Lukaku anavyofukuzia rekodi ya mastaa hawa Ulaya

Lukaku anavyofukuzia rekodi ya mastaa hawa Ulaya

Muktasari:

  • CHELSEA inahangaika kunasa straika mpya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na sasa wanahamishia nguvu yao kwa mchezaji wa zamani kumaliza tatizo linalowakabili.

LONDON, ENGLAND. CHELSEA inahangaika kunasa straika mpya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na sasa wanahamishia nguvu yao kwa mchezaji wa zamani kumaliza tatizo linalowakabili.

Timo Werner ameshindwa kumaliza kiu ya timu hiyo kushuhudia ikifunga mabao ya kutosha baada ya usajili wake wa pesa nyingi kutoka RB Leipzig kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.

Tammy Abraham yupo kwenye orodha ya watakaopigwa bei na Olivier Giroud tayari ameshaachana na timu hiyo ya Stamford Bridge.

Kocha Thomas Tuchel mipango yake ni kushusha straika mpya kwenye safu yake ya ushambuliaji, ambapo staa wa Erling Haaland ulikuwa mpango namba moja, lakini Wajerumani Borussia Dortmund wameweka ngumu kwa kumuuza pesa nyingi. Na sasa Chelsea wanaangalia kwenye unafuu, wakirudi kwa straika wao wa zamani, Romelu Lukaku.

Lakini, Inter Milan inayommiliki Lukaku kwa sasa, imeng’ang’ania ilipwe Pauni 100 milioni - kiwango cha pesa ambacho The Blues ipo tayari kukilipa ili kumrudisha straika huyo Stamford Bridge, mahali ambako itakuwa ikimlipa mshahara wa Pauni 250,000 kwa wiki - kama inavyoelezwa.

Hata hivyo, Lukaku atakapokamilisha dili lake la kurudi Chelsea, hatakuwa mchezaji wa kwanza kujiunga na timu yake ya zamani baada ya jambo hil kufanywa na masupastaa kibao wa maana kabisa kwenye soka.

Didier Drogba - Chelsea

Awamu ya kwanza: 2004-2012

Awamu ya pili: 2014-2015

Hakuna ubishi, Drogba ni moja wa mastraika bora kabisa waliowahi kuichezea Chelsea kwenye zama za Ligi Kuu England. Staa huyo wa Ivory Coast alishinda mataji 10 kwa muda wake aliotumikia timu hiyo ya Stamford Bridge katika awamu yake ya kwanza. Drogba alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja katika miaka minane. Baada ya kuondoka kwa miaka miwili, akienda kutamba Shanghai Shenhua na Galatasaray - Drogba alirejea Chelsea mwaka 2014 na kuisaidia timu hiyo kubeba ubingwa mwingine wa Ligi Kuu England na kupandisha zaidi hadi yake kuwa gwiji wa The Blues.

Thierry Henry - Arsenal

Awamu ya kwanza: 1999-2007

Awamu ya pili: 2012 (mkopo)

Supastaa mwingine matata kabisa kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England. Henry aliondoka Arsenal baada ya miaka minane, akiwa amebeba mataji mawili ya Ligi Kuu England, ikiwamo lile la msimu wa 2003-04, ambapo Arsenal ilicheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza. Staa huyo alitimkia zake Barcelona mwaka 2007 na baadaye akatimkia New York Red Bulls kwenye kumalizia maisha yake ya soka mwaka 2010.

Mwaka 2012, Henry alirudi Arsenal kwa mkopo wa miezi miwili, aliponaswa kuja kuchukua nafasi za Marouane Chamackh na Gervinho - waliokuwa majeruhi kwenye kikosi hicho kilichokuwa chini ya Arsene Wenger kwa wakati huo.

Robbie Fowler - Liverpool

Awamu ya kwanza: 1993-2001

Awamu ya pili: 2006-2007

Fowler alijipatia umaarufu mkubwa sana kwa mashabiki wa Liverpool na walimuita kuwa mungu wao. Pamoja na mapenzi yote hayo, Fowler aliwavunja mioyo Kop alipoamua kutimkia zake Leeds United mwaka 2001, mahali ambako alicheza kwa miaka miwili kabla ya kwenda kujiunga na Manchester City. Baada ya kutemwa na Man City mwaka 2006 kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara, Fowler alirudi zake Liverpool ambako alikwenda kuwachangia mabao 12, ikiwamo manane kwenye Ligi Kuu England.

Gareth Bale - Tottenham

Awamu ya kwanza: 2007-2013

Awamu ya pili: 2020-2021

Bale alitamba sana kwenye soka akiwa White Hart Lane kabla ya kupata dili lililomfanya awe mchezaji ghali zaidi duniani, aliponyakuliwa na Real Madrid mwaka 2013. Baada ya kupata mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Real Madrid kwa miaka yake ya mwanzo, staa huyo wa kimataifa wa Wales, mambo yalikuja kutibuka baada ya timu hiyo kuwa chini ya kocha Zinedine Zidane. Aliwekwa benchi kwa muda mrefu kabla ya msimu uliopita kurudi kwa mkopo kuitumikia Spurs, alikomaliza msimu na kupata nafasi ya kwenda kuitumikia Wales kwenye michuano ya Euro 2020.

Wayne Rooney - Everton

Awamu ya kwanza: 2002-2004

Awamu ya pili: 2017-18

Supastaa, Wayne Rooney alilitambulisha jina lake kwenye soka baada ya bao matata kabisa alilowafunga Arsenal mwaka 2002 kipindi hicho akiwa Everton na kabla ya kunaswa na Manchester United. Kinara huyo wa mabao wa muda wote wa England na Man United, alikwenda kutamba Old Trafford kwa miaka 13, akibeba mataji matano ya Ligi Kuu England, taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuyataja kwa uchache. Mwaka 2017, Rooney alirudi zake Everton na kucheza kwa msimu mmoja kabla ya kutimkia zake MLS side DC United mwaka 2018.

Sol Campbell - Arsenal

Awamu ya kwanza: 2001-2006

Awamu ya pili: 2010

Beki Sol Campbell alilitikisa soka la England mwaka 2001 wakati alipoamua kujiunga na Arsenal bure kabisa akitokea kwa mahasimu wao wakuu, Tottenham Hotspur. Baada ya miaka mitano kwenye klabu hiyo ya Arsenal, beki huyo wa zamani wa England alikwenda kuitumikia Portsmouth kwa miaka mitatu kabla ya kuibukia Notts County kwenye nyakati za mwisho kabisa za soka lake. Lakini, Campbell alifanya maajabu mengi alipoachana na timu hiyo ya Midlands siku chache tu baada ya kucheza mechi yake ya kwanza na aliamua kwenda kufanya zake mazoezi huko Arsenal ili kujiweka fiti. Kocha Arsene Wenger alimuona anafaa na kumpa nafasi nyingine ya kuitumikia Arsenal, ambapo alicheza mechi 14 za kumalizia msimu wa 2009-10 kabla ya kutimkia Newcastle - alikokwenda kustaafu.


Paul Pogba - Man United

Awamu ya kwanza: 2009-2012

Awamu ya pili: 2016-hadi sasa

Pogba alikuwa amecheza mechi saba tu kwenye kikosi cha kwanza kwenye awamu yake ya kwanza Manchester United kabla ya kutimkia zake Juventus. Kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 19, ambapo uhamisho wake huo wa kwenda Juventus ulimpa staa huyo wa Ufaransa kwenda kutengeneza jina lake na kuwa mmoja wa viungo bora kabisa kwenye soka la dunia. Mwaka 2016, Man United iliamua kumrudisha kwenye kikosi chao mchezaji huyo, ambapo ililipa ada ya uhamisho ya Pauni 89 milioni iliyovunja rekodi kwa kipindi hicho. Kwa sasa Pogba amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake huko Old Trafford na kinachosemwa kwa sasa anaweza kupigwa bei kama ataendelea kugomea kusaini mkataba mpya.

Jermain Defoe - Tottenham

Awamu ya kwanza: 2004-2008

Awamu ya pili: 2009-2014

Katika awamu yake ya kwanza kwenye kikosi cha Tottenham - akiwa amesajiliwa kutoka West Ham - Defoe alijitengenezea nafasi kubwa kwenye kikosi cha kwanza cha England kwa sababu alikuwa akicheza soka maridadi kabisa na kuwa straika supastaa. Mwaka 2008, Spurs ikampiga bei kwenda Portsmouth kucheza chini ya Harry Redknapp. Mwaka mmoja baadaye Redknapp alipata kazi Spurs na kuamua kurudi na mshambuliaji huyo kwenye kikosi hicho cha Spurs. Safari hii, Defoe alidumu White Hart Lane kwa miaka mitano, akifunga mabao 79.

Juninho - Middlesbrough

Awamu ya kwanza: 1995-1997

Awamu ya pili: 1999-2000 (mkopo)

Awamu ya tatu: 2002-2004

Fundi huyo wa mpira wa Kibrazili alikuwa na mapenzi ya dhati na Middlesbrough baada ya kuichezea timu hiyo kwa awamu tatu tofauti. Juninho aliisaidia Middlesbrough kufika fainali ya Kombe la FA na Kombe la Ligi mwaka 1997, lakini aliondoka kwenda kujiunga na Atletico Madrid baada ya timu hiyo kushuka daraja. Baada ya hapo, alirudi Middlesbrough kwa mkopo katika msimu wa 1999-2000, lakini majeruhi yalitibua maisha yake. Juninho alirudi tena kwenye timu hiyo mwaka 2002, kuisaidia klabu hiyo ya Riverside kushinda Kombe la Ligi mwaka 2004 na kuwaingiza kwenye michuano ya Ulaya.

Nemanja Matic - Chelsea

Awamu ya kwanza: 2009-2011

Awamu ya pili: 2014-2017

Chelsea ilimsajili staa huyo wa Serbia kwa ada ya Pauni 1.5 milioni mwaka 2009. Lakini, Matic alicheza mechi tatu tu za kikosi cha kwanza cha The Blues kabla ya kutolewa kwa mkopo Vitesse Arnhem na kisha kuuzwa Benfica. Baada ya miaka mitatu ya kibabe Ureno, Chelsea walimrudisha kwenye kikosi chao, wakilipa Pauni 21 milioni kunasa siani yake. Matic aliisaidia Chelsea kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu England kabla ya kuipa faida timu hiyo kwa karibu Pauni 20 milioni wakati alipojiunga na Manchester United mwaka 2017, ambako yupo hadi sasa.

Wachezaji wengine

Orodha ya mastaa waliorudi klabu za zamani ni ndefu, ambapo wakali wengine waliofanya hivyo ni hawa hapa; Shinji Kagawa (Borussia Dortmund), Peter Crouch (Portsmouth), Carlos Tevez (Boca Juniors), Mathieu Flamini (Arsenal), Joe Cole (West Ham), Teddy Sheringham (Tottenham), Claudio Pizarro (Werder Bremen), Kaka (AC Milan), Mark Hughes (Man United), Robbie Keane (Tottenham), Mario Gotze (Borussia Dortmund), Mats Hummels (Borussia Dortmund).