzuia lakini pia kushambulia tutakapopata nafasi, tunatakiwa kujiongezea umakini wa kumalizia nafasi tutakazotengeneza hili pia lilitupa wakati mgumu kwenye mchezo uliopita."


MASTAA NA FAINALI

Nyota wa timu hiyo walisema baafa ya kumaliza mambo ya Ligi Kuu kwa sasa akili yao ni kubeba taji la CAF licha ya kutambua mechi ya Jumatano ugenini itakuwa ngumu.

Mshambuliaji Mzambia Kennedy Musonda aliyefunga bao la kwanza katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Dodoma, alisema tayari wameshasahau vaibu la ubingwa huo wa 29.

Musonda alisema kila mchezaji wa timu yao akili yake Sasa Iko sawasawa tayari kwa mchezo huo wa mkondo wa pili ili waendelee kuweka hai malengo yao ya kutinga Fainali.

"Tumechukua ubingwa Ile furaha yote mliyoiona uwanjani jana (juzi) imeishia pale tumeondoka na morali pekee ambayo tutaitumia katika kujituma kwenye mechi ijayo,"alisema Musonda.

"Tunakwenda kucheza mechi ngumu ugenini tutacheza kama hatukushinda mechi ya kwanza, tunahitaji sana kucheza fainali ya mashindano haya makubwa Afrika hiyo ni kiu yetu kubwa."

Kinara wa mabao wa Yanga, Fiston Mayele alisema wamepania kufanya vizuri katika mchezo huo wa marudiano.

"Tunatambua tuna kazi ngumu katika mechi ya marudiano kwani wapinzani wetu ni wazuri na pia watakuwa kwao. Tumeshatwaa ubingwa wa ligi hapa sasa ni zamu ya kutafuta ubingwa wa Afrika. Muhimu ni kupambana mchezo wa marudiano tuweze kufika fainali na tukivuka hapo naamini hata kombe tutabeba kwani nakiamini kikosi chetu, " alisema Mayele, huku Aziz Stephan Ki alisema kama wachezaji wamejiandaa kuandika historia nyingine kwa kushinda kisha kutinga fainali.

"Tuna hamu ya kucheza fainali ya Afrika, kila mchezaji ana morali na matamanio hayo hivyo hilo litachangia kila mmoja kujituma kuhakikisha tunatinga fainali na kuandika historia mpya. Mungu ni mwema naamini atatusaidia kulitimiza hilo " alisema Aziz Ki

Kiungo na beki , Yannick Bangala alisema kama wachezaji wote watakuwa makini na kuelekeza akili zao kwenye mchezo huo basi watashinda na hata ubingwa wa Afrika watabeba.


MASHABIKI ZAIDI YA 100

Yanga haina upweke Sauzi kwani makundi ya mashabiki wao walianza safari tangu jana alfajiri kwa njia mbili tofauti kuifuata timu yao ugenini.

Mashabiki wasiopungua 55 wao waliondoka jana kwa njia ya barabara walitarajiwa kusafiri kwa siku tatu mpaka kuingia nchini Afrika Kusini huku wengine kwa makundi tofauti wakiondoka kwa njia ya anga.

Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji alisema mashabiki hao wataungana na Watanzania waliopo nchini Afrika Kusini ambao nao wanaisubiri timu yao.