NYUMA YA PAZIA: Tumuombee Pogba yupo katika miaka ya tabu

MWAKA wa tabu. Aliwahi kuimba rafiki yangu Ally Choki. Moja kati ya nyimbo bora ambazo zinaashiria matatizo ya mfululizo kwa mwanadamu. Wakati mwingine ni kama filamu ya kutungwa. Wakati mwingine inatokea katika maisha ya mwanadamu.

Anafariki baba, unafiwa na mtoto, ghafla mahakamani unakutwa na hatia kwa kosa usilofanya na unafungwa, ukirudi uswahilini unakuta mkeo ameolewa. Kuna wanadamu huwa wana mlolongo wa matatizo ingawa huwa hayafanani.

Ni kama inavyomtokea Paul Pogba kwa sasa. Tuanzie wapi? Sijui. Akiwa na Manchester United dunia iligawanyika. Kipaji chake kilikuwa hadharani kwa kila mtu kukiona. Wapo waliokuwa wanamponda kwamba hana msaada katika timu, wapo waliona kwamba alikuwa na uwezo mkubwa.

Kilichokera zaidi ni maisha yake binafsi. Ubishoo kama walivyo Wafaransa wengi. Kila siku kubadili staili za nywele. Kila siku kujiona staa pengine kuliko mastaa wa ukweli wa wakati huo kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Wakati huo Pogba hakuwa na maisha ya kuhurumiwa sana, lakini sasa wote tunaweza kumuonea huruma Paul. Ana mikasa mingi ambayo inaleta ladha mbaya katika mdomo wa mwanadamu. Ilianzia pale alipoamua kurudi Juventus.

Kwanza kabisa, wakala wake, Mino Raiola alifariki juu ya kitanda cha hospitali ya San Raffaele jijini Milan Januari 2022. Huyu ndiye mtu aliyempa Pogba utajiri mkubwa. Ndiye ambaye wakati ule aligombana na Sir Alex Ferguson kwa kumhamisha bure Pogba kutoka Manchester United kwenda Juventus, huku Sir Alex akisubiri mchezaji wake aingie katika kikosi cha kwanza.

Pia ndiye wakala ambaye hatimaye alifanikiwa kumrudisha Pogba Manchester United mwaka 2016 katika dili ambalo lilivunja rekodi ya uhamisho wa dunia. Pogba pia akawa miongoni mwa mastaa wanaolipwa pesa nyingi duniani. Kifo cha Raiola kilimuacha Pogba akiwa mpweke.

Kadri mwaka 2022 ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo ambavyo dunia ilikuwa inajiandaa na michuano ya Fainali za Kombe la Dunia ambayo ingefanyika Qatar. Julai Pogba akaumia goti. Ikaonekana kama vile angekaa miezi miwili nje.

Baadaye ikaonekana kwamba alihitaji upasuaji. Naam, akajikuta analikosa Kombe la Dunia ambalo nchi yake Ufaransa ilikwenda hadi fainali na kuonekana kama ingetetea baada ya kutwaa michuano ya 2018. Kama Kolo Muani angefunga lile bao alilokosa dakika za majeruhi dhidi ya Argentina huenda Pogba angekuwa pia amekosa kuchukua Kombe la Dunia.

Halafu ikaja zahma nyingine ya kijinga. Kaka yake Pogba, Mathias Pogba akaunda kikundi cha wahuni wenzake na kuanza kumzunguka kaka yake, huku akidai kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa Pogba kwa madai ya kuendelea kumtunzia siri zake ambazo anazo.

Mathias hakuona njia nyingine ya kupata pesa kutoka kwa Pogba zaidi ya kumtishia kwamba angetoa siri zake kadhaa. Moja kati ya siri hizo ni madai kwamba Pogba alikuwa ni mshirikina na aliwahi kumroga staa mwenzake wa Ufaransa, Kylian Mbappe ili yeye awe staa zaidi.

Umewahi kufikiria ujinga wa namna hii? Ndugu yako wa damu anajaribu kukutoa shimoni na kukuchomoa noti. Mwishowe Pogba alikiri kwamba pesa zimemgombanisha na ndugu zake.

Katika mtandao wa Al Jazeera aliripotiwa akidai: “Panapokuwa na pesa inabidi uwe makini sana. Pesa zinawabadili watu. Zinaweza kuvunja familia na kuleta vita. Kuna wakati nilikuwa nakaa mwenyewe nasema ‘Sitaki kuwa na pesa tena. Sitaki kucheza soka tena, nataka kuwa mtu wa kawaida ili wanipendwe kama nilivyo na sio kwa sababu ya pesa.”

“Wakati mwingine ni vigumu, lakini Mungu alinisaidia. Nilifahamu hilo katika maisha inabidi upambane. Inakufanya uwe imara zaidi,”  alimalizia Pogba. Huyu ndiye mchezaji ambaye licha ya kuwa na pesa nyingi lakini kumbe moyo wake ulikuwa unawaka moto.

Kuongezea chumvi katika kidonda kibichi, mapema wiki hii imegundulika kwamba Pogba alikuwa anatumia dawa zisizoruhusiwa michezoni. Baada ya kukaa nje kwa muda mrefu aliingia uwanjani kucheza pambano dhidi ya Bologna. Kisha tena Juve ikaja kushinda 3-0 ugenini didi ya Udinese Agosti 20. Ukweli mchungu ni kwamba Pogba alikuwa ni ‘sabu’ ambaye hakutumika, yaani haku-cheza hata dakika moja.

Lakini mamlaka ya udhibiti wa dawa zinazokatazwa michezoni nchini Italia (NADO) ikathibitisha kwamba Pogba amebainika anatumia dawa za kuongeza nguvu katika vipimo vya kawaida tu ambavyo wachezaji hufanyiwa michezoni.

Na sasa amesimamishwa kucheza soka kwa muda usiojulikana. Ikigundulika kwamba ana hatia kuna uwezekano mkubwa Pogba akafungiwa kifungo kirefu asicheze soka.

Huyu ndiye Pogba ambaye anakumbana na majaribu kwa sasa. Jaribu kumtazama mrundikano wa matatizo aliyonayo. Kama unadhani kwamba Harry Maguire ni miongoni mwa wachezaji wenye bahati mbaya duniani, basi fahamu kwamba Pogba ndiye mchezaji anayepitia wakati mgumu zaidi kwa sasa.

Ameandamwa na matukio mengi kimya kimya. Ni vile tu kwa sasa hachezi tena England na ndio maana watu wameacha kumfuatilia. Hata hivyo ukweli ni kwamba wengi tumemsahau kwa sababu anapitia kipindi kigumu.

Anapitia majeraha, vifo, vita ya familia, lakini sasa yupo katika habari ya madawa. Kama akinusurika na janga hili basi ni vema katika umri wake wa miaka 30 akaamua kwenda zake Saudi Arabia kuchota noti za Waarabu.

Tatizo kama akigundulika kwamba ni kweli alitumia kwa makusudi dawa za kuongeza nguvu michezoni basi kifungo kitamfuata popote alipo. Kitu ambacho kipo wazi zaidi ni kwamba huu unaweza kuwa mwanzo wa mwisho wake. simuoni akiibuka tena.

Sijui kama hizi ni laana za Sir Alex ambaye alikasirika mno pale Pogba alipoondoka Manchester United, wakati yeye binafsi alikuwa anamuandaa kucheza nafasi ya Paul Scholes. Hatuwezi kujua. Kitu kilicho wazi ni kwamba hana nafasi tena ya kurudi kucheza soka katika kiwango cha juu zaidi.