Nyota hawa wanazibeba timu zao AFCON 2025
Muktasari:
- Hadi sasa ni wachezaji 12 waliochaguliwa kuwa nyota wa mchezo katika raundi ya kwanza ya makundi ya AFCON 2025.
Katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yanayoendelea huko Morocco, hadi sasa imeshapigwa michezo 12 ya raundi ya kwanza katika hatua ya makundi. Hata hivyo, imeonekana wachezaji wanaokipiga kwenye ligi mbali mbali Ulaya na Uarabuni ndiyo wanaozibeba timu zao kupata matokeo mazuri kwa asilimia kubwa.
Ili timu iweze kupata matokeo mazuri uwanjani, ubora wa kila mchezaji unahitajika, lakini baada ya mchezo kumalizika huwa anakuwepo mmoja ambaye anatajwa kama mchezo bora wa mchezo (Man of the Match).
Kawaida mchezaji bora wa mchezo ni yule anayeonyesha kiwango bora uwanjani kinachochangia timu yake kupata matokeo mzuri. Nyota wa mchezo si lazima awe amefunga bao peke yake kwani anaweza kuwa hata ametoa pasi ya mwisho na kuonyesha kiwango kikubwa uwanjani ndipo akachaguliwa.
Tukirejea katika michuano hii ya AFCON 2025, inayoendelea nchini Morocco, katika mechi 12 za raundi ya kwanza kwenye hatua ya makundi, takribani wachezaji 12 wanaokipiga nje ya ligi za Bara la Afrika wamechaguliwa kuwa nyota wa michezo hiyo.
Hii ina maana kwamba wachezaji hao ndiyo wameonyesha viwango bora hadi sasa na kuzisaidia timu zao kupata matokeo mazuri.
Ifuatayo ni orodha ya wachezaji bora wa kila mchezo katika raundi ya kwanza ya hatua ya makundi.
Brahim Diaz
Huyu ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Morocco anayekipiga kwenye klabu ya Real Madrid inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania 'La Liga'.
Diaz alionyesha kiwango bora kwenye mchezo wa ufunguzi uliopigwa Desemba 21, mwaka huu wakati Morocco ilipokuwa ikikabiliana na Comoros, kwenye Uwanja wa Moulay Abdellah jijini Casablanca.
Katika mchezo huo Morocco ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0 huku Diaz akifunga bao la kwanza kabla ya Ayoub El Kaabi kufunga la pili. Katika mchezo huo nyota huyo alionyesha kiwango cha juu na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.
Lassine Sinayoko
Huyu ni mshambuliaji wa Kimataifa wa Mali anayecheza Ligi Kuu ya Ufaransa 'League One' katika Klabu ya Auxerre. Sinayoko alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo katika mechi dhidi ya Zambia ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Mohamed V.
Katika mchezo huo, Sinayoko alikuwa wa kwanza kuifungia Mali bao la kuongoza katika dakika ya 61 kabla ya mshambuliaji wa Zambia, Patson Daka anayekipiga Leicester City ya England kusawazisha katika dakika za majeruhi.
Lyle Foster
Nyota huyu wa Afrika Kusini aliisaidia timu yake kuibuka na ushindi dhidi ya Angola baada ya kufunga bao la ushindi katika mchezo ambao Bafana Bafana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Marakech.
Foster ambaye anakipiga kwenye Klabu ya Burnley ya pale Ligi Kuu nchini England 'EPL' alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo uliopigwa Desemba 22 baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi katika dakika ya 79.
Omar Marmoush
Katika mchezo kati ya Misri dhidi ya Zimbabwe uliopigwa Kwenye Uwanja wa Adrar mjini Agadir, nyota wa kimataifa wa Misri, Marmosh alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo baada ya kuonesha kiwango kizuri alipoifungia timu yake bao la kusawazisha kwani Zimbabwe ilikuwa mbele kwa bao moja ambalo liliwekwa wavuni dakika ya 20 na Prince Dube.
Marmosh anayekipiga Manchester City ya England alifunga bao hilo kwa ustadi dakika ya 64 kabla ya Mohamed Salah wa Liverpool kufunga la ushindi katika dakika za majeruhi.
Théo Bongonda
Nyota huyu anachezea Klabu ya Spartak Moscow ya Urusi, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo katika mechi iliyoikutanisha DR Congo dhidi ya Benin iliyopigwa Desemba 23 kwenye Uwanja wa Al Barid huko Rabat, Morocco.
Katika mchezo huo Bongonda alionyesha kiwango bora na kuifungia DR Congo bao moja ambalo lilidumu hadi dakika 90 zinamalizika na DR Congo ikaibuka na ushindi.
Nicholas Jackson
Huyu ni mshambuliaji wa Kimataifa kutoka Senegal anayekipiga kwenye Klabu ya Bayern Munich kwa mkopo akitokea Chelsea ya England.
Jackson alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kati ya Senegal dhidi ya Botswana uliopigwa Desemba 23 kwenye Uwanja wa Ibn Batouta ambapo Senegal iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Katika mchezo huo, Jackson alifunga mabao mawili katika dakika ya 40 na 58 kabla ya kufanyiwa mabadiliko dakika ya kumpisha Cherif Ndiaye ambaye alifunga bao la tatu dakika za mwishoni mwa mchezo.
Semi Ajayi
Huyu ni beki wa kati wa Nigeria anayekipiga kwenye Klabu ya Hull City inayoshiriki ligi daraja la kwanza England 'Championship'.
Ajayi alionyesha kiwango bora katika mchezo dhidi ya Tanzania 'Taifa Stars' uliopigwa Desemba 23 kwenye Uwanja wa Fez na akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Nigeria kupata ushindi wa mabao 2-1.
Beki huyo ndiye aliyeipa 'Super Eagles' bao la kuongoza dakka ya 36 kabla ya Ademola Lookman kufunga la pili dakika ya 52 baada ya Charles M'Mbobwa kuisawazishia Tanzania dakika ya 50.
Elias Achouri
Huyu ni mshambuliaji wa Tunisia anayekipiga kwenye Klabu ya Copenhagen ya Denmark, Achouri alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo uliozikutanisha Tunisia na Uganda Desemba 23 kwenye Uwanja wa Olympique de Rabat.
Katika mchezo huo, Tunisia iliondoka na ushindi wa mabao 3-1 huku mshambuliaji huyu akifunga mara mbili na kuwa ndiye mfungaji bora wa AFCON hadi sasa akiwa na mabao mawili sawa na Mahrez wa Algeria.
Edmond Tapsoba
Huyu ni beki wa kimataifa kutoka Burkina Faso anayecheza kwenye Klabu ya Bayern Levakusern inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ujerumani 'Bundesliga'.
Tapsoba alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo uliochezwa Desemba 24 kwenye Uwanja wa Mohamed V jijini Casablanca. Katika mchezo huo uliomalizika kwa Burkina Faso kuibuka ushindi wa mabao 2-1, Tapsoba alionyesha kiwango bora baada ya kufunga bao la pili dakika za majeruhi na kuisaidia timu yake kuondoka na pointi tatu muhimu.
Riyad Mahrez
Mshambuliaji huyu anayekipiga kwenye Klabu ya Al Ahli ya Saudi Arabia, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo uliozikutanisha Algeria na Sudan Desemba 24 kwenye Uwanja wa Prince Moulay Hassan jijini Rabat.
Katika mchezo huo Algeria iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku Mahrez akitupia mawili kambani katika dakika ya pili na 61 huku bao la tatu likifungwa na Ibrahim Maza dakika ya 85.
Amad Diallo
Wengi wanamjua nyota huyu kwa kuwa anakipiga kwenye Klabu maarufu duniani ya Manchester United. Mshambuliaji huyu wa Ivory Coast alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Mozambique uliochezwa Desemba 24 kwenye Uwanja wa Marakech.
Katika mchezo huo, Diallo aliipa ushindi timu yake baada ya kufunga bao moja ambalo lilidumu hadi mwamuzi alipopuliza kipyenga cha mwisho.
Bryan Mbeumo
Kama ilivyokuwa kwa Diallo, ndivyo ilivyo kwa Mbeumo ambaye pia anatambulika na mashabiki wengi wa soka kutokana na kuichezea Manchester United ambayo ni moja ya timu kubwa yenye mashabiki wengi duniani.
Mshambuliaji huyu anayeiwakilisha Cameroon katika michuano ya AFCON 2025, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Gabon uliopigwa kwenye Uwanja wa Adrar Desemba 24, mwaka huu.
Katika mchezo huo, Cameroon iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Karl Etta Eyong kwa pasi ya mwisho iliyopigwa na Mbeumo ambaye pia alionyesha kiwango bora.