Nabi kupiga chini watano Yanga, majembe mapya yaandaliwa

Wednesday June 09 2021
YANGAAAPICC
By Mwandishi Wetu

YANGA inataka kufanya usajili wa kimapinduzi ambao utawapa jeuri ya kwenda kupindua ukame wa kukosa mataji ya ndani mawili ambayo wamepishana nao kwa takribani miaka minne.

Malengo hayo yamewafanya mabosi wa timu hiyo kupiga hesabu ndefu ambapo katika ripoti ya kiufundi inayokabidhiwa leo huenda ikaondoka na mastaa watano.

Ripoti hiyo haitawagusa wageni pekee lakini panga lingine litapita kwa wazawa baadaye.

Michael Sarpong

Staa wa kwanza ambaye atakuwa katika mstari wa kuachwa ni mshambuliaji, Michael Sarpong ambaye msimu huu amefunga mabao manne pekee.

Ukame huo umekuwa kinyume na matarajio ya mabosi wa Yanga wanaona ni wakati muafaka pande hizo mbili kuachana ingawa mwenyewe Sarpong tayari alishawaambia anafikiria kuwasiliana na meneja wake kusitisha mkataba wake.

Advertisement

Fiston Abdulrazack

Mwingine ni mshambuliaji, Fiston Abdulrazack ambaye ameshindwa kufanya kile ambacho wakubwa wa klabu hiyo walikitarajia lakini kwavile mkataba wake ni mfupi wa miezi sita umeirahisishia Yanga kuchukua uamuzi huo.

Haruna Niyonzima

Kiungo mkongwe Haruna Niyonzima hatavaa jezi ya timu hiyo kwa msimu ujao kutokana na kushindwa kupenya katika kikosi cha kwanza lakini takwimu pia zikimchinja akifunga bao 1 pekee lakini pia akitoa pasi mbili za mabao pekee.

Yanga inataka kutafuta kiungo fundi mwenye kiwango bora zaidi kazi ambayo mabosi wa Yanga wameshaianza kwa muda mrefu huku hatua ya Niyonzima kumaliza mkataba wake mwisho wa msimu ukiirahisishia zaidi Yanga.

YANGAPIC

Carlinhos tayari

Staa mwingine ambaye ni kama aliwahi kubutua na kusepa zake ni Carlos Carmo ‘Carlinhos’ ambaye mabosi wa Yanga hawana shida na kiwango chake lakini shida ilikuwa maisha yake nje ya uwanja. Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba wameachana kwa makubaliano ya kimaandishi ambayo Yanga watafaidi akiuzwa popote.

Lamine Moro/Shikhalo

Beki na nahodha mkuu Lamine Moro au Kipa Farouk Shikhalo mmoja kati yao anaweza pia kuondoka au wote wakabaki kutokana na kugawanyika kwa hoja ndani ya uongozi.

Yanga inaona Lamine anazidi kupungua ubora akiwa na makosa mengi lakini hatua mbaya ameingia kwenye ishu za utovu wa nidhamu. Habari zinasema kwamba mabosi wengi hawakubaliani na maisha yake ndani ya klabu huku kinachowaumiza kichwa kikiwa ni mkataba wa mwaka mmoja uliosalia.

Kipa Shikhalo naye bado kuna shida lakini mabadiliko yake katika mchezo wa mwisho dhidi ya Mwadui na ule wa kirafiki uliopigwa juzi pale kambini kwao Avic dhidi ya African Lyon na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 mabosi wanaona kama apewe muda kidogo.

Ujio wa kocha wa makipa, Razak Siwa ambaye sio tu Shikhalo amewaongezea kitu hata, Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili unaonekana kuwabadili makipa hao na Yanga wanaona aendelee. Yanga wamekubaliana kukamilisha usajili mpya ndani ya muda mfupi ili kupata muda mrefu wa kuandaa timu mpya ingawa wanafanya siri kubwa mpaka msimu utakapomalizika wikichache zijazo.

Advertisement