Nkane amsikilizia Nabi tu
Dar es Salaam. Winga kinda wa Yanga, Denis Nkane amerejea mazoezini baada ya kupona majeraha ya nyonga yaliyomuweka nje tangu Desemba na sasa anamsikiliza kocha mkuu wa kikosi hicho, Nasreddine Nabi ampe nafasi ya kuanza kukiwasha.
Nkane alikaa nje kwa kipindi kisichopungua wiki sita akiuguza jeraha hilo la nyonga, ambalo Daktari wa Yanga, Moses Etutu alithibitisha kuwa alivunjika mfupa mdogo na kusababisha nyonga kujikunja, lakini sasa yupo fiti na tayari kwa mapambano.
Akizungumza jana, Nkane ambaye tayari amejiunga na kikosi cha Yanga katika mazoezi ya jumla, alisema yupo tayari kucheza wakati wowote ambao benchi la ufundi litaamua kumpa nafasi.
“Niko poa sasa, na siku yeyote mtaniona uwanjani nikicheza kwani nimepona tayari,” alisema Nkane.
Aidha, sambamba na Nkane, Mwananchi limethibitisha kuanza mazoezi madogo madogo kwa winga mwingine machachari wa Yanga, Bernard Morrison aliyekuwa nje tangu mwanzoni mwa Feburuari akiunguza jeraha la nyonga.