Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NJE YA UWANJA: Mbrazili anavyoipasua kichwa Yanga

Dar es Salaam. Kiungo Bruno Gomes wa Singida Big Stars kila shabiki anayefatuilia soka la Tanzania kwa sasa anajua jina hilo la kiungo huyu kutoka Brazil kutokana na ubora anaoonyesha.
Bruno licha ya msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu ameendana na kasi na mwisho wa siku amekuwa staa ambaye anategemewa katika kikosi cha Singida Big Stars.

Singida yamtoa Brazil
Bruno anasema hakuwahi kufikiria kwamba anaweza kuja kucheza soka la kulipwa nchini, lakini mwisho wa siku amejikuta akija baada ya wakala wake kumwambia kuna timu imevutiwa na huduma yake.
Kiungo huyo anasema kazi yake imeoneka kupitia mtandao wa YouTube, ndipo Singida Big Stars ikavutiwa na huduma yake na alipopelekewa ofa hakusita kuipokea.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kuja hapa na awali sikuwa nikifahamu kitu kabisa kuhusu Tanzania, wakala wangu alinipigia simu na kuniambia kuna timu imevutiwa na mimi kupitia video zangu walizoziona.
“Ni mara yangu ya kwanza pia kupata dili nje ya nyumbani kwetu Brazil, kwahiyo ilipokuja nikadhani itaanzisha safari nyingine kutoka hapa na kwenda popote pale katika soka,” anasema

Miaka minne yaibania Yanga
Baada ya kujiunga na Singida BS, mabosi wa timu hiyo walimpa mkataba wa miaka miwili lakini kadri siku zilivyokuwa zinaenda mbele mabosi wa timu hiyo walimuongezea tena mkataba wa miaka miwili mingine.
Bruno anasema awalki aliona taarifa za kuhusishwa na Yanga, lakini aliheshimu zaidi mkataba wake na Singida kwa sababu ndiyo timu ambayo imemfanya aonekane na timu nyingine.
“Nakumbuka ilikuwa Agosti ndiyo waliniongezea mkataba mwingine, kwahiyo bado nina miaka mitatu mbele kutoka sasa, ikitokea ofa nzuri naweza kuondoka, lakini kwa sasa mimi ni mchezaji wa Singida.
“Kama mchezaji nilijisikia vizuri kuhusishwa na Yanga kwa sababu maana yake kazi ambayo naifanya nikiwa Singida inaonekana na inapendwa, hauwezi kufatiliwa au kuhusishwa ikiwa haufanyi kitu kizuri.
“Inabidi niipambanie timu yangu izidi kuwa kubwa na kuleta ushindani katika Ligi Kuu ambayo tunashiriki,” anasema.

Bongo ni nguvu tu
Bruno anasema baada ya kufika nchini kitu pekee ambacho kilitaka kumpa tabu ni aina ya soka ambalo amelikuta, ambalo ni kutumia nguvu nyingi kuliko kucheza soka la unyumbulifu.
“Hapa soka lake ni nguvu sana tofauti na nyumbani Brazil, haijanisumbua sana kwa sababu tayari nilikuwa na unyumbulifu, kwahiyo nilichokiongeza ni nguvu na ndiyo maana nacheza,” anasema.
Kiungo huyu anasema chakula hajakutana na changamoto kubwa kwa sababu vyakula vingi vinavyolika hapa ndivyo vipo pia nchini Brazil.
“Lugha ndiyo changamoto kwangu kwa sababu kiingereza sijui, kiswahili ndiyo nimeanza kuzungumza kidogo kidogo, mimi najua kireno na kibrazil tu ila nashukuru uwanjani naelewana na wenzangu,” anasema kiungo huyo.

Uwanja wa Mkapa
Bruno anasema tangu amekuja nchini amecheza katika viwanja vingi, lakini anaukubali zaidi Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, kutokana na nyasi zake zilivyo pamoja na wingi wa mashabiki wanavyoingia.
“Viwanja havinipi changamoto kubwa kama mchezaji, naweza kucheza sehemu yoyote ile lakini Uwanja wa Mkapa ndiyo nipo huru zaidi, halafu napenda namna ambavyo mashabiki wanavyokuwa wengi pale,” anasema Bruno.
Anasema amekutana na timu nyingi za Ligi Kuu zenye wachezaji wazuri, lakini anapojua anakwenda kucheza mechi ya Simba au Yanga, akili yake inakuwa inajiandaa kukabiliana na washindani zaidi.
“Mechi za Simba, Yanga na Azam ndiyo huwa ngumu kwangu kwa sababu timu hizi zimekamilika kila sehemu na hata soka lake jinsi lilivyo wanacheza vizuri, huwa napata wakati mgumu kukabiliana nao,” ansema nyota huyo mwenye mabao tisa ya Ligi Kuu.

Chama, Kagoma wamkuna
Ni ngumu moja kwa moja mchezaji ambaye anacheza Ligi Kuu kuonyesha anakubali uwezo wa mchezaji kutoka timu nyingine, lakini kwa Bruno imekuwa tofauti.
Raia huyo wa Brazil anaweka wazi kukubali kiwango cha kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama hasa kwenye upigaji wake wa mipira ya adhabu pamoja na uwezo wake wa kupiga pasi.
“Chama ni mchezaji mzuri anajua sana kukaa na mpira, kupiga mipira iliyokufa pamoja na pasi zake zenye macho hasa katika kupeleka mashambulizi langoni kwa wapinzani.
“Hapa kwetu pia nakubali sana kiwango cha Kagoma (Yusuph), ni mchezaji mzuri ambaye ana uwezo mkubwa halafu mpambanaji, nadhani akiendelea kuonyesha hii anachokifanya anaweza kufika mbali zaidi,” anasema kiungo huyo.

Balaa la upigaji faulo
Ukianza kutaja majina ya wachezaji ambao ni wakali wa kupiga faulo na kwenda moja kwa moja wavuni, huwezi kuacha jina la kiungo huyu wa Singida Big Stars.
Akizungumzia ubora wake wa kufunga mabao hayo huku akikumbukwa kwa kufunga kwenye mchezo wa Azam FC na Simba, Bruno anasema ni kutokana na kufanya sana mazoezi ya mipira hiyo.
Anasema licha ya mazoezi, akija kwenye mechi huwa anamuangalia kipa wa timu pinzani namna ambavyo amepanga ukuta wake na yeye anajua wapi apige.
“Mfano mechi na Azam FC, kipa wao hakuwa makini, nilipiga mpira haraka na kwenda wavuni, upande wa Simba kipa wao alikuwa makini lakini kwenye upigaji wangu niliongeza nguvu.
“Kweli najua watu wengi wanapenda lile bao nililofunga dhidi ya Simba, lakini mimi napenda nililowafunga Azam FC kwa sababu lilitupa pointi ila upande wa Simba halikuwa na maana kwetu na kwangu,” anasema.

Mtu wa Mungu hasa
Bruno kila akifunga huwa anaonyesha fulana ya ndani ya jezi ambayo inakuwa na maneno ya Biblia, lakini wakati mwingine huonyesha vidole viwili juu.
Kiungo huyu anasema yeye si chochote kile bila Mungu na ndiyo maana akifunga huwa anaelekeza mabao yake kwa Mungu.
“Napeleka ushangiliaji wangu kwa Mungu na Yesu kwa sababu wao kwangu ndiyo kila kitu, sijui kingine zaidi hapa duniani zaidi ya wao.
“Nikifunga si kwa ajili yangu na timu tu, bali ni kwa ajili ya Mungu, imani yangu ni kwamba yeye ndiye atakayeniongoza kwenye kila hatua yangu,” anasema.

Kupata namba Selecao ni ngumu mno
Bruno anang’aa nchini kwa kile anachokifanya, lakini hilo halimfanyi kuwa na uhakika wa kuitwa katika timu ya Taifa ya Brazili (Selecao), hata yeye mwenyewe kama mchezaji amekiri.
Anasema ni ngumu kwake kuicheza Brazili kutokana na wingi wa vipaji vilivyopo, lakini pia kitendo cha wachezaji wao kusambaa nchi mbalimbali.
“Sidhani kwakweli kama naweza kucheza kwa sababu kuna wachezaji wengi wapo kwenye nchi ambazo zipo juu kisoka na bado hawaitwi, Brazil kuna wachezaji wengi sana,” anasema.
Alipoulizwa kuhusu kukua kwenye misingi bora ya soka na kucheza na nyota wa Kibrazili, Bruno anasema: “Kweli nimetokea chini na wachezaji wengi wenye majina, lakini nao niliokuwa nao ni nyota pale nyumbani.”

Achukua mtoto Singida
Bruno amezidi kuonyesha yeye ni mtu wa Mungu kwani akiwa nyumbani kwake Singida amekuwa akionekana na mtoto wa kiume, ambaye ana asili ya kiafrika.
Alipotakiwa kueleza kuhusu mtoto huyo, Bruno anasema aliamua kukaa naye baada ya kuvutiwa jinsi alivyo, hivyo anamsapoti katika kila kitu.
“Nilikutana naye mwanzoni mwa msimu nikiwa na mke wangu, yule mtoto anaitwa Ismail au Suma, naishi naye nyumbani na ninampenda sana.
“Familia yake ipo na mama yake mzazi huwa anakuja nyumani kwangu kumuangalia namna ambavyo mtoto wake anaendelea, nilimpenda jinsi alivyokuwa na uchangamfu wake na nidhamu,” anaeleza Bruno.
Wazungu wengi wamekuwa na kawaida ya kuchukua watoto wa kiafrika kisha huwalea na kuwasomesha na baadaye kuishi nao kama watoto wao wa kuwazaa.


Aiona Singida Big Stars mbali
Bruno anasema huu ni msimu wake wa kwanza akiwa na Singida BS, lakini amejifunza mengi kama mchezaji, hivyo anaamini katika msimu ujao timu hiyo itazidi kuwa tishio.
“Niliambiwa hii ni timu mpya katika Ligi Kuu, lakini angalia namna ambavyo timu ipo na ushindani ambao upo kuanzia kwa wachezaji wenyewe hadi nje.
“Ukweli ni kwamba ikiendelea hivi, Suingida Big Stars tutakuwa miongoni mwa timu ambazo zimekuwa kwa haraka Afrika na kuleta ushindani,” anaongeza.