Prime
Okello alivyotikisa usajili Yanga, CAF hayumo…
Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Allan Okello akifanya mazoezi. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Mbali na mafanikio ya klabu, ana uzoefu wa mashindano ya kimataifa baada ya kuichezea Vipers na KCCA FC katika michuano ya kimataifa, sambamba na kuitumikia timu ya Taifa ya Uganda katika mechi 36, akifunga mabao sita na kutoa pasi 10 za mwisho.
Dar es Salaam. Januari 12, 2026 macho na masikio ya wapenzi wa soka hapa nchini yalikuwa bize kusubiri ni mchezaji gani ambaye atatambulishwa na Klabu ya Yanga baada ya timu hiyo kutoa taarifa hapo awali kuwa itamtambulisha mchezaji majira ya saa 5:00 usiku.
Hakukuwa na mwingine aliyetambulishwa usiku huo zaidi ya Allan Okello ‘Star Boy’ kutokea katika Klabu ya Vipers ya nchini Uganda ndiye ambaye alitangazwa rasmi kujiunga na Wananchi, Yanga. Inadaiwa kuwa Yanga imelazimika kutoa Dola 300,000 sawa na Sh740 milioni ili kukamilisha usajili wa kiungo huyo anayejulikana kwa umahiri wa kutumia mguu wa kushoto.
Ubora na uzoefu
Okello ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza kwa ufanisi katika nafasi zaidi ya moja uwanjani, na kutoa mchango muhimu kwa timu iwe kwa kufunga mabao au kutengeneza nafasi za mabao. Anaweza kupangwa kama winga wa kushoto au kulia, lakini pia hucheza kwa ufasaha zaidi katika nafasi yake anayoimudu vyema ya kiungo mshambuliaji.
Kwa muda mrefu amekuwa na kiwango cha juu, jambo linaloonekana wazi kupitia takwimu zake. Msimu huu tayari amehusika katika mabao matano ndani ya mechi saba za Ligi Kuu ya Uganda alizoichezea Vipers, akifunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mwisho. Katika msimu uliopita, Okello alihusika moja kwa moja katika mabao 23 ya Vipers kwenye Ligi Kuu ya Uganda, akifunga mabao 19 na kupiga pasi tatu za mabao, mafanikio yaliyomfanya kuibuka Mfungaji Bora wa ligi hiyo.
Mbali na mafanikio ya klabu, ana uzoefu wa mashindano ya kimataifa baada ya kuichezea Vipers na KCCA FC katika michuano ya kimataifa, sambamba na kuitumikia timu ya Taifa ya Uganda katika mechi 36, akifunga mabao sita na kutoa pasi 10 za mwisho.
Nidhamu
Okello ni mchezaji anayejitofautisha kwa nidhamu ndani ya uwanja, hali inayothibitishwa wazi na takwimu zake.
Akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Uganda, hajawahi kuonyeshwa kadi yoyote, huku katika soka la ngazi ya klabu akionyesha nidhamu ya hali ya juu zaidi kwa kutowahi kupewa kadi nyekundu na kuonyeshwa kadi za njano tatu pekee tangu aanze kucheza soka la ushindani hadi sasa.
Hachezi Ligi ya Mabingwa Afrika
Yanga italazimika kusubiri hadi msimu ujao ndipo iweze kumtumia Okello katika michuano ya Kimataifa, kwani kwa msimu huu hana sifa ya kucheza mashindano hayo baada ya msimu huu kuichezea Vipers katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mashindano ambayo Yanga nayo inashiriki.
Mazingira yalimshinda Algeria
Okello anakabiliwa na changamoto ya kuzoea mazingira mapya ya ugenini, hali ambayo imekuwa tofauti na alivyokuwa akionekana katika soka la nyumbani nchini Uganda. Hii ni mara ya pili kwa kiungo huyo kucheza nje ya mipaka ya Uganda. Mara ya kwanza alijaribu bahati yake nchini Algeria akiwa na Paradou AC, alikodumu kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kurejea nyumbani baada ya kushindwa kuhimili mazingira ya soka la Algeria lakini kwa sasa anaweza kuhimili mazingira ya Tanzania kutokana na ukaribu pamoja na kufanana kwa mazingira na hali ya hewa ya Afrika Mashariki ukilinganisha na Uarabuni ambako mara nyingi kumekuwa na baridi sana.
Avunja rekodi ya usajili
Baada ya Yanga kukamilisha uhamisho wa Okello, timu ya Vipers kwa sasa imevunja rekodi ya usajili ya kikosi chake na kuivuka ile iliyokuwa inashikiliwa na Cesar Lobi Manzoki. Okello amekamilisha usajili huo baada ya mazungumzo ya pande zote mbili kati ya Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na Lawrence Mulindwa wa Vipers, ambapo wawili hao walikutana tangu wiki iliyopita jijini Kampala, Uganda ili kukamilisha dili hilo.
Baada ya dili hilo kukamilika, Yanga imetoa kiasi cha Sh740 milioni ambazo ni Dola 300,000, akiwa ni nyota wa pili ghali kuuzwa na Vipers, baada ya kiungo mshambuliaji, Farouk Miya aliyejiunga na Standard Liege.
Miya aliyejiunga na Standard Liege ya Ubelgiji mwaka 2016, ndiye mchezaji ghali zaidi kuuzwa na Vipers, ambapo kiungo huyo mshambuliaji aliuzwa kwa Sh986 milioni.
Nyota mwingine anayefuatia kwa kuuzwa fedha nyingi ni mshambuliaji, Cesar Manzoki aliyeuzwa China mwaka 2022 na kujiunga na kikosi cha Dalian Professional, ambapo Vipers iliingiza Sh493 milioni.
Kwa maana hiyo, Farouk Miya ndiye mchezaji anayeendelea kushikilia rekodi ya kuuzwa kwa kiasi kikubwa cha fedha akitoka Vipers, akifuatiwa na Okello aliyejiunga na Yanga huku akimpiku pia, Manzoki aliyekuwa akihusishwa na Simba mara kwa mara.
Okello anaungana na nyota wengine wapya waliosajiliwa dirisha hili dogo, baada ya kiungo, Mohamed Damaro aliyetokea katika kikosi cha Singida Black Stars. Wengine ni, Emmanuel Mwanengo aliyekuwa TRA United zamani Tabora United na mshambuliaji, Laurindo Dilson Maria Aurelio 'Depu' raia wa Angola, aliyetua ndani ya kikosi hicho akitokea Radomiak Radom ya Poland, ili kwenda kuongeza nguvu mpya.
Baada ya kujiunga na Wananchi nyota huyo wa Kimataifa wa Uganda sasa atakuwa na kibarua kingine cha kushindania nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kocha, Pedro Gonçalves ambacho kimejaa mastaa wengine wenye uzoefu kama yeye.