Nguvu ya Haji Manara Yanga

Nguvu ya Haji Manara Yanga

Muktasari:

  • Jana jioni, Yanga imemtambulisha Haji Manara, hiyo imekuwa ni 'sapraizi', si tu kwa mashabiki wengi wa Simba, ambako Manara amewahi kuwa Ofisa Habari, lakini pia hata kwa mashabiki wa Jangwani.

Dar es Salaam. Jana jioni, Yanga imemtambulisha Haji Manara, hiyo imekuwa ni 'sapraizi', si tu kwa mashabiki wengi wa Simba, ambako Manara amewahi kuwa Ofisa Habari, lakini pia hata kwa mashabiki wa Jangwani.

Manara, ambaye aliondoka Simba akiwa na mgogoro na baadhi ya viongozi wa juu wa klabu hiyo, ameingia Yanga na kauli ya kishindo kwamba ametua kwa mabingwa wa kihistoria na sasa ataishi kwa raha zaidi ya alikotoka.

Japo baadhi ya wadau wa soka wametofautiana kwenye 'usajili' wa Manara Yanga, hasa ukizingatia ametokea kwa watani wa jadi, Simba, lakini nguvu yake aliyonayo huenda ikawa na faida kwenye timu hiyo.

Wapo wanaoamini Manara kujiunga Yanga ndiyo anguko lake, lakini pia wapo wanaoamini alichokifanya Manara ni taaluma, ingawa kunaweza kuwa faida au hasara kwake.

Sanifu Lazaro nyota wa zamani wa Yanga anaamini Manara hatokuwa na kipya kujiunga kwake Yanga, huku akitaja kauli zake 'tata' alizokuwa akizitoa dhidi ya Yanga wakati akiwa Simba huenda zikampa wakati mgumu katika ufanyaji kazi wake.

Hata hivyo, Ally Mayay anaamini alichokifanya Manara ni sehemu ya taaluma yake na amethibitisha kwamba inawezekana kwa mtu yeyote kutoka Simba na kujiunga Yanga, vivyo hivyo kwa Yanga kwenda Simba.


"Ni mtu ambaye anaweza promosheni, hivyo binafsi naona hata kujiunga na Yanga ni sahihi kwake kwa kuwa ile ni kazi na si vinginevyo," anasema Mayay.

Nguvu ya Manara

Akiwa Simba, Manara alikuwa na nguvu ya ushawishi kwa mashabiki katika kuzungumzia chapa ya Simba, hususani timu yao na matukio ambayo klabu ilikuwa ikiyafanya.

Manara katika mechi za kimataifa aliwaaminisha Wanasimba kwamba timu yao haiwezi kufungwa nyumbani, licha ya kucheza na timu kubwa barani Afrika ikiwamo Al Ahly na Kaizer Chiefs.

Alikuwa ni kaulimbiu kadhaa ikiwamo ya 'Do or Die', ambazo zilifanikiwa kwa kuongeza hamasa ya mashabiki na hata kwenye timu na matunda yalionekana.

Kwenye mitandao ya kijamii ya twitter, instagram na kwingineko, Manara alikuwa na wafuasi wengi ambao aliwatumia pia kuimarisha Simba katika promosheni.

Kama yote haya atayahamishia Yanga na yakatiki, basi timu hiyo kongwe itakuwa imelamba dume kwenye 'usajili' wa Manara.

Kitakachomkwamisha

Jambo pekee ambalo linaweza kumkwamisha Manara Yanga ni kauli zake 'tata' alizokuwa akizitoa kwa timu hiyo wakati akiwa ofisa habari wa Simba.

Miongoni mwa kauli hizo ni ile ya kwamba hawezi kufanya kazi Yanga labda maiti yake, jambo ambalo linaleta ukakasi na kuwafanya Yanga kugawanyika juu ya 'usajili' huo.

Leo Manara atakuwa na kibarua cha kupindua meza katika tukio lake la kwanza Yanga la kuzindua jezi za timu hiyo baada ya utambulisho jana, huku akikumbukwa pia kwa vibonzo kadha wa kadha alipokuwa Simba kama kile cha Nawakeraaaaaa...... nawaudhiiii...... acheni niwakereeeee, acheni niwaudhiiiiiii na vingine vingi.

Huyu ndiye Manara aliyedumu Simba kwa miaka saba na sasa yuko Jangwani.