Nabi mpango umetiki, aikwepa Bamako
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi.
Muktasari:
- Yanga imepaa kwa Ndege ya Shirika la Ethiopia ikiifuata Bamako kupitia nchini Ethiopia na kutua Mali jana mchana tayari kwa mchezo huo, huku ikiondoka na msafara wenye wachezaji 24 tayari kwa mchezo huo wa tatu wa Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Dar es Salaam. Klabu ya Yanga baada ya kumaliza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, usiku wa Jumatano, Februari 22, 2023 ilianza safari yake kuiguata Real Bamako ya Mali katika mchezo wake wa tatu katika Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kocha wa timu hiyo ametuma salamu nzito kwa wapinzani wao, akisema kazi inaendelea baada ya mipango kutiki.
Yanga imetua Mali jana mchana tayari kwa mchezo huo, huku ikiondoka na msafara wenye wachezaji 24 tayari kwa mchezo huo wa tatu wa Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika unaotarajiwa kuchezwa Jumapili Februari 26 mwaka huu.
Wakati Yanga ikipaa, kocha wake, Nasreddine Nabi ameliambia Mwananchi, hawataki kurudia makosa kama yaliyofanyika Tunisia walipoenda kucheza na US Monastir na kuchapwa mabao 2-0, kwa vile wanataka kuzipata pointi tatu za kwanza ugenini.
Yanga ilipata ushindi nyumbani katika mechi iliyopita ya CAF kwa kuichapa TP Mazembe ya DR Congo ukiwa ushindi wao wa kwanza, huku ikicheza pia soka kubwa na Nabi alisema wameifuata Bamako ikiwa na mifumo mitatu ambayo wataamua ni upi wautumie huku akiringia kiwango walichoonyesha katika mchezo uliopita.
Kocha huyo alisema dili lake la kutumia mfumo wa 4-3-3 ameridhishwa na jinsi safu yake ya kiungo na ile ya ushambuliaji ilivyopigana katika mchezo huo na kwamba kazi itaendelea hata kwenye mechi ya Jumapili hii ugenini mjini Bamako.
“Kitu bora tumetanua matumizi ya mifumo yetu na tunaweza kubadilika kulingana na mpinzani ambaye tutacheza naye kwa ubora wake, hii ni faida yetu kubwa,” alisema Nabi na kuongeza;
“Nimewaambia wachezaji, kuwa kitu ambacho kitatupa thamani kubwa ni kwenda kuendeleza ushindi wetu, ingawa nafahamu haitakuwa rahisi, tunapaswa kujitoa kwa kucheza kwa umakini mkubwa.”
Nabi aliongeza, ingawa bado anatamani kuona mambo makubwa zaidi lakini anafurahia muunganiko unaendelea kujitengeneza kwa washambuliaji wake wawili Fiston Mayele na Kennedy Musonda ambao kama kasi yao itazidi Yanga itashinda zaidi.
“Fiston na Musonda walicheza vizuri, tulikuwa tunataka nguvu ya namna hii, unaweza kuona Fiston hakufunga lakini kwangu mimi alifanya kazi kubwa kuutengeneza ushindi kwa kasi yake na pasi zake, hili likiongezeka zaidi tutakuwa na ubora wa kushinda zaidi.”
Kikosi cha Yanga kilichoondoka kimewajumuisha makipa Metacha Mnata, Eric Johola na Djigui Diarra, mabeki wakiwa ni; Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mamadou Doumbia, Kibwana Shomari, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, David Bryson na Yannick Bangala
Wamo viungo Dickson Ambundo, Farid Mussa, Zawadi Mauya, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Tuisila Kisinda, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, huku washambuliaji wakiwa Mayele, Musonda, Stephane Aziz KI, Clement Mzize.