Namungo yapenya kibabe Shirikisho

Tuesday January 05 2021
namungo pic
By Oliver Albert

Namungo FC imefuzu hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-3 dhidi ya Hilal El Obeid ya Sudan.
Hiyo ni kutokana na sare ya mabao 3-3 waliyoipata Namungo kwenye  mchezo wa marudiano uliofanyika nchini Sudan.

Katika mchezo wa kwanza  uliofanyika Desemba 23 mwaka jana jijini Dar es Salaam ,Namungo ilishinda mabao 2-0 .
Kutokana na matokeo hayo sasa Namungo itasubiri kujua itacheza na nani hatua nayofuata baada ya kufanyika kwa droo ya upangaji wa ratiba itakayofanyika Januari 17.

Washindi waliotinga hatua ya mtoano watacheza na timu zilizotolewa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mapema Februari.
Katika mchezo huo mabao ya Namungo yalifungwa na  Steven Sey dakika ya pili akiweka rekodi ya kuifunga Hilal El Obeid katika mechi zote mbili huku mabao mengine yakifungwa na Bigirimana Blaise dakika ya 39 na Edward Manyama dakika ya 50.

Sey anaweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga katika mechi zote za mashindano hayo ambazo Namungo imecheza mpaka sasa msimu huu kwani katika mchezo wa hatua ya awali dhidi ya Al Rabita ya Sudani Kusini, mchezaji huyo alifunga mabao mawili na kuiongoza timu yake kushinda mabao 3-0 huku mchezo wa marudiano ukishindwa kufanyika baada ya Shirikisho la soka Afrika (Caf) kuufuta kutokana na Chama cha  Soka Sudani Kusini kushindwa kumamilisha taratibu kuhuus waamuzi waliopangwa kuchezesha mechi hiyo.
Katika mchezo wa awali uliofanyika Desemba 23 mwaka jana, Sey alifunga bao la pili baada ya bao la kwanza kufungwa na Sixstus Sabilo na mchezo huo kumalizika kwa Namungo kushinda mabao 2-0.

Advertisement