Ntibazonzika aendeleza furaha Yanga

Muktasari:

Straika mpya wa Yanga, Saido Ntibazonkiza amelinda furaha ya mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kukomboa bao dakika 76 dhidi ya Prisons, iliyokuwa imetangulia kufunga dakika ya 51.

Straika mpya wa Yanga, Saido Ntibazonkiza amelinda furaha ya mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kukomboa bao dakika 76 dhidi ya Prisons, iliyokuwa imetangulia kufunga dakika ya 51.

Ntibazonkiza aliitumia kwa umakini pasi ya Kaseke ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Farid Mussa, kuifungia bao Yanga.

Yanga inaingia mwaka 2021 kwa kishindo kwani ndio timu pekee ambayo haijafungwa mpaka sasa katika mechi 18, imeshinda 14, sare nne ina imekusanya pointi 43.
                                                           
DAKIKA 45 KWANZA


Dakika 45 za kipindi cha kwanza, hazikuwa rahisi kwa mastaa wa Yanga na wenyeji wao Tanzania Prisons, kutokana na Uwanja wa Nelson Mandela kuwa na maji, hivyo walijikuta wakibutuabutua mipira.

Mpira ulianza kwa ugumu, huku wachezaji wa timu zote mbili wakijaribu kupeleka mipira mbele, kuna wakati pasi zilikuwa zinakataa kwenda na mpira kutuama kwanye maji yaliyokuwepo uwanjani kutokakana na mvua kubwa iliyonyesha mchana wa leo.

Angalau mashuti ya mbali ndio yalikuwa na uhai wa kwenda kulenga kwenye malango ya makipa kwa maana ya Metacha Mnata upande wa Yanga na Jeremiah Kusubi kwa upande wa Prisons.

Dakika ya 30 beki namba tatu wa Prisons, Benjamini Asukile alijaribu kupiga shuti la mbali ambalo vipimo vyake vilikosea kidogo tu kulenga lango la Yanga na mpira ule kutoka nje.
Kwa upande wa Yanga, winga wao Mkongomani Tuisila Kisinda licha ya uwanja kuwa na maji, haukumzuia kukimbia mbio akitokea pembeni na dakika ya 41 usingekuwa umakini wa kipa wa Prisons, angeipatia timu yake bao la kuongoza.

Kipa wa Prisons aliongeza umakini wa kumsoma Kisinda baada ya kuona mabeki wake wa pembeni wamezidiwa mbio, hivyo akaudaka mpira.

Ukiachana na changamoto ya uwanja kuwa na maji, bato ya Said Ntibazonkiza na Jumanne Elifadhir ilikuwa kali kwani alipokuwa anatua mguu Ntibazonkiza na Elifadhir alikuwa nyuma yake na kufanya mashabiki wa Yanga kushindwa kufaidi utamu wa mguu wa staa wao kutoka Burundi.

Dakika ya 51 Prisons ilipata bao, baada ya Charles kupiga faulo na Elifadhir kumalizia kwa pasi, huku mabeki wa Yanga wakiwa hawana la kufanya baada ya kuruka na kukosa mpira.

Bao hilo ni kama liliwaamsha Yanga kupambana zaidi ili kupata bao la kusawazisha na kuna muda nyota wa Yanga Ntibazonkiza alipiga mpira wa tikitaka nje ya 18, lakini ulipita juu kidogo ya goli la mlinda mlango wa Prisons.

Dakika ya 63 Yanga ilikosa bao baada ya Michael Sarpong kubaki na kipa wa Prisons na kupiga mpira uliookolewa na Kisubi mlinda lango wa Prison jambo ambalo Deus Kaseke ni kama lilimtoa imani na kwenda kukagua eneo la mlinda mlango wa upinzani kama kuna chochote kimewekwa.

Mabadiliko aliyoyafanya kocha wa Yanga, Cedrick Kaze dakika ya 60 kumtoa Farid Mussa na kumuingiza Kaseke kuliichangamsha safu ya mbele ya timu hiyo kushambulia zaidi kipindi cha pili, ambacho Prisons ilikoswakoswa.

Dakika 76 Yanga ilisawazisha bao kupitia kwa Ntibazonkiza baada kutokea pige nikupige na mabeki wa Prisons, umakini wake ukafanya aitumie vyema pasi ya Kaseke.

Bao la Yanga lilifungwa sekunde chache baada ya kocha wa Prisons,Salum Mayanga kumtoa Kimenya ambaye alikuwa anatumia akili kumkaba Tuisila, nafasi yake akachukua Ezekiel Mwashilindi, aliyekuwa beki wa zamani wa Yanga B.
Mayanga aliendelea kufanya mabadiliko akamtoa Mohamed Mkopi na nafasi yake ikachukuliwa na Kassim Mdoe.

Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, kocha wa Yanga, Kaze alisema kipindi cha kwanza wachezaji walijikuta wakicheza aina ya mipira mirefu waliyokuwa wanacheza nyota wa Prisons, lakini wakaja na plani B raundi ya mwisho iliyowapa bao.

"Kipindi cha pili, tulikuwa tunacheza pasi kidogo, huku tukitafutia bao kutokea pembeni, lakini kwa bahati mbaya tumeambulia sare, jambo la kuwaambia Wanayanga wawe wavumilivu tuna mwelekeo mzuri wa malengo yetu," alisema.
Naye Kaseka ambaye alionekana nyota wa mchezo huo baada ya kuivuruka mipango ya mabeki wa Prisons, alisema walipambana kwa kadri walivyoweza lakini bahati haikuwa upande wao.

Nahodha wa Prisons, Asukile alisema baada ya kupata bao dakika ya 51 walipunguza kasi, huku Yanga ilikuwa inakusanya nguvu iliowafanya wasawazishe bao.
"Ni kama tulipunguza kasi, Yanga ikaongeza nguvu ambayo imewapa ushindi wa bao walilosawazisha," alisema.
 
Mechi nyingine Azam FC iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania ambao unakuwa ushindi wao kwanza baada ya kutoshinda mechi sabab mfululizo na Namungo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Kikosi cha Yanga Metacha Mnata, Kibwana Shomary, Yasin Mustapha, Limine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tunombe, Tuisila Kisinda, Fei Toto, Farid Mussa, Saido Ntibazonkiza na Michael Sarpong.

Kikosi cha Prisons ni Jaremeah Kisubi, Michael Ismail, Benjamin Asukile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elifadhir, Salum Kimenya, Lambart Charles, Mohamed Salum, Samson Baraka na Jaremia Juma.