Bao la Chama laibuliwa Msimbazi
Dar es Salaam. Wakati Yanga ikisherehekea paredi la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tano mfululizo, mashabiki wa Simba wamezidi kujifariji kwa bao lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Clatous Chama katika mechi kati ya timu hizo ya 'Kariakoo Derby', ya Mei 3, 2026.
Hali hiyo imejitokeza katika mitaa ya Msimbazi wakati Yanga iliposimama kwa ajili ya kusherehekea ubingwa huo ikiwa ni njia ya kuwakejeli watani zao wa jadi, Simba ambao wamekosa taji hilo kwa mara ya tano mfululizo.
Wakati Yanga ilipowasili mitaa ya Msimbazi, kulikuwa na skrini kubwa iliyokuwepo ambapo ilitumika kwa ajili ya kuonyesha bao la Chama ikiwa ni njia ya kujibu mapigo kutokana na mashabiki wa Yanga kushangilia taji hilo katika maeneo hayo ya Msimbazi.
Katika mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya timu hizo maarufu 'Kariakoo Derby', Chama alifunga bao kwa staili ya tiki-taka likiwa ni miongoni mwa mabao bora, yanayopigiwa chaguo ya kushinda bao bora la msimu wa 2025-2026.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, Dar es Salaam, Mei 3, 2026, iliisha kwa miamba hiyo kutoka sare ya mabao 2-2.