Inawezekana tumeuona mwisho wa Jose Mourinho

Ushindi kidogo tu, Mourinho aanza kiburi

Muktasari:

  • Hata kama kwa mara nyingine Jose anakwenda kuvuna kitita cha Pauni 15 milioni kama fidia kwa kufukuzwa kazi, lakini hakuna mwanadamu anayependa kufukuzwa kazi.

TOUGH times never last, but tough people do. Alijisemea hivi mzungu mmoja. Sisi Waswahili tukatafsiri kiurahisi tu kwa kusema: “Nyakati ngumu hazipiti, lakini watu wagumu wanapita.”

Hakuna tulichopunguza wala kuongeza. Inawezekana ni katika maisha ya kazi. Inawezekana ni katika maisha ya dunia. Yuko wapi Saddam Hussein? Vipi kuhusu Fidel Castro? Vipi kuhusu Hugo Chavez? Na unasemaje kuhusu Idd Amin na wengineo? Hawapo tena. Waliondoka duniani.

Lakini katika maisha ya kazi nako kunashangaza. Watu huja, hutamba na kisha huondoka. Nilikuwa nikimtazama Jose Mourinho akibeba mizigo yake na kuondoka katika uwanja wa mazoezi wa Tottenham Hotspurs, Enfield Town pale London Kaskazini. Tabasamu usoni, lakini huzuni moyoni.

Alikuwa amefukuzwa na Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy. Alikuwa akiondoka kazini kwa mara nyingine tena. Hakuna mwanadamu anayependa kufukuzwa kazi. Hakuna.

Hata kama kwa mara nyingine Jose anakwenda kuvuna kitita cha Pauni 15 milioni kama fidia kwa kufukuzwa kazi, lakini hakuna mwanadamu anayependa kufukuzwa kazi.

Tangu mwaka 2013 aliporudi Chelsea, Jose amefukuzwa kazi mara tatu. Hii ilikuwa mara ya tatu. Alifukuzwa na Chelsea yenyewe, akafukuzwa na Manchester United na sasa amefukuzwa na Tottenham. Ni mwisho wa Jose? Nadhani tumeuona mwisho wake.

Hawa wawili wa kwanza wangeweza kumtunishia misuli Mourinho, lakini huyu ambaye amemfukuza kocha huyo mapema wiki hii ametufanya tutafakari na kuanza kuamini kwamba huenda tumeuona mwisho wa Mreno huyo.

Ikiwa na ubingwa wake wa mwisho wa Ligi ilioutwaa miaka 60 iliyopita mnamo mwaka 1961, Spurs inapata wapi kiburi cha kumfukuza Mourinho, tena ikiwa siku sita kabla haijacheza fainali yake ya michuano ya Carabao dhidi ya Manchester City?

Spurs wanapata wapi ubavu wa kumfukuza Mourinho huku taji lao la mwisho wakiwa wametwaa mwaka 2007? Ni wazi kwamba wameona inatosha. Kwa walichokiona kwa Mourinho hawana hamu tena. Unamfukuzaje kocha wa mataji kama yeye? Nadhani wameona suala la mataji kutoka kwa Mourinho imebakia historia.

Wameona wazi kwamba Spurs haichezi kama ile ya Mauricio Pochettino. Nadhani wamegundua kwamba Jose hana maajabu tena. Hana maajabu ya aina mbili. Kwanza hachezi soka la kuvutia kama makocha wengi wa kisasa wanavyofanya. Lakini pili wameona hata ubunifu wake katika kushinda mechi kwa namna yoyote ile umetoweka.

Spurs ilikuwa katika makali yake ikiwa na watu wanne pale mbele. Harry Kane, Son Heung-Min, Dele Alli na Christian Erikssen. Walifika hadi fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini leo tuna Tottenham ambayo hatujui inachotaka uwanjani.

Leo tuna Spurs ambayo hatujui kama ina ubora katika kukaa na mpira au ina ubora katika kujihami, ama ina ubora katika kushambulia. Kifupi ni kwamba haivutii kutazama. Wakati ikiwa na Pochettino ilikuwa inavutia kuitazama licha ya ukweli kwamba hawakushinda lolote.

Wakati huu wakiwa na Jose haivutii kutazama na haionekani kama inaweza kutawala soka la Ulaya hata kwa mbinu za kizamani za Mourinho ambazo zilimuwezesha kutwaa ubingwa wa Ulaya akina na Porto na Inter Milan.

Spurs baada ya kukosa mataji kwa miaka mingi inawezekana walimhitaji Mourinho kwa ajili ya kushinda mataji bila ya kujali aina ya soka ambalo watacheza.

Hata hivyo ndio kwanza walikuwa wanaondoka Top Four ya Ligi Kuu ya England na hii ilikuwa na maana kwamba mambo yote mawili yasingewezekana. Isingewezekana kutwaa ubingwa wa England wala wa Ulaya.

Hatimaye waliamua kuchukua maamuzi magumu baada ya uchunguzi wao wa muda mrefu kwa Mourinho. Nadhani baada ya kuondoka Porto mwaka 2004 na kwenda Chelsea, tunaweza kusema Spurs ndio timu ndogo zaidi iliyowahi kumfukuza Mourinho. Hapa tunaona mwisho wake.

Jose ameendelea kuwa yuleyule tu. Ameendelea kuwa na tabia zile zile ambazo zilim-fukuzisha Chelsea kwa mara ya pili na kisha

zikamfukuzisha Manchester United. Ameendelea kulaumu kila kitu kasoro kujilaumu mwenyewe.

Leo ataamka atalaumu waamuzi, kesho atamlaumu kocha wa timu pinzani, keshokutwa atashambulia wachezaji wake. Hakuna siku ambayo atabeba uwajibikaji wa kipigo kama ambavyo makocha wengine wameendelea kufanya kokote duniani.

Mwisho wa siku lazima mchezaji mmoja staa awe mhanga wa Mourinho. Popote anapokwenda lazima atasaka mchawi. Aliporudi Chelsea alimtoa kafara Juan Mata. Alipokwenda Manchester United akamtoa kafara Paul Pogba. Akiwa na Tottenham aliamua kuwatoa kafara Dele Alli na Danny Rose.

Kikubwa katika wote hawa ni ukweli kwamba Jose lazima atawatoa kafara watu ambao wanapenda kucheza soka la kushambulia halafu yeye anaona hawana msaada katika ukabaji. Jose anaweza kwenda Manchester United akadai kwamba Bruno Fernandes hafai. Hataangalia mchango wake katika ushambuliaji, ataangalia mchango wake katika ulinzi.

Wenzake kina Jurgen Klopp wanaiangalia zaidi timu inavyokwenda mbele na kumnyanyasa adui huku ikisifika ukweli wa kwamba ni timu bora duniani. Jose haangalii hilo kwanza. Anaangalia ni namna gani atazuia kwa unyenyekevu mkubwa. Wachezaji wakubwa katika klabu zote alizopita huwa hawana raha na akili ya Jose. Sawa ni mshindi, lakini wachezaji wanapenda kujitanua zaidi na kujiona wababe. Jose anaingiza akili ya timu ndogo katika wachezaji wanaocheza timu kubwa.

Hapo zamani alikuwa anafanikiwa, lakini kwa sasa hafanikiwi. Mwenyewe anadai kwamba wachezaji wa kileo ni tofauti na wale kina Claude Makelele. Anaweza kuwa anasema kweli, lakini ukweli ni kwamba dunia inabadilika na Jose anashindwa kwenda nayo sambamba.

Nadhani tumeuona mwisho wake. Sijui ataibukia wapi lakini baada ya kufukuzwa katika klabu tatu za mwisho Chelsea, Manchester United na Tottenham sidhani kama soko lake litaenda juu tena. Wakubwa wote watasita kumchukua.

Labda ni wakati mwafaka kwake kufundisha katika timu ya taifa ya Ureno baada ya michuano ya Euro 2020. Labda ni wakati mwafaka kwake kwenda Marekani. Anaweza kuibuka tena katika klabu yenye hadhi ya Tottenham? Sina uhakika.

Anaweza kuibuka katika klabu nyingine kubwa Ulaya? Sina uhakika. Wakubwa huwa wanaambiana hawa. Na wengi watahoji kwanini anafukuzwa kwa sababu zilezile kila anapokwenda? Inawezekana tumeuona mwisho wa mmoja kati ya makocha bora zaidi duniani.