Ni Phiri, Luis kikosini Simba

Dar es Salaam. Washambuliaji wa Simba, Luis Miquissone na Moses Phiri wana nafasi ya kuiongoza timu hiyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, Jumamosi.

Ubora waliouonyesha wawili hao katika kipindi hiki cha mapumziko kwenye mechi tatu za kirafiki dhidi ya Kipanga, Cosmopolitan na Ngome na Phiri akifunga mabao mawili na Luis moja ni miongoni mwa sababu zinazompa jeuri kocha Robert Oliveira 'Robertinho' na kuanza kupiga hesabu za kuwapa mechi ya Dyanamos.

Washambuliaji hao hawakuwa kwenye kiwango bora mwanzoni mwa msimu, kwani Phiri alikuwa ametoka kuuguza majeraha, huku Luis akikosa utimamu wa mwili (match fitness) kutokana na kukaa muda mwingi bila kucheza lakini sasa wamejipata.

Nafasi yao kuachiwa mechi na Dyanamos inazidi kuwa kubwa, kwani Simba ipo hatarini kukosa huduma ya Saidi Ntibanzokiza 'Saido', aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa msimu uliopita kwa mabao 17, kutokana na kubanwa na ratiba ya timu ya taifa lake.

Saido yupo nchini Cameroon na timu yake ya Burundi na leo usiku watakuwa wakicheza mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) na baada ya hapo ataanza utaratibu wa kujiunga na Simba.

Hata hivyo, huenda akakwama kujiunga na Simba ndani ya muda tarajiwa, jambo ambalo Robertinho amelishtukia na sasa anatafuta mchezaji atakayeziba pengo la Saido kati ya Phiri na Luis.

Saido amekuwa mhimili wa Simba kwenye safu ya ushambuliaji tangu amejiunga na timu hiyo msimu uliopita na msimu huu ameendelea, akiungana na Clatous Chama, Kibu Denis na Willy Onana kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi.

Hata hivyo, hilo halina shida kwa Simba kwa mujibu wa Robertinho, kwani anaamini Phiri na Luis tayari wamekuwa kwenye utayari wa kucheza.